Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo. Nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo mlipambana vya kutosha wakati tumepata baa la nzige. Kwa kweli hongereni mlifanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna ambaye hatambui umuhimu wa kilimo hapa nchini na sote tunatambua jinsi gani ambavyo kilimo kinachangia kwenye uchumi wetu au kwenye pato la Taifa kwa maana asilimia 26 ya pato letu la Taifa linatokana na sekta ya kilimo, kinatoa ajira kwa asilimia 58 lakini mauzo ya bidhaa za nje kwa asilimia 30 na pia sekta ya kilimo inachangia asilimia 65 ya malighafi viwandani.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano uliweka kipimo kwamba kilimo kiweze kukua kwa asilimia 7.6 lakini hadi leo kilimo hiki kimekuwa kwa asilimia 4.9 Sasa tunaweza kujiuliza kwamba kama tunajiwekea mipango au vipimo fulani vya kutupima kama nchi na hatuvifikii maana yake kuna visababishi vingi ambavyo vinasababisha hicho ambacho tunakiweka tusikifikie.

Mheshimiwa Spika, mojawapo kwanza kilimo hakipati uwekezaji wa kutosha. Kama nchi sina hakika kama tumeona kilimo pamoja na haya nilioyataja huko juu namna gani kinachangia uchumi wa nchi lakini sina hakika kama Serikali mmeona umuhimu wa kuwekeza vya kutosha kwenye kilimo ambacho kinawasaidia Watanzania wengi sana karibia asilimia 80. Hivyo basi ni muhimu sana mkaona umuhimu wa kuwekeza vya kutosha kwenye kilimo. Kama ambavyo tunafanya jitihada kubwa ya kuwekeza kwenye miundombinu kwa maana ya labda Wizara ya Ujenzi, barabara, Siegler’s, SGR na kila kitu, vivyohivyo tufikirie namna gani ya kuwekeza vya kutosha kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiwekeza vya kutosha kwenye sekta ya kilimo maana yake hata hawa vijana wetu walio nje wengi huko hawana ajira wanamaliza vyuo, tukifanya mazingira mazuri na watu wakapenda kilimo na watu wakaona kilimo si tu cha kupanda mahindi kwa maana ya mahitaji ya chakula lakini wakafikiri kwamba nitapanda mahindi lakini pia itakuwa ni sehemu ya biashara na kuniingizia kipato. Maana tunahitaji pia kubadilisha mitizamo ya watu kwa kuwawezesha kwamba ninalima kilimo kama biashara na akiba nitakayopata nyingine itakuwa kama chakula. Kwa hiyo, tunahitaji sana kuwa na mbinu hizo za kubadilisha mfumo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia mchawi mwingine mkubwa wa kilimo chetu ni fedha tunazoidhinisha hapa Bungeni za miradi ya maendeleo, haziendi kama inavyotakiwa. Tukitafuta uchawi ni nini? Nadhani uchawi mkubwa uko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano, mwaka 2017/2018, tuliidhinisha shilingi bilioni 150 kwenye fedha za maendeleo tu, zilizokwenda ni shilingi bilioni 27. Mwaka 2018/2019, tuliidhinisha shilingi bilioni 98, zilizoenda ni shilingi bilioni 46; mwaka 2019/2020 tuliidhinisha shilingi bilioni 143, zilizoenda ni shilingi bilioni 46. Mwaka huu ambao bado hatujaumaliza, lakini mpaka Aprili, tuliidhinisha shilingi bilioni 150 lakini mpaka Aprili zilizotoka ni shilingi bilioni 68. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tusitegemee muujiza wa kuikomboa sekta ya kilimo kama hata hiki kidogo tunachokitenga hakiendi. Ukiangalia hapa, maana yake hata asilimia 50 ya fedha tulizotenga kwenye miradi ya maendeleo kwa maana ya kilimo, hazijawahi kutoka kwa miaka hii niliyoitaja. Ndiyo maana nasema upo umuhimu wa Serikali kuona kwamba tunawekeza vya kutosha kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hebu tuiombe na kuishauri Serikali kwamba safari hii hiki ambacho tutakipitisha hapa kiende kwa asilimia angalau 80. Halafu tujipime kwamba hicho tutakachokipeleka: Je, kweli kitakwenda kufanya yale tunayoyakusudia na kuleta mapinduzi ya kilimo?

Mheshimiwa Spika, huko nyuma tulikuwa na slogans nyingi za kilimo, wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne pia kilimo kiliingia kwenye Big Results Now, Kilimo Kwanza, mambo mengi sana. Ni vyema hizo slogans tunazoziweka na hiyo mikakati tunayoiweka tuitekeleze kwa Serikali kutoa fedha zinazotakiwa, zilizoidhinishwa hapa Bungeni zitoke zote kama ambavyo inatakiwa. Hilo ni muhimu sana. Hapa tutakuwa tumeondokana na uchawi wa sekta ya kilimo kwa ujumla, angalau tutakuwa tumepunguza. Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikatazama hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, kwa mujibu wa report ya CAG, ameonesha mambo mengi sana ambayo ni changamoto au ni madhaifu kwenye sekta ya kilimo. Ameonesha mfano mmojawapo, kwamba wakulima hawana ujuzi wa matumizi ya mbegu, mbolea na viuatilifu. Sasa haya ni mambo ambayo Wizara mnaweza kuyafanya yakatekelezeka, mkulima huyu akapata ujuzi, akajua matumizi ya mbegu bora, akajua matumizi ya mbolea sahihi kulingana na ardhi yake, anatakiwa atumie mbolea gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii itakwenda sambamba na kuangalia yale maabara ya kupima udongo, kwamba hapa udongo huu nikilima naweza kutumia mbolea ya aina gani? Ifike mpaka wilayani, tusiweke tu hivi vituo kwenye centre za mikoa, ni ngumu kwa mwananchi kufika, lakini tukiweka mpaka centre za halmashauri zetu kwa Maafisa Ugani kule chini, maana yake tutakuwa tumemsaidia mwananchi kwa kumpa ujuzi kujua kwamba udongo wangu hapa ninapaswa kutumia mbolea ya aina gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linguine, CAG ameