Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba iliyoko mbele yetu. Kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, yeye pamoja na wasaidizi wake kwa kazi nzuri. Hotuba yake hii imejaa matumaini mazuri sana kwa wananchi wetu wa Tanzania. Naamini kwa kuwa yumo ndani ya Serikali Sikivu, basi hata haya ambayo sisi Waheshimiwa Wabunge tunachangia, atayachukulia kwa uzito unaostahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nitaupeleka katika huduma za watoto yatima, nitazungumzia kidogo suala la maiti na nilikuwa nizungumzie Kampeni ya Nyumba ni Choo, lakini bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge aliyepita ameshalizungumzia. Hata hivyo, kama nitapata nafasi, naweza nikaligusia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri na pia nimepata nafasi ya kuisoma tena. Kuna maeneo ambayo yananisikitisha kwamba hotuba hii haijataja kwa uwazi kabisa watoto yatima. Hili ni eneo ambalo, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ameligusia, watoto ambao wapo katika mazingira magumu, lakini nadhani ingekuwa busara tukawataja, kwa sababu nchi hii sasa hivi ina watoto yatima ambao wametokea tu katika lile kundi ambalo wazazi wao wamefariki kwa HIV, wako takribani 1,400,000 ukiachilia wale wengine ambao wazazi wamefariki wao katika magonjwa mengine na acts of God wameondoka, yawezekana kuna watoto wengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hii, naomba sana Mheshimiwa Waziri afikirie. Yawezekana Taifa hili sasa linahitaji kuwa na sera specific kwa ajili ya watoto yatima. Kwa nini nasema haya? Nasema hivi kwa sababu najua kuna Sera ya Maendeleo ya Watoto ile ya mwaka 2008, lakini kutokana na hali halisi ambayo sisi Waheshimiwa Wabunge tunakumbana nayo katika Majimbo yetu, utaona ni hakika watoto yatima wanahitaji watu wa kuwasemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwishoni mwa wiki nilipata nafasi ya kutembelea vituo vinne vya kulelea watoto yatima katika Jimbo langu la Kinondoni. Nilikwenda katika Kata ya Hananasifu, nikaenda kwenye Kata ya Mzimuni, Kata ya Tandale na Ndugumbi. Niliyoyaona kule yawezekana kabisa yanaakisi hali ya watoto yatima katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa sababu hii napenda niwapongeze kwanza wale wananchi ambao wamejitoa, kwa sababu hawa ni wananchi wa kawaida na wengi wao ni akina mama ambao ni watu wazima, lakini wamejitoa kwa hali na mali. Wengine wana watoto 50, wengine wana watoto 200, wengine wana watoto 300, wanategemea wafadhili na wana kazi ngumu sana ya kuwapeleka shule watoto hawa, kuwafundisha tabia njema na utashangaa watoto wanajua dini, wana tabia njema pengine tofauti na hata watoto wetu ambao wako majumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia ni kwa jinsi gani Serikali inaweka mkono wake pale? Hili mtanisaidia Mheshimiwa Waziri, ni kwa jinsi gani Serikali inasaidia watoto yatima ambao wanalelewa katika mazingira ya kijamii. Labda niseme kitu kimoja, kuna hali ambayo badala ya wale watu wa ustawi wa jamii kusaidia na kuwapa moyo wale ambao wamejitolea, kuna wakati mwingine wanawakatisha tamaa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nilifika katika kituo kimoja kinaitwa cha Bi Maunga pale Hananasifu; katika kukagua kagua nilikuwa namwuliza kuhusu upakaji wa rangi, maana kuna baadhi ya sehemu hazijapakwa rangi vizuri. Akasema suala hili pia liligusiwa na watu wa Ustawi wa Jamii, lakini badala ya kunisaidia, wamenitisha. Wanasema kama sikupaka rangi, watakifunga kile kituo. Kauli kama hizi siyo nzuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya, mfano wakifunga kile kituo, wale watoto 100 wanakwenda wapi? Sasa lazima wafanyakazi wetu wa Ustawi wa Jamii wawe ni vijana au wawe ni akina mama au wawe ni watu wa rika lolote lile, wajifunze kuwa na customer care nzuri sana wanapozungumza na watu kama hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na changamoto nyingine na wengi wameizungumza, sasa sijui katika Majimbo mengine; watoto hawa wakipelekwa shule kuandikishwa, wanahitajika kuwa na Birth Certificate (zile hati za kuzaliwa) ambazo watoto wale ambao ni yatima waliopatikana katika mazingira ambayo mengine ni magumu, hawana hizo hati. Wanapata matatizo, hawapelekwi shule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iangalie katika zile haki za Watoto, mojawapo ni haki ya kuendelezwa; haki ya elimu. Naiomba Serikali itoe kauli, naye atafute njia rahisi ya kuweza kusaidia watoto hawa kuweza kupata hati za kuzaliwa. Pale ambapo itakuwa na ugumu, angalau waanze kuruhusiwa kusoma huku taratibu nyingine zikitafutwa ili waweze sasa kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, wakati nazunguka nilikutana na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanaosoma Saikolojia, walikuwa wanakwenda pale kuwapa nasaha wale watoto ambao wanajitambua. Jambo lile limenifurahisha sana. Kwa hali hiyo, naiomba Serikali itoe wito kwa vijana wanafunzi ambao wanasoma katika vyuo kama hivi wakipata nafasi watembelee maeneo ya yatima, wazungumze nao na kuwapa encouragement kwamba kuwa yatima siyo mwisho wa maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja la mwisho ambalo napenda nilizungumze kuhusu huduma za maiti. Huduma za maiti kule kwetu Kinondoni wakati tunafanya kampeni lilikuwa ni suala moja zito sana. Maneno ni kwamba, watu wanapofariki miili haitolewi mpaka watu walipie. Sawa, ni haki kabisa kulipia, lakini jambo kama hili linatakiwa Serikali ilitolee mwongozo ambao utasaidia kupunguza machungu ya watu wanaofiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuruhusu watu wakapewa miili ile, yaani maiti wakaenda kuzika na kukawa na utaratibu mwingine wa kuweza kuzipata zile fedha, ama njia nyingine zozote ambazo zinawezekana. Ila lugha ambayo ilikuwa inatumika jamani, ni kwamba Serikali inatuuzia maiti. Maiti wanauzwa! Kwa maana huwezi kumpata maiti mpaka ulipe pesa. Nilikuwa naomba tu Serikali iweze kutafuta njia ambayo inaweza ikasaidia kuondoa machungu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)