Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nijumuike na wenzangu kumshukuru Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu. Lakini pia nichukue fursa nayo kumshukuru Waziri wa Ulinzi, kwa kweli nina kila sababu ya kuzungumza na Waziri wa Ulinzi jinsi anavyojiweka kwetu, tunavyozungumza naye na ni Waziri ambaye yupo tayari kuzungumza na kila Mbunge mmoja wapo iwe nje au ndani, kwa kweli ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze kwenye masuala ya barabara ya ulinzi. Katika mipaka yetu inawezekana tukazungumza suala la ulinzi kiujumla, lakini suala la ulinzi kama hatujalipa kipaumbele inawezekana majeshi yetu tukawapa kazi kubwa sana kwenye ulinzi. Mfano nataka nizungumzie mpaka wa Mtwara na Msumbiji tuna barabara hapa ya ulinzi ya kilometa 300; unatoka Mtwara hadi Tunduru. Barabara hii kwa hali jinsi ilivyo haiwezi kupitika kwa urahisi iwapo litatokea janga lolote la kitaifa au la uvamizi hawa wanajeshi wetu hawawezi kufika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu nadhani Waziri wa Ulinzi wafanye mazungumzo na Waziri wa Ujenzi barabara ile ya ulinzi ambayo iko madhubuti kabisa kwa ajili ya ulinzi wa mpaka wa kusini iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamezungumza sana kuhusu migogoro ya ardhi, kuhusu makambi ya majeshi yetu; kule kwangu ni sehemu pale Mtwara ni sehemu ya waathirika wa makambi hayo. Ukienda kwenye Kata ya Ufukoni ina watu takribani zaidi ya 12,000 lakini katika kata hiyo watu 12,000 kuna watu zaidi ya 4,000 wana mgogoro na Kambi ya Jeshi, na hili ni lazima nilizungumze kwa sababu kwenye mgogoro ule utawakuta wanajeshi/makamanda wako wana viwanja na wamejenga nyumba za kisasa. Kwa hiyo, rai yangu nataka nizungumze kwamba niombe muda wa bajeti hii ikishaisha tumemaliza hili Bunge ikimpendeza Waziri twende tukatatue mgogoro ule haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima tunaozungumza vijana wetu wa JKT; wenzangu wamezungumza sana, vijana hawa wa JKT tumekuwa tunawapa mafunzo na mafunzo haya wanayopewa ni mafunzo ya kijeshi. Lakini nataka nitoe angalizo kwa Serikali, vijana hawa tunapokwenda kuwapa mafunzo ya kijeshi na baadaye tukaendelea kuwaacha idle nje, iko siku hawa watabadilika sasa kuwa watu wabaya ndani ya Serikali yao. Kwa sababu tayari tumewapa mafunzo, lakini tunashindwa sasa kuwatumia kimafunzo sahihi. Nashauri wenzangu wamezungumza sana kuhusu viwanda, lakini wenzangu wamezungumza kuhusu activity nyingi kuhusu vijana hawa. Kama ikikupendeza na Serikali ikiipendeza naomba vijana hawa sasa waandaliwe shughuli mahususi wanapotoka kwenye mafunzo ya jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la ulinzi tukirudi nyuma kwenye historia ya nchi yetu tumepigana vita kule na Uganda, lakini wakati tunapigana vita na Uganda tulifika mahala tukaathirika kama Watanzania na Jeshi letu. Baada ya daraja letu ambalo tulikuwa tuna daraja pale Kagera halikuwa na uwezo wa kuwa na daraja kama daraja. Haya nayazungumza kwenye historia hii, natoa mfano sasa tunazungumza Mtwara na Msumbiji na nimekuwa nikizungumza sana Bunge hili, lakini nimekuwa naishauri sana Serikali juu ya kujenga daraja baina ya Msumbiji na Mtwara kwa pale ambapo tunasema barabara yetu ya ulinzi ya mpaka ule ndiyo inapoanzia basi twendeni sasa tujenge daraja ili jambo lolote litakalotokea kuwepo na unafuu wa kuweza kuboresha jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niendelee kulipongeza Jeshi hili, nalipongeza Jeshi katika nchi zetu za Kiafrika ni jeshi la kwanza ambalo halijayumba na hili lazima tukubaliane kwamba tayari tuna majemedari ambao wamefika mahali wamegeuka kuwa wazalendo ndani ya nchi yao. Lakini ukiangalia kwenye nafasi zao na maudhui jinsi wanavyoishi pale kwangu Mtwara tunazo nyumba za wanajeshi nyumba zile zilijengwa takribani miaka ya 1980.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba zile ukienda kuziona siku ya leo na ukaangalia ukaona kwamba nyumba hizi wanakaa wanajeshi wetu, ni aibu kubwa sana. Niiombe na Serikali twendeni tukazikarabati zile nyumba kwa sababu ufanisi wa jeshi letu, ufanisi wa wafanyakazi wetu lazima wafike mahala wajue yale maudhui wanayoishi kwenye Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nazungumzia wanajeshi kukaa nje ya makambi; mimi nataka niishauri Serikali hawa wenzetu wanafanya mazoezi mazito sana na kwa bahati nzuri asilimia kama 20 ya mazoezi hayo mimi nayafahamu. Lakini wanapojumuika na wananchi ndiyo tunasema hawa ni rafiki sawa na wananchi lakini yako mambo ya msingi ambayo wanajeshi kama wanajeshi kwenye taaluma yao haitakiwi kujichanganya na wananchi. (Makofi)

Sasa hili natoa angalizo kwa Serikali leo tumeona maeneo mengi nasikia jeshi wamempiga mwananchi huko, jeshi wamempiga siyo kwamba wanakusudia kufanya vile kwasababu hawa wanajeshi huwezi kumpeleka jeshi aende akalinde benki siyo kazi yake na siku utakayomchukua mwanajeshi kwenda kulinda benki, inawezekana maudhui ya yeye na mteja yakawa ni mambo mawili tofauti. Kwa sababu siyo kitu ambacho wamesomea au wamejifundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi niiombe Serikali twendeni sasa tuwajengee mazingira ya kuishi kwenye makambi na wale maafisa ambao tunasema maafisa wetu hawakai kwenye makambi wanakaa uraiani, tutengeneze sasa nyumba za kisasa kwa ajili ya kukaa hawa wanajeshi wetu. Suala hili la ujenzi wa nyumba halikuanza jana wala juzi, kwa kumbukumbu zangu kabla sijaingia Bunge hili, lakini mabunge yaliyopita Wabunge wengine walizungumza sana kuhusu ujenzi wa nyumba za wanajeshi. Kwa hiyo na mimi niungane na wenzangu nikuombe Naibu Spika na Serikali kwa ujumla hebu twende sasa tuwaangalie wanajeshi wetu haswa kwenye makazi salama ambayo wanaishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wanajeshi wetu wanafanyakazi kubwa sana na kama Serikali itafika mahala tukatenga bajeti leo tunazungumza kuhusu vijana hawa wanaotoka JKT, wanafanya shughuli gani tunawaacha idle, kama tumeweza kupeleka fedha tukatunga sheria, tukasema sasa tunatoa asilimia 10 kwa ajili ya wajasiriamali kwenye manispaa zetu, kwanini Serikali sasa isijiwekeze tukasema sasa tunaamua sasa tutengeneze kiwanda kimoja kikubwa ndani ya nchi yetu tutafute wabia, lakini hawa vijana wetu kwa sababu wengi wanakuwa wataalam kutoka huko jeshini waende wakafanye kazi kwenye viwanda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii rai naitoa kwasababu hawa vijana wako wengi sana na kila muda tunapowachukua kuwapeleka kule Jeshini kwenye mafunzo reaction yake inakuwa kubwa ya ukomavu wale vijana. Lakini kwenye ukomavu wao hatuwajengei sympathy ya kurudi kule kwenye maeneo wakawa wana uwezo wa kujitegemea. Tutengeneza mazingira, kama tumeelemewa basi twende na njia mbadala sasa ya kufika mahali tukasema sasa vijana wetu hawa tunawatafutia activity yoyote ile ambayo inawezekana wakaweza kuishi na kufanya shughuli zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru na niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)