Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kipekee namshukuru Mungu kwa siku ya leo na zaidi sana niseme nafurahi na ninawashukuru wageni kutoka Kilimanjaro kwenye Jimbo la Mheshimiwa Profesa ambao wale kwa kweli ni mabosi wangu kazini. Na leo wataniona nikichangia live mubashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipongeze sana Profesa kwa hotuba ya kurasa 143 ambayo imesheheni kila jambo la kilimo. Na niseme kwamba, yote ni mazuri, lakini sasa sisi tunafanya nyongeza na maombi. Naona kabla sijasahau nianze na maombi, wametaja vitu vizuri, mbegu za maparachichi, wametaja mbegu za alizeti, wametaja mbegu za maharage, yote hayo yametajwa hapa ndani, lakini hayajatufikia hata kule Rombo hayajafika.
Mheshimiwa Spika, sasa niombe kupitia kwako tuweze kupatiwa mbegu hizo. Maparachichi yale nikayasambaze haraka sana na mbegu zote ambazo ni nzuri, lakini zaidi sana watupatie mbegu ya kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TACRI iko Kilimanjaro unaifahamu, lakini tunaambiwa kwenye hotuba waliosambaziwa mbegu za bure ni wakulima 220 tu; ni wachache ni tone tu la maji kwenye bahari. Naomba sasa ikiwapendeza watusambazie mbegu hizo, wamekua wakiitisha sana semina hapa za wakulima, lakini wakulima wa Kaskazini wa kahawa hatujafikiwa. Kwa hiyo, tunaomba elimu hiyo, ili tuweze kwendanayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwamba, sisi Tanzania tumekuwa na baraka miaka mitano iliyopita hatukuwa na njaa na mpaka tumegawa chakula na tulizalisha zaidi asilimia 126, hiyo ni neema pekee. Kwa hiyo, tulipata shida ya mafuta na kama tulipata shida ya mafuta mwanamke hawezi kutofautishwa na mafuta ya kupika, pale ambapo huna chochote cha kupika unatupa kitunguu kwenye mafuta unafunga mlango, watoto wanasikia kikiungua wanadhani unapika pilau kumbe hamna kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ninawaomba hii mbegu ya alizeti waliyoizungumzia isambazwe kote kwenye kaya zote Tanzania, kila mwanamke akizalisha debe moja la alizeti tumejikomboa, hatutangoja mafuta kutoka bandarini yanayoshushwa ambayo ni ya kiwango cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ametueleza katika vipaumbele vyake, ameeleza Mheshimiwa Waziri kwamba, anatamani kuona alizeti inazalishwa kwa wingi na hapa Dodoma kutakuwepo na mashamba ya mfano. Na nawaombea Wabunge wote wapate eka mbili-mbili hapa Dodoma, hapa kwako, ipitishwe kwenye halmashauri yako tukalime hiyo alizeti yawe mfano. kila Mbunge awe na shamba, asiwe tu Mbunge wa kuongea kwenye karatasi, haitusaidii sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa vile wewe ni diwani wa huku nakuomba sana utufikirie Wabunge wenzio tuweze kwenda kulima. Kwa sababu, amesema mbegu hiyo nzuri ya RECORD ya alizeti mpaka sasa imesambazwa kwenye mikoa mitano tu ikiwepo Mbeya na hiyo iko kwenye ule ukurasa wa 31, Kigoma, Dodoma mpo, Morogoro na Singida, huko kwingine je?
Mheshimiwa Spika, natamani kuona kila kaya. Na haya mafuta yaitwe, ikimpendeza sana Mheshimiwa Waziri, amuombe mama Rais Samia Suluhu Hassan, Jemadari wa nchi hii, aweze kuitwa mafuta yake yaitwe Samia. Tumechoka kula mafuta ya Korie na ya nini hayana viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninalotaka kumuomba tu Waziri wetu wa Kilimo, Profesa Mkenda, ni kuhusu kilimo hai (Organic Agriculture). Organic agriculture au mazao yanayozalishwa kwa kilimo hai yamekuwa na bei kubwa sana nchi za nje. Kahawa inayozalishwa katika viwango hivyo inafika hata kilo moja shilingi 10,000 ambapo bei ya kawaida Arabika Coffee ambayo ni nzuri kabisa ni shilingi 4,000. Na ninazungumzia Arabika Coffee kwa sababu, Kahawa ya Arabika Kilimanjaro sisi tunalima Arabika na tunalima katika tambarare ya Mlima Kilimanjaro ambayo ardhi yake imepata volcano kidogo. Ndio kahawa ambayo ina-blend kahawa zote duniani ili kuipa aroma nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sasa kahawa hii watu baada ya kuona ni shida sana kulima wameamua kung’oa ile kahawa na sasahivi watu wanalima ndizi badala ya kahawa. Nimuombe sana Profesa atusaidie na ana Katibu mzuri tu, Katibu Mkuu mzuri ambaye anayajua hayo maeneo, tuweze kurudisha tena hili zao la kahawa katika njia yake nzuri kwa sababu, wengi wa miaka hiyo wamesomeshwa na zao la kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini bahati ya kahawa ya arabika unaweza kuotesha mazao mengine, ni inter- cropping. Kwa hiyo, haizuwii ndizi kuoteshwa, haizuwii maharage kuoteshwa, haizuwii mahindi kuoteshwa. Kwa hiyo, kwenye kahawa hizo unaweza ukalima mazao mengi na ikawa ni faida kwa familia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nazungumzia hivyo kwa sababu, natoka eneo ambalo watu mashamba yao ni kidogo na yanaitwa vihamba. Kihamba kikubwa kabisa tena cha tajiri ni eka saba, sasa wengine wote ni eka tatu, mbili na moja na nusu na wote wanategemea hayohayo. Nimewaona wadau wa kilimo hapa, nimemsikia Jaqueline yupo, tunaomba basi afike na watusaidie tulime kahawa hizo pamoja na haya mazao ya horticulture. Zao mojawapo ambalo naliomba sana ni zao la parachichi, lakini pia tunaomba hata hii migomba yetu iweze kuboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utakubaliana na mimi kwamba, zao la mgomba linavunwa mwaka wote mzima, yani vijana wanakwambia 24/7 annually. Kila siku ndizi inakatwa na ndizi itaota, lakini unakuta sasa wasipopelekwa vizuri katika kulea migomba hii inatoa mikungu midogo sana ambayo haina tija. Nilikuwa naomba sasa ili kilimo hiki kiweze kuwa cha tija, tuweze kupatiwa mbegu ambazo zinatoa mikungu mikubwa, lakini pia tuweze kupatiwa maafisa ugani ambao watakuwa kama wale wa zamani; maafisa ugani wa zamani walikuwa wanajua kaya fulani ina migomba mingapi, kaya fulani ina kahawa ngapi, kaya fulani inazalisha kiasi gani na kwa pamoja sasa ndio inaweza kuleta summation, yaani junla ya mavuno yote ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kuna mazao ambayo yapo tu siku zote, ni kama mazao ya mtama yanalimwa kidogo sana kwenye tambarare, lakini muhogo umekuja na sisi wachaga tunaogopa mihogo kwa sababu, mihogo tunaogopa ina sumu, lakini nasikia kuna mihogo mizuri imekuja ambayo ni salama.
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ah sante. (Makofi)