Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia kwenye sekta hii ya afya ambayo ni muhimili wa amani na utulivu na maendeleo watu wenye afya watafanya vizuri kwenye shughuli za kilimo shughuli za elimu shughuli za ujasilliamali na nyinginezo. Na mimi kwa kuanza niungane na Wabunge wote waliopongeza juhudi za Serikali na Wizara ya Afya mahususi katika kuimarisha sekta hii ya afya kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, karibu kila Mbunge yeyote aliyeko hapa na asiyekuwepo anapotoka kuna athari ya jambo jema lililofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na sekta ya TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natoka Mkoa wa Mara, kule kuna Ushahidi wa jambo kubwa ambalo Awamu ya Tano na ya Sita watakumbukwa na wananchi wa mara hususani juu ya hiyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali ile ina historia ndefu ujenzi wake kwanza waliweka jiwe la msingi mwaka 1975, ujenzi ukaendelea mpaka mwaka 1987 ukasimama lakini kwa maamuzi yenye tija ya mpendwa wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwenyezi mungu amweke roho yake mahala pema peponi 2018/2019 waliweza kufanya uhamuzi wa kutoa zaidi ya bilioni 15 kwa ajili ya kuhakikisha hospitali ile inakamilishwa. Na sote sasa tunaona hospitali ile inapendeza bahati nzuri imejengwa kwenye mwinuko wa Mlima Mkendo ina vutia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa, Serikali ikamilishe majengo machache yaliyobaki ili huduma muhimu za rufaa ngazi ya mkoa ziweze kuanza kutolewa kwa ukamilifu. Lakini hilo la muhimu kwa majengo yaliyokamilika ambayo yanaweza kuanza kutoa huduma za rufaa ngazi ya mkoa, ni vizuri tupate vifaa tiba majengo yale ukifika utakuta maeneo mengi yanayotakiwa kuwepo vifaa tiba hakuna vifaa tiba ndio maana hadi sasa huduma zinaendelea kutolewa kwenye hospitali iliyokuwa inatumika kimsingi ni hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni watumishi Wabunge wengi waliozungumza wameonyesha upungufu wa watumishi maeneo yote sasa na huku ambako tumejenga hospitali hizi mpya, ni vizuri kuwe na mkakati maalum kama wa ajira kwa ajili ya watumishi wa kada zote za sekta za afya zinazohitajika. Wakiwemo madaktari, madaktari bingwa, wauguzi wafamasia wataalam wa usingizi nakadhalikadhalika. Kwa hospitali hii ya rufaa ya Mkoa wa Mara ina upungufu mkubwa sana, niombe wizara kwa jambo jema mlilolifanya likamilishwe kutuletea wataalam wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ninalotaka kuzungumza kwenye sekta ya afya ni mafunzo ya watalaam wa afya hususani madaktari bingwa, uzoefu unaonyesha kuwa hospitali kubwa za mijini hasa majiji makubwa ya Dar es salaam, Arusha, Mbeya, Mwanza, Tanga nakadhalika, wanaomadaktari na madaktari bingwa wakutosha, kuliko mikoa inayoonekana ni ya pembezoni, kiasi kama mkoa wangu wa mara. Nakumbuka miaka michache iliyopita wizara ilifanya uhamuzi wa kufanya rationalization ya kuhamisha bahadhi ya madaktari bingwa kutoka jijini Dar es salaam, na kuhamishia mikoa ya kusini na mikoa yetu kama kule Simuyu nakadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ilivyoonekana wataalam bingwa waliokwisha zoea Dar es Salaam si rahisi sana kukubali kwenda kufanya kazi kwenye mikoa hii ya pembezoni. Taarifa nilizonazo wengi wa madaktari wale waliamua ku-resign waliamua kuacha kazi na kurudi Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri sasa kwenye hilo tufanyaje, ninadhani wakati umefika sasa tuzisaidie hizi Hospitali za Rufaa za mikoa huko zilizo wawe na utaratibu wakuwaendeleza watumishi wao mabingwa, kama mtu ameshazoea kuwa Musoma kule ukienda ukampeleka ni rahisi kurudi lakini aliyezoewa Dar es Salaam ukwamwambia nenda Musoma anaona kama vile katupwa hivi na wengi wanasema nimetupwa Mara nimetupwa Mtwara, nimetupwa Katavi wakati kule kuna watanzania wanaohitaji huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwenye hili naomba niwapongeze of course Katibu Tawala wetu wa Mkoa wa Mara pamoja na medical officer incharge huyu Dr. Johakimu Eiyembe na RMO wake kwa uhamuzi wakutraini maafisa wataalam wao wanne. Lakini kwa uamuzi ule wa kutumia mapato yao ya ndani wizara ikaamua kuwasaidia kuwasomesha mmoja vitu vya aina hii vikiendelea vitatupunguzia mahitaji makubwa ya madaktari bingwa kwenye hizo hospitali za pembezoni. Kwa hiyo, hili niwasifu Wizara kwa kulifanya kwa ajili ya wataalam wetu kutoka kule Mkoa wa Mara, lakini liendelee kufanyika mara kwa mara ili kujenga uwezo wa hospitali hizi za pembezoni pia kupata wataalam wanahitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni makusanyo ya mapato ya ndani, ukipitia taarifa ya wizara ya utekelezaji utaona kwamba kwa sehemu kubwa, taasisi za Wizara hazikusanyi vya kutosha mapato yao ya ndani. Na nimeona zipo taasisi chache kwa idhini yako nizitaje zimefanya vizuri sana. Hospitali ya Mloganzira kwa mfano imekusanya zaidi ya asilimia 99 ya malengo yake lakini ipo Hospitali ya Benjamin Mkapa hii imevuka malengo kwa asilimia 118 ambako imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 13, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imekusanya zaidi ya asilimia 74 sawa na bilioni 45, taasisi ya chakula na lishe asilimia 73 lakini taasisi nyingine zinazobaki zinasuasua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili pia lipo kwenye hospitali za Rufaa za Mkoa, pia kuna mapungufu ya ukusanyaji, ushauri wangu kwenye hili wizara iweke utaratibu wa watu kwenda kujifunza kwenye hizo hospitali zilizofanya vizuri ili uzoefu huu usaidie kuimarisha mapato ya ndani kwenye hospitali zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkona hoja nawatakia heri katika utekezaji wa majukumu yao. (Makofi)