Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba uniruhusu nimshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu na kuweza kuhitimisha hoja yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe mwenyewe kwa kutupa nafasi hii, lakini nakushukuru sana kwa kuweza kuongoza mjadala huu kwa umahiri na weledi mkubwa, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kurudia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua, kuniamini na kunipa nafasi hii ili niweze kulitumikia Taifa kwa kuiongoza Wizara hii, namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilikuwa na pacha wangu hapa, Mheshimiwa Mwanaidi, utaona kwamba nilikaa kwa utulivu. Unajua ukikaa na mama mambo yanakuwa barabara, sikuwa na pressure, nilikuwa napata ushauri wa kutosha. Kipekee nimshukuru sana, lakini pia nimefanya zoezi la kudumisha Muungano wetu. Ninamshukuru sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata wachangiaji wengi, Waheshimiwa Wabunge 26 kama sikosei wamechangia kwa kuzungumza, nilipata pia michango ya Waheshimiwa Wabunge wawili ambao waliitoa kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda nitumie nafasi hii kuwapa pongezi nyingi sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao, lakini nipokee pia pongezi nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge mmezitoa kwa wingi sana, lakini pia mmewapongeza wenzangu hapa, Jenerali pamoja na timu yake na Wizara kwa ujumla. Kwa hiyo, hizo pongezi nazichukua na ninazifikisha kwa kweli kwa uzito ule ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, niwashukuru mmeonesha dhamira ya dhati ya kuona kwamba Wizara yangu inapata fedha za kutosha na sina mashaka Waheshimiwa Wabunge kwamba mtatupitishia bajeti hii ili twende tukafanye kazi yetu, tukatimize jukumu letu. Kikubwa hapa ni kuwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu maneno yenu yametutia moyo sana, pia mmetupatia maeneo ambayo sisi tukitoka hapa kwa michango na ushauri wenu tunakwenda kuufanyia kazi, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Pinda, amezungumza kwa kirefu juu ya masuala ya ardhi. Lakini ninafikiri nianze na hilo na niongezee kidogo kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge, Mbunge wa Biharamulo umezungumza hapa juu ya eneo la Biharamulo na changamoto zake, na siyo hapa tu, Waheshimiwa Wabunge hawa tumekuwa na mijadala na majadiliano kule nje ya Bunge ili kuhakikisha kwamba changamoto ambazo zipo kwenye masuala ya ardhi tunakwenda kuzitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba nimewasikia, nimemsikia Mheshimiwa Mbunge wa Mtwara, nimekusikia ndugu yangu Mheshimiwa Tabasam kule Sengerema na ulizungumza na kunipa historia ya muda mrefu sana na maeneo mengi kwa kweli yenye mgogoro ni migogoro ambayo ilikuwa imekaa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siiti mgogoro, naona tu kwamba ni changamoto ambazo zilijitokeza kwa sababu maeneo ya Jeshi ni mengi, tunayo maeneo mengi na wakati mwingine wananchi ulifika wakati wakaona labda saa nyingine hatuyahitaji, lakini maeneo yote tuliyokuwa nayo tunayo kwa ajili ya kuona kwamba lile jukumu la ulinzi linakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimewasikia Waheshimiwa kule Kyerwa na Katavi kwa Mheshimiwa Taska Mbogo, mchango wa maandishi wa Mheshimiwa Martha Mariki naye alizungumza kuhusu mgogoro ambao upo. Lakini kimsingi ninataka niseme tu kwamba katika maeneo yote tunakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo hili pia tulisikia kuhusu kule Kaboya kama sikosei, lakini pia tulikuwa tumezungumza hapa na ananitazama hapa Mheshimiwa Dkt. Bashiru kwamba ile issue ya maeneo yale, nitakwenda lakini taarifa ambazo zipo ni kwamba pia wenzetu wa milki, kwa sababu tulianzisha Kitengo cha Milki ili kurahisisha uratibu na kuhakikisha kwamba changamoto ambazo ziko kwenye maeneo ya ardhi tunakwenda kuzimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kuishukuru Serikali, tumepokea fedha kwa ajili ya kuifanya ile timu yetu ambayo inakwenda kuhakiki maeneo yetu ambayo yana changamoto, inakwenda kufanya kazi. Na nikuhakikishie tu kwamba kati ya maeneo 94 yaliyokuwa na changamoto likiwepo eneo ambalo Mheshimiwa Esther Matiko amelizungumza, lenyewe limefikia katika hatma yake, fedha zipo, wataalam wamekwenda, tunakwenda kulimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na maeneo yako mengine kama 44 hivi ambayo kwa sasa timu yetu ya milki imepata fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya kwenda kumaliza mgogoro katika maeneo haya. Kwa hiyo, niseme maeneo yote Waheshimiwa Wabunge nimewasikia yaliyokuwa na changamoto ya migogoro hii ya ardhi, tutakwenda kuimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba nimepokea pia ombi la kwenda kwenye maeneo kadhaa, na baada ya Bunge lako hili tutakwenda kule na mimi napenda nikienda katika maeneo haya niende wataalam wakiwa wamemaliza changamoto zilizokuwepo kwenda kuwatia moyo wananchi wetu na kuhakikisha kwamba tunasonga mbele. Na tunafanya zoezi la kuhakikisha kwamba tumekwenda kutengeneza maeneo haya yawe na hati miliki. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Pinda kwa ufafanuzi wake kama alivyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie kidogo maeneo ambayo Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imetoa mapendekezo hapa. Niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ni sikivu, na mimi ninaamini kabisa Waheshimiwa Wabunge Kamati hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama watakubaliana na mimi kwamba tumekuwa na mijadala mizuri ya kuhakikisha kwamba tunafanya Jeshi letu linakwenda kutekeleza majukumu yake kisawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote ambayo wameonesha kwenye ripoti, yako mengi ambayo tayari tumeshachukulia hatua nzuri, yako kwenye hatua nzuri na yako mengine ambayo yako kwenye mipango mizuri ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kuyatekeleza. Ninaamini kabisa maelekezo na ushauri wa Kamati utakwenda kutuboreshea utendaji kazi wetu katika Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kueleza machache yaliyoko kwenye ripoti ya Kamati, ninaomba nitoe ufafanuzi kwamba takwimu za utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambazo nimezionesha zilikuwa ni kwa kipindi ambacho kinaishia hadi Aprili, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninataka niseme kwamba kiwango kikubwa cha bajeti ambacho tumepokea baada ya Aprili, 2021 kwamba tumepokea fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha na kuendelea na shughuli zetu za mafunzo ya Jeshi, upande wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, ukarabati wa miundombinu na shughuli za mashirika ambayo tunayasimamia katika Wizara. Kwa hiyo, tumeendelea kupata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Mambo ya Nje imeshauri pia Serikali ione umuhimu wa kutoa fedha za maendeleo kwa Fungu 39 kwa mtiririko uliopangwa, aidha, itoe kwa ukamilifu fedha zote za maendeleo ambazo bado hazijatolewa katika Fungu 38 – Ngome na Fungu 57 – Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niseme tu kwamba katika mwaka wa fedha 2020/2021, Fungu 39 liliidhinishiwa shilingi bilioni nne kwa fedha za maendeleo, lakini mpaka ninapozungumza tumepokea shilingi bilioni 3.5 na ushehe hivi. Kwa hiyo utaona kwamba karibu asilimia 100 ya fedha zote tulizotengewa tunazipata. Ninao uhakika mpaka tutakapokwenda kumaliza mwaka tutakuwa tumepokea asilimia 100. Naishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Fungu 57 – Wizara kupitia Fungu 58 – Ngome tumepokea shilingi bilioni 83.8 kati ya shilingi hizo bilioni 150. Lakini pia tulipokea shilingi bilioni 9.694 kati ya shilingi bilioni kumi mtawalia. Ninataka nioneshe tu kwamba kuanzia kipindi kile cha Aprili mpaka sasa hivi mtiririko wa fedha kwa kweli tunashukuru sana, ni mzuri. Tunakwenda vizuri sana.

Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tu kwamba ninaamini kabisa kwa makubaliano na Wizara ya Fedha kwa mazungumzo tulifanya na tukakubaliana, mpaka kufikia Juni tutakuwa tumefanya mapokezi makubwa na saa nyingine itakuwa kwenye rekodi nzuri katika kipindi hiki kwamba ninaweza nikasema haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia ilitushauri kukamilisha mpango wa kuwapatia wahitimu wote wa kidato cha sita mafunzo ya JKT. Tunashukuru kwamba tumeendelea kupata fedha, ndiyo maana utaona kwa rekodi ya wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kwa sasa hivi kwa fedha tulizopata tutakwenda kupokea wanafunzi hawa 35,000 ukilinganisha na kipindi kilichopita tulipokea wanafunzi 21,000. Kwa hiyo, unaona kwamba mambo yanakwenda barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipokea pia pesa kama nilivyosema, kwa ajili ya JKT, hizo shilingi bilioni 3.5 kati ya bilioni nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ilishauri kwamba tukamilishe haraka mpango wa kuwezesha vijana kujitolea kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa kuwapatia mitaji kwa kushirikiana na sekta na taasisi nyingine. Huo mpango ndiyo upo kama nilivyowahi kueleza hapo awali pia, kwamba tunafungamanisha sasa mafunzo haya ili tuweze kuwapokea watoto kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara kama ya Kilimo, Mifugo, Viwanda na Fedha ili tuone kwamba tutakuja na mpango kwamba vijana wetu wote ambao wanamaliza na kupata ujuzi tunakwenda kuwawezesha ili sasa yale mafunzo yao yalete maana kwa maana ya kwamba waweze kupata kazi ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niaombe tu Waheshimiwa Wabunge wakiwemo Wabunge vijana ambao mmezungumza kwa uchungu sana kuhakikisha kwamba hawa vijana ambao tunawaanda ili tutakapowarudisha wakirudi kule wakiwa wamepata mafunzo wamesheheni mambo mbalimbali, sasa waweze kwenda kujitegemea lakini pia kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Kwa hiyo, mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala ambalo pia Kamati imetushauri kwamba katika miradi yetu Kamati imeona kwamba wakati mwingine tunapata fedha hizi za ufadhili zinakuwa na utaratibu wa kuwa labda imehitaji mshauri elekezi akatoka sehemu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri huu pia tumeuchukua kwamba tutaendelea kuona kwamba tunaisimamia vizuri ili pale tunapopata fedha au tumefadhiliwa, lakini mshauri mwelekezi awe sehemu yetu ili tuweze kufanya kulingana na mahitaji yetu. Kwa hiyo na hilo tumeweza kulichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mchango Waheshimiwa Wabunge wamezungumza juu ya kuliimarisha Shirika letu la Nyumbu pamoja na mashirika mengine. Nataka niseme tu kwamba tunayo mashirika, tuna Shirika letu hilo la Nyumbu (TATC), lakini pia tuna Shirika letu la Mzinga na SUMA JKT.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumza juu ya Shirika letu hili la Nyumbu, kwanza tumepata fedha ambapo sisi wenyewe kupitia Nyumbu tunakwenda kutengeneza nguzo zile za umeme na kazi imeanza. Naishukuru sana Serikali, tumepata fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya maboresho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kwenda kufanya ufufuaji, ip0 mitambo 116 ambayo kipindi cha nyuma ilifanya kazi vizuri, lakini pia kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia; upande wa Serikali tumejipanga vizuri, tumepata ule mpango wa maendeleo kwa ajili ya kuinyanyua Nyumbu. Na hii imekubalika Serikalini sasa tunakwenda kufanya maboresho makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, yako mambo mengi yatakwenda kufanyika kule Nyumbu na tunapenda pia Nyumbu iwe kitovu. Tutakwenda pia kuzingatia kuwachukua vijana ambao watakuwa na weledi wa tofauti, wabunifu. Tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunaifanya iwe center wale vijana wote ambao tunaona wanaweza kuwa na uwezo wa kitofauti tutawachukua. Lakini kazi yetu sisi ni kuwatengeneza na pia kuweza kuwatoa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuona kwamba ule ujuzi wao tunauendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejipanga vizuri, tunakwenda kuiboresha Nyumbu na tutakwenda kuweka fedha za kutosha kabisa na utaratibu unakwenda sawasawa. Kwa hiyo Nyumbu tutakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mzinga tunafanya uzalishaji – Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanachangia, Mheshimiwa Ahmed alichanganya kidogo Nyumbu na Mzinga; Mzinga ndiyo tunazalisha yale mazao muhimu. (Makofi)

