Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri, lakini pili naipongeza Kamati kwa ushauri na mapendekezo yake mazuri; naunga mkona hoja zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwanza kwa kumteua Mkuu mpya wa SUMA JKT, sisi tuliokuwa kwenye Kamati ya Nishani na Madini mwaka jana tumeona kazi nyingi sana alizozisimamia na nina imani kwamba baada sasa ya kupewa rungu mambo yatakuwa mazuri zaidi, Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napenda kushauri kuhusiana na suala la mfumo, mimi nitazungumzia sana kwenye JKT. Mfumo wa JKT kwa mzamo wangu mimi nikitizama JKT natazama kama uchumi mkubwa sana kwenye Taifa letu, lakini ukiangalia jinsi SUMA JKT inavyochagua vijana wa kwenda kujiunga na JKT inaweka vigezo vya elimu tena ina division na point na wanapoenda kule wanasoma wengine mpaka miaka mitatu wakiwa na malengo haya haya kwamba nitaenda jeshini na kule jeshini wanajua wanavyochagua baadhi ya watu wachache wanaenda, hao wengine wote wanarudi nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa shida inakuwa moja, sisi Wabunge humu wengi ikifika kipindi cha vijana wanahitajiwa JKT karibu kila Mbunge ana message za wazazi wanaomba watoto wao waingie kule, lakini wakimaliza tena wakirudi nyumbani, shida inakuwa tena kwa Mbunge yule yule tusaidie kupata ajira.
Sasa mimi ushauri wangu, nilikuwa napenda kushauri kwamba kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana JKT, lakini wangeondoa masharti ya elimu, wakachua vijana wote wenye uwezo kwa sababu ninavyoitazama JKT ni kama sehemu ya kwenda kufundishwa maisha halisi ambayo tunaweza kuyafanya hata sisi ambao hatukupata elimu kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mtu anaenda kufundishwa uselemala, anaenda kufundishwa kulima, anaenda kufundishwa kazi za kila siku, mimi najiuliza kama wanapanda watu cheo kwa kusimamia kazi za ujenzi, inakuwaje mtu unafundishwa JKT, unakaa miaka mitatu, unarudi tena na kusubiri kuajiriwa kwa shilingi 120,000, tunawafundisha vitu gani kule yani kama mgechukua watu wa darasa la saba ambaye anajuwa mimi nikitoka huku na taaluma yangu ya ujenzi, nikitoka shuleni ni kwenda kuomba kibarua nilipwe shilingi 20,000 kwa siku ambayo nitapata shilingi 360,000. Kwa hiyo mimi nilikuwa nadhani, tunatengeneza bomu kubwa sana na ndio maana tunaanza kuona vijana wanaandamana, wanakiukwa masharti ya kijeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe tu kwamba muone namna wenzetu wa JKT muondoe lile sharti la elimu, mchague vijana kwa uwezo na watu ambao watawaelewa na ninyi muonekane mnafundisha watu, wanaporudi huku wawe na kazi zao za kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Waziri, lakini pia nipongeze na Jeshi. Niliwahi kuchangia hapa nikazungumza suala la Mererani kwamba kulikuwa na upekuaji ambao haukuwa mzuri, lakini nikupongeze sana Waziri na Jeshi kwa sababu ule upekuaji tena hakuna. Umerudi upekuaji wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii ndiyo maana kila siku mimi nasema nidhamu ya Jeshi ni kubwa sana na ninadhani kuna watu walituelewa vibaya, lakini nadhani ninyi mlivyokwenda kuchunguza mliona hiki kitu kinafaa na sasa mmeondoa na mnakagua vizuri na watu hawana kelele tena na kudhalilisha Jeshi letu ambalo sisi tunaliheshimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nilitoa mapendekezo; mimi nashughulika na mambo ya madini, kwenye taaluma ya assessment ile wanayofanya pale niliomba, mimi naamini sana Jeshi, hebu chukueni vijana 100 muwapeleke wakasome, hawamalizi miezi sita, warudi wapewe hizo nafasi. Hawa waliopo bado tunapigwa na wanajeshi wako pale pale. Kwa hiyo, nilitoa ushauri, kama utaufanyia kazi nadhani baadaye utakuja kuona mafanikio kwa sababu mimi binafsi nina imani kubwa sana na Jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa ushauri na ninatoa ushauri kwa upole sana. Mimi kama ninavyosema, naliheshimu sana Jeshi la Wananchi, lakini sijui ni kwa nini wanajeshi wetu tumewaweka kama tumewasahau kidogo kwenye suala la makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua Serikali inajitahidi kujenga, lakini mkarabati na za zamani. Hebu jaribuni kupita tu, mimi nachukua mfano mmoja, pengine wenzetu hawa wanajeshi hawana watu wa kuwasemea humu ndani, ukipita Mwenge pale unamuona mwanajeshi ametoka amevaa smart, anang’aa, angalia nyumba anayotoka. Nenda Mwanza, nenda kila sehemu, jamani hata kukarabati tu kupiga rangi kweli Mheshimiwa Waziri? Hata wewe mwenyewe ungeishi hiyo nyumba halafu unatoka nje unaendesha V8! Hii siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Jeshi letu linasifika Kimataifa, hata Wachina, Wazungu, wakija waone mwanajeshi anatoka kwenye nyumba nzuri. Tuna maghorofa, tuna majengo mazuri, kupaka tu rangi? Mheshimiwa Waziri, mimi kwenye shilingi kuhusiana na uchafu kwa kweli kwanza mimi niko jirani nao pale Mwenge, sitakubaliana nalo kabisa kama hutokuja na maelezo mazuri. Ninapenda uje na maelezo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niliona nichangie tu hayo kwa ufupi kwa sababu Jeshi letu linafanya kazi nzuri na mimi nalipenda. Nilitaka nimshauri Waziri kwa hayo machache, nakushukuru sana. (Makofi)