Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mikumi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia machache katika hoja hii iliyo mezani inayohusu Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kuwa tumekuwa tukipanga mikakati mingi na kujinasibu kwamba tunataka kuipeleka nchi yetu kwenda kwenye uchumi wa kati ili tuweze kuipata Tanzania ya viwanda, wakati tunasahau kuwa hatuwezi kuwa na nchi ya viwanda nchi nzima kama bado tuna tatizo sugu na kubwa la nishati ya umeme katika sehemu zetu nyingi za vijijini ambako ndiko tunataka na tunapaswa kupeleka viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tutakuwa tunafanya kazi bure kama hatutaweka mkakati wa dhati huku tukisukumwa na dhamira ya mioyo yetu ya kufufua sekta ya kilimo. Yatupasa kuwekeza zaidi kwenye kilimo mfano, pamba, kahawa, korosho, miwa na kadhalika ili tuweze kutimiza dhamira yetu ya kuipata Tanzania ya viwanda ambayo pia itatusaidia kutoa ajira kwa watu wetu na kuongeza kipato kwa wakulima wetu na kujiletea maendelea ya nchi yetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumekuwa kila siku tukisema tunataka kufufua viwanda ambavyo vimekufa lakini hatutaki kusema ni nini kimeua viwanda vyetu. Mfano Mkoa wetu wa Morogoro ulikuwa ni moja ya mikoa iliyoshamiri kwa viwanda kadha wa kadha ambavyo sasa vimebinafsishwa, vingine vimeshakufa kabisa na kuwa mabanda ya kufugia mbuzi na kuku na vingine vipo njiani kufa maana kama ni mgonjwa basi yupo ICU anapumulia mipira kupata hewa na ndugu wapo mbioni kuzima mashine yenyewe ya kupumulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana kwa niaba ya wananchi wa Mkoa mzima wa Morogoro, Mheshimiwa Waziri kabla ya kusema ni vipi atafufua hivi viwanda, pia atuambie hali halisi ya viwanda vyetu vya Mkoa wa Morogoro ambavyo vilikuwa vinatoa fursa ya ajira kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Morogoro. Mfano, nataka kujua viwanda vyetu vya Mang’ula Mechanical and Machine Tools Limited (MMMT), Morogoro Canvas Mill Limited, Tobacco Processing Factory na MOPROCO vipo kwenye hali gani na vinasaidia nini kwenye ubinafsishaji uliofanyika na kama vina tija kwa Taifa letu. Pia kwenye Jimbo langu la Mikumi kuna kiwanda cha Kilombero Sugar Company Ltd. ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa sukari lakini kilibinafsishwa Aprili mwaka 1998 kwa Kampuni ya ILLOVO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali kuwasisitiza wakulima wa Wilaya ya Kilosa walime miwa na kuacha kulima mpunga na mahindi lakini wakulima hao wa miwa wamekuwa wakilalamika sana kunyonywa kuhusu idadi ya asilimia ya miwa inayoingizwa kwenye kiwanda hicho cha ILLOVO. Lakini pia wakiwa na malalamiko mengi ya upimaji wa utamu wa miwa hiyo (sucrose) na pia mabaki ya miwa hiyo (buggers) ambayo ni mabaki ya miwa yamekuwa yakitengeneza umeme na pia kuna morales ambayo inatengenezea pombe kali (spirits) lakini wakulima wamekuwa hawalipwi zaidi ya tani za utamu wa sukari tu ambapo sasa ndani ya kiwanda cha ILLOVO pia kuna kiwanda kingine cha kuzalisha pombe na bado wanasema kiwanda kinapata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kupata sukari ya kutosha kama hatutaweka mazingira mazuri na salama kwa wakulima wa miwa. Wakulima wa miwa wa nje wanataabika sana na wanayonywa sana na wanahitaji sana msaada wa Serikali kuwasaidia wakulima wao wapate mzani wao wa uhakika ili waweze kupima na kuingiza miwa yao kwa haki badala ya sasa kuwekewa mzani wasiouamini. Wapimaji ndio hao hao wenye kiwanda ambao pia ndio wanaopanga bei ya zao hilo, nasisitiza na naomba sana Serikali ifanye mpango wa kuwaletea wakulima mzani ili wapate haki yao na kufutwa machozi yao ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko makubwa sana ya wafanyakazi wa Kiwanda cha ILLOVO ambapo kumekuwa na mateso na unyanyasaji mkubwa sana wa wafanyakazi wa ngazi ya chini wa kiwanda hicho. Nakushauri siku moja uende pamoja na mimi kwenye Kiwanda cha ILLOVO ili tukasikilize kilio cha wafanyakazi wao na ninakuomba usiende kuonana na uongozi wa kiwanda bali tuonane na viongozi wa vyama vya wafanyakazi au wafanyakazi wenyewe ambao wamekuwa kama watumwa ndani ya ardhi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, lakini pia kumekuwa na malalamiko makubwa ya ajira za kindugu, ajira za kirafiki na ajira za rushwa ya ngono. Vyeo vinapandishwa kwa upendeleo mkubwa, lakini mbaya zaidi ni mishahara midogo sana ambapo Kampuni ya Sukari Kilombero (ILLOVO) imekuwa ikiwadanganya wafanyakazi kwamba wanapata hasara pindi linapokuja suala la majadiliano ya mishahara ingawa ukweli ni kwamba hakuna mwaka waliopata hasara bali ndiyo kwanza wanaendelea kuongeza kiwanda kingine cha tatu cha pombe, pamoja na ununuzi wa vifaa vyote vya usafiri kama magari, pikipiki ambavyo kila mtu akitumia kwa miaka mitatu tu viongozi hao wanauziwa kwa shilingi 100,000 tu.