Kwa hiyo, tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunakwenda kufanya sasa uzalishaji wa mazao ya kutosha kwa sababu sisi wenyewe mahitaji ya yale mazao ni makubwa sana, lakini bado ziko taasisi nyingi za kiulinzi hapa nchini zinahitaji kupata huduma ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali pia muda siyo mrefu tumepokea fedha nyingi sana na tumeshaagiza mitambo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kuzalisha kwa hali ya juu, kwa hiyo tumejipanga vizuri. Kule Mzinga tutakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengine ambayo tunakwenda kufanya maboresho kama nilivyozungumza, kule SUMA JKT. Kwa sababu taasisi zetu hizi zimejipanga sasa kwenda kufanya uzalishaji wa hali ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo niwatoe hofu tu kwamba tumejipanga kweli kweli na yako maeneo mengine tutakwenda kufanya maboresho ya sheria zetu ili kufanya taasisi zetu zifanye kazi, zitumie weledi, tuwatumie wataalam tuliokuwa nao vizuri bila kuwa na kikwazo chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo haya yote yanalenga kuhakikisha kwamba ile historia ambayo Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mkiirejea kwamba tunayo historia ya taasisi zetu hizi kipindi cha nyuma tuliweza kutengeneza magari, tuliweza kutengeneza mpaka nyambizi, tutakwenda kufanya hivyo. Lakini tutakwenda kujikita zaidi pia kwenye eneo hili la utafiti, na ndiyo maana upande wa Serikali tumejiandaa na tulikuwa na andiko ambalo niko nalo hapa ambalo linalenga kwenda kuboresha taasisi zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla niseme kwamba Wabunge walivyochangia nilikuwa najaribu kuangalia, angalau kuweka kwenye ma-group maeneo ambayo wamezungumza, kwa ujumla wake nikijaribu kupitia ninaona kwamba kulikuwa na masuala ya bajeti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, lakini niseme tu kwa hali ya bajeti hii ambayo naiombea sasa hivi hapa kumekuwa na ongezeko la bilioni 217 kama nilivyozungumza, hii ni asilimia kumi, siyo haba. Lakini bado Serikali imeonesha nia kwamba huko tunakokwenda tutakwenda kufanya maboresho makubwa sana ya ongezeko la bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sana kwa concerns zenu, lakini naishukuru pia Kamati kwa sababu Kamati imezungumza vizuri sana na kutoa maelekezo. Kwa sababu uko umuhimu wa kupata fedha za kutosha ili hizi zana ambazo tunazimiliki tuweze kuzitunza, tuweze kuzifanyia mazoezi, kwa sababu ili tuweze kuwa vizuri zaidi upande wa mazoezi ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa masuala ya kibajeti mmezungumza masuala ya pensheni. Tumeanza kughughulikia suala la pensheni, tumeanza na level ya Major Generals na Lieutenant General na majenerali kuhakikisha kwamba ile sheria ambayo ilipitishwa tunakwenda kuitekeleza. Kwa hiyo, tunaendelea kuifanyia kazi kuona maslahi ya askari wetu tunayaweka vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia yale masuala ya pensheni Waheshimiwa Wabunge mmezungumza hapa tunachukua ushauri wenu, lakini pia mmetoa pia masuala ya kibajeti juu ya ununuzi wa vifaa na hili tupo nalo vizuri, vifaa vya kwetu tulivyokuwanavyo tunavyo vya kisasa, tupo vizuri. Waheshimiwa Wabunge msiwe na wasiwasi, tupo vizuri. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge wamezungumza pia juu ya stahili za wanajeshi ni kweli zipo changamoto, lakini upo ukweli kwamba changamoto hizi tumezizungumza wenzetu wa Hazina, na ni ukweli kwamba tumewasilisha mahitaji yetu na mahitaji ya wanajeshi wetu ambayo wanadai na uhakiki unaendelea kukamilishwa kwa sababu tayari tumeshakuwa na mwelekeo na makubaliano kwamba tutakwenda kulipa haya madeni ya vijana wetu ambayo yamekaa muda mrefu. (Makofi)

Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge nimewasikia na imetia moyo kuona mnawajali sana vijana wetu, Jeshi hili ni la kwetu, vijana hawa ni wa kwetu, lazima tuwahudumie ili waweze kutufanyika kazi nzuri, waendelee kufanya kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuhusu stahili zao na maboresho ya maslahi niliambie tu Bunge lako na mimi mwenyewe nipo mstari wa mbele kuhakikisha kwamba ninakuwa na jeshi ambalo ni la kisasa lakini jeshi ambalo linahudumiwa na jeshi ambalo sasa linakuwa na morali na motisha ya kutosha kwenda kufanya kazi. (Makofi)

Kwa hiyo, hili halina wasiwasi tumefanya vikao kadhaa kwa nia ya kufanya maboresho. Waheshimiwa Wabunge, niwatoe hofu tunakwenda kufanya mapinduzi makubwa ili jeshi letu hili zuri lenye sifa nzuri tuendelee kuona kwamba tunawatendea haki vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuhusu maeneo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla mmechangia ni juu ya mafunzo ya JKT, Mheshimiwa Musukuma ulizungumza sifa, sifa zipo ndiyo maana tunaonesha sifa ya vijana wa kujitolea tumeionesha kuanzia darasa la saba tunakwenda, kwa sababu tunakata hata yule kijana ambaye hakubahatika kwenda shule, lakini akija kwetu tutamtengeneza, akirudi kule kijijini anakwenda kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sifa zipo zinamuonyesha kijana ambaye tutaweza kumchukua kwa ajili ya kujitolea na wale vijana kwa mujibu wa sheria. Kama mlivyozungumza kwamba sifa zipo tutaendelea kufanya hivyo, pale ambao patalazimika kuwa na kutengeneza sifa za ziada kulingana na mazingira ambayo tupo nayo tutafanya hivyo kwa nia hiyo hiyo yakuona kwamba tunaendelea kuwatengenezea vijana sifa nzuri, uzalendo, uchapakazi na kuweza kutoa mchango wao kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimuarifu tu Mheshimiwa Matiko hapa alizungumza kwamba kuna deni kule SUMA guard, labda hii rekodi ya miaka mingi lakini mpaka ninapozungumza sasa hivi kwa vijana ambao wameajiriwa huko SUMA guard hatuna deni. Kwa hiyo hii, kama labda saa nyingine sikukuelewa naomba tu baadaye tunaweza tukazungumza nikupate sawa sawa, eeh si ndiyo haina mashaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu pia ipo michango ilitolewa kuhusu ushirikiano wa JKT na JKU na ushauri uliotoka Mheshimiwa tumeupokea lakini niseme tu, nakuliarifu Bunge lako tangu mwaka 2001 yapo mashirikiano ambayo tunayafanya, tunabadilishana uzoefu, tunabadilishana mafunzo, tunabadilishana hata vijana kwa ajili ya kuona kwamba tunakwenda sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwatoe wasiwasi ndugu zangu na mimi hata nimetembelea kule Zanzibar na nina programu za kwenda Zanzibar pia, kwa hiyo nikitembelea kule nitaendelea pia kufanya mijadala kwa ni hiyo hiyo ya kuona kwamba tunafanya majeshi yetu yanafanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu ili kuona kwamba sisi wote tunakwenda sawa, kwa hiyo, Unguja nilikwenda na Pemba nitakwenda siyo mara moja, nitaendelea kwenda kwa nia hiyo hiyo ya kuona kwamba tunaweza kujiweka vizuri ili tuone kwamba tunatembea wote pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ongezeko la bajeti kama nilivyozungumza kwa ajili ya mafunzo kule JKT na pia kuna ushauri uliotolewa kwa ajili ya elimu ya muungano kupitia majeshi yetu tutaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nilikuwa naona record pia ya bajeti hata ya JKT kwa maana ya mafunzo kwa mujibu wa sheria imeongezeka kutoka shilingi bilioni 16 kwenda bilioni 21.6 hii siyo jambo dogo, nilijaribu kuonyesha tu kwamba tunajitahidi sana kuomba fedha ili tuendane sambamba na mahitaji ya kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mambo mengine ambayo yalizungumzwa kwa ujumla ilikuwa ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ushauri tumeuuchukua, hata mimi nimetembelea hizi nyumba katika maeneo kadhaa tunahitaji kupaka rangi, tunahitaji kufanya maboresho na hiyo ni jambo la kawaida. Huwezi kujenga nyumba ukakaa nayo muda wote bila kuwa uliifanyia ukarabati na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mapungufu kadhaa ambayo tumeyaona hata tulivyokuwa na Kamati, tumejipanga kwenda kushughulikia upungufu wa nyumba lakini upo mpango pia wa kuendelea kujenga nyumba kwa ajili ya wanajeshi wetu, mmeshuhudia nyumba nyingi zimejengwa kwa kipindi kifupi, lakini mpango ule siyo kwamba umeisha tunaendelea kwenda kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengine walizungumza juu ya mchango wa jeshi letu kwa ajili ya ulinzi wa amani. lakini pia Mheshimiwa Lucy Mayenga alizungumza juu ya kuongeza idadi ya akinamama katika operation zetu. Niwahahakishie tu asilimia 6.5 ya wanajeshi waliopo kwenye operation tunao akinamama, yapo mahitaji mengine ni maalum yanahitaji akinamama wanajeshi kuwasaidia wenzetu katika maeneo ya operation. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kunapokuwa na machafuko maeneo kadhaa waathirika wakubwa ni akina mama na watoto, tunahitaji pia kuwa na weledi kupitia jeshi letu kuweza kusaidia. Kwa hiyo tutaendelea kuongeza idadi kadri itakavyokuwa kwa sababu yapo makubaliano ambayo tunayafanya na wenzetu tunapokuwa tunapeleka askari kwenye operation. Kwa hiyo, tutaendelea kuona hivyo na tunafanya mijadala mingi ili kuona kwamba tunakidhi mahitaji ya wanajeshi wetu katika ulinzi wa amani katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, kama nilivyozungumza juu ya upimaji na uthamini wa ardhi kwamba mambo tumechukua lakini Wabunge wengi pia walizungumza juu ya huduma za afya, ndiyo maana tumejipanga na Waheshimiwa Wabunge msiwe na wasiwasi kwa wale ambao mngeweza kupata nafasi ya kutembelea kule Lugalo mnaweza kuona kwamba tumetengeneza eneo maalum kwa ajili ya kumudu magonjwa hatari ikiwemo Ebola na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kule utaona, tunavyo vifaa maalum. Mheshimiwa Kuchauka, yapo maeneo ukifika kule utashangaa maana yake mimi nilishangaa na mimi kidogo nina uzoefu kidogo, sasa wewe uliyetoka Liwale nafikiri ukienda kule nikukaribishe uone mambo mazuri ambayo yanafanyika kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejipanga kwa ajili ya kupokea hatari yoyote ikitokea kwa sababu wanajeshi wetu wanapokwenda kwenye operation pia kuna maeneo yana hatari sana, kwa hiyo tumejipanga hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi ya hapo kama nilivyozungumza kwenye hotuba yangu asilimia 80 ya huduma tunazotoa kwenye hospitali zetu ni kwa raia wetu kwa watanzania wenzetu. Kwa hiyo, unaona kwamba tunavyoimarisha hospitali zetu inalengo pia ya kwenda kuwahudumia wananchi wa watanzania na tunaendelea kufanya hivyo ndiyo maana tumeona kwa sababu Serikali sasa imehamia hapa Dodoma tumeanza ujenzi pale Msalato na ujenzi huu fedha tunazo, tutasimamia kuhakikisha hospitali hii inakamilika ili sasa tuweze kugawana kutoa huduma katika maeneo ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sidhani muda upo kwenye nafasi yangu, nimalizie tu, kukushukuru sana, nikushukuru sana kwa kuendesha mjadala, lakini Waheshimiwa Wabunge nimeona leo wametulia sana, kwa hiyo, ninawashukuru sana, walikuwa makini sana na nilifikiria kwamba saa nyingine tutakuwa na wachangiaji wachache, lakini tumepata michango mingi sana, na saa nyingine niseme tu siyo rahisi michango yote niweze kuizungumza moja kwa moja, lakini niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge tumewasikia na leo timu yangu ilikuwa kubwa kwa sababu ya kuhakikisha kwamba hatuachi neno hata la Mheshimiwa Mbunge mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ndiyo jeshi letu, jeshi letu limejipanga vizuri kama mnavyoliona hakuna mashaka, jambo lolote Waheshimiwa Wabunge mmelizungumza hapa tunaenda kulifanyia kazi kwetu sisi ndiyo mmetupa kazi ya kuweza kuhakikisha kwamba tunawatumikia watanzania kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kuwapongeza sana Katibu Mkuu yupo hapa na viongozi wote wa Jeshi wapo hapa, kazi nzuri inafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata nafasi kadhaa ya kuzungumza na wenzetu kutoka nje ya nchi na kwenye mashirika mbalimbali, jeshi letu linatamanisha sana liwepo maeneo mengi, mchango wake ni mkubwa na mchango wake ni mzuri sana, jeshi letu lipo katika ubora wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa NaibU Spika, kwa hiyo mimi naendelea kuwapongeza najisikia furaha sana kuwa Waziri katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba sasa kutoa hoja.

WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.