Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru sana kuniruhusu nichangie wa mwisho.
Kwanza nianze na pongezi, naipongeza sana Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lakini pia niwapongeze viongozi wa Jeshi. Nianze na ndugu yangu Jenerali Mabeyo, lakini pia Mnadhimu Mkuu Jenerali Yacoub Mohamed, Makammanda wote wa Jeshi letu. Wamefanya kazi kubwa kuituliza nchi baada ya tukio kubwa hili la kupotelewa na Mheshimiwa Rais Marehemu Magufuli.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Almas Maige, huyu Mnadhimu Mkuu wa Jeshi ni Luteni Jenerali maana nafikiri nchi inakuwa na Jenerali mmoja halafu wengine wanakuwa ni Majenerali wastaafu.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunisahihisha. Luteni Jerenali Yacoub Mohamed. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo mimi nimejielekeza kwenye malengo ya Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na nianze na lengo la kwanza, kuwa Jeshi dogo lenye ufanisi mkubwa. Jeshi hili litakuwa na ufanisi mkubwa kama litapewa vifaa na zana hasa zana za EW (electronic warfare). Vita imeacha kupiganwa sana sana kwa mizinga na bunduki, lakini electronic warfare au vita vya elektroniki vinafanya kazi imara. Jeshi letu litakuwa na nguvu sana sana kama litapewa hela za kutosha kununua vifaa na zana hizi za EW. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye utafiti ambao ni lengo la Wizara lengo la tatu (c ). Hapa ndipo tunapata taabu sana na Jeshi letu, hawana hela za kufanyia utafiti. Jeshi litakuwa la kisasa, usasa ule na weledi utatokana na tafiti ambazo wanazifanya wao wenyewe. Huko tulikopita Jeshi lilitakiwa liandike andiko lipeleke COSTECH likasome, ndiko hela zipo, halafu wazipe Jeshi. Andiko la Jeshi ni la siri, haiwezekani raia wasome andiko la Jeshi wafanya maamuzi ya kuwapa hela. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iweke hela za utafiti wa Jeshi kama kweli tunataka amani ya nchi hii na utendaji wa Jeshi ufanyike. Wapeleke hela Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa au moja kwa moja Ngome. Wafanye utafiti wa silaha, utafiti wa maisha ya watu ili waweze kuwalinda. Utafiti haufanyiki na matokeo yake Jeshi hili haliwezi kuwa dogo likawa na nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongelee eneo (d) kuimarisha Jeshi la akiba. Jeshi la akiba zamani tuliliita mgambo lilifanya kazi kubwa sana wakati wa vita vya Kagera, mimi nilikuwepo. Jeshi la akiba ni jeshi muhimu sana. Sasa hivi Wizara haina hela ya kuendeshea au kulifanya Jeshi hili liendelee kuwepo. Mafunzo na mazoezi ya jeshi la akiba ni muhimu sana, hela hakuna. Mimi nashauri Serikali iipe Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi lenyewe hasa ili waweze kuendeleza uwepo wa jeshi la akiba. Wamelitaja kama ni lengo la tatu katika malengo ya Wizara. Napendekeza, ni muhimu sana jeshi la akiba liendelee kuwa imara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la JKT; JKT imefanya kazi kubwa sana ya kuwafanya Watanzania wawe wazalendo. Suala hili naona kama lililegalega huko nyuma mpaka Jeshi lenyewe la JKT likaacha kuchukua vijana. Limeanza kuchukua vijana sasa hivi, lakini hawatoshi. Wafanyakazi, Mawaziri walioko leo madarakani ni watendaji wazuri wa Serikali, wana uzalendo kwa sababu walipita JKT. Katikati hapa vijana walianza kutawanyika bila kueleweka wewe ni Mtanzania au sio Mtanzania kwa sababu hawakuwa na uzalendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Kujenga Taifa ndicho chombo pekee kinachojenga uzalendo kwa Watanzania. Naomba hela zipelekwe ili watu wanaotakiwa kwenda kupita JKT wapiti, wale wa kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea. Mimi nasema uzalendo ndiyo chombo muhimu sana. Leo hii tungesema tupigane vita vya Kagera tungepata taabu sana. Mwaka ule wa 1978 wanajeshi wanasimamisha magari wanapeleka front line, mstari wa mbele. Leo mtu atasema nilipeni kwanza hela zangu ndipo niwapeni gari langu, uzalendo umepungua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chombo pekee cha uzalendo ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Naomba sana Serikali ifikirie kurudisha hela nyingi kwenye chombo hiki ambachi kimetusaidia sana kuleta amani na utulivu nchini. Watu wakiwa wazalendo hawawezi kutoa maneno ya misonge misonge kwa sababu watasema sisi ni Watanzania. Tunasema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee. Inaendelea kwa sababu kuna uzalendo rohoni, hawasemi tu mdomoni, kazi iendelee, hapana! Tunasema kwa sababu tunasema kweli na tumefundishwa na JKT. Kwa hiyo, Jeshi la Kujenga Taifa ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sasa eneo la mwisho kuhusu SUMA guard, wanafanya kazi nzuri sana lakini ni sehemu ya sekta ya ulinzi binafsi, ni wanachama pia wa Chama cha Sekta Ulinzi Binafsi (TSIA). Liko tatizo, SUMA guards leo wanapewa kazi bila zabuni. Ni sehemu ya kazi za makampuni ya ulinzi binafsi pia, lakini wao wanapewa kazi bila zabuni. Lakini pia wanaomba zabuni kwenye kazi nyingine hizi. Kumekuwa na utata kidogo, kuna kusukumana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya ulinzi binafsi inazimika kwa sababu kazi zote za Serikali ambazo walikuwa wanalinda na wao pia wanapewa JKT, lakini na wao pia ni kampuni za ulinzi. Sasa hivi kumekuwa na mkorogano zaidi, hata Jeshi la Magereza nao wameanzisha, wanaita SHIMA. Mkorogano huu unaleta migongano na kuua ufanisi hasa wa sekta ya ulinzi binafsi.
Mimi nashauri SUMA guards washiriki zabuni, lakini pia waoneshe kwamba wanafanya kazi kweli sehemu ya ulinzi binafsi. Sasa ilivyo kuna upendeleo mkubwa huu ambao unavuruga mfumo mzima wa sekta ya ulinzi binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Nimemaliza.
NAIBU SPIKA: Ameshamaliza muda wake. (Kicheko/ Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.