Hii ni kama ile kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa John Magufuli, ni kwamba viongozi wa Kampuni ya ILLOVO wanaishi kama malaika na wafanyakazi wa chini ambao kimsingi wamekuwa wakifanya kazi ngumu kwa jasho na damu wanaishi kama mashetani. Sasa kuna wafanyakazi wa kigeni 23 pale ILLOVO, wakati wafanyakazi wa kigeni hawakutakiwa kuzidi wafanyakazi watano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo kubwa sana la wafanayakazi zaidi ya 2000 waliokuwa wanafanya kazi kwenye kiwanda cha Kilombero Sugar Company, kwa masikitiko makubwa sana nataka nipate majibu ni lini watatendewa haki zao na kulipwa mafao yao kama wanavyostahili kwa kupitia mkataba wao na mwajiri Na. 4/1995 ambapo walilipwa miezi kumi badala ya miezi 40 kadri ya Kifungu Na. 10.3.7 kinachohusu upunguzwaji kwenye mkataba huo wa hali bora za wafanyakazi, hivyo basi walipunjwa kiasi cha miezi 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri aje na majibu ya hoja hii ya msingi sana ambapo pia wafanyakazi hao walifutiwa malipo ya utumishi ya muda mrefu kama wanavyostahili kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na malalamiko mengi sana juu ya vipimo vya kazi kwa wafanyakazi wanaofanya kazi za vipimo. Sera waliyonayo ni kuhakikisha wanawapa vipimo vikubwa ili wasiweze kumudu kumaliza, hivyo kwao inawasaidia kubana matumizi kwani mfanyakazi asipomaliza kipimo kile alichopewa hawezi kulipwa hata kama kazi imebaki robo. Huu ni utumwa wa kiwango cha juu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inabidi ilifuatilie kwa kina na kuchunguza makampuni haya ya sukari yenye mashamba kwani wananchi hawa wanateseka sana. Serikali inaweza kufurahia kwamba wananchi wanapata ajira kumbe wamo utumwani ndani ya ardhi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ningeiomba Serikali ituambie ni lini itaanza kujenga viwanda vya kusindika viazi ambapo kilimo hicho cha viazi kimeshamiri sana katika Kata ya Kisanga ambapo tumebarikiwa kulima viazi kwa msimu mzima kwa wingi kushinda hata Gairo. Na pia napenda kuishauri Bodi ya Sukari itimize wajibu wake wa kuhakikisha inasimamia haki stahiki za wakulima wa miwa kuanzia kwenye mikataba yao dhidi ya makampuni ya sukari na wamiliki wa viwanda maana kwa sasa unyonyaji umezidi kwa wakulima wa miwa na kilio chao kikubwa ni kuwa na mzani wa kupimia sukari unaomilikiwa na wakulima wenyewe, tofauti na sasa ambapo mwenye kiwanda ndiye anayemiliki mizani hiyo na kuleta malalamiko ya miwa mingi kutupwa kwa kukosa ubora na utamu wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Waziri aje na majibu, ni tani ngapi za wakulima maskini zimeshatupwa mpaka sasa na ni hasara gani ambayo wakulima wameipata mpaka sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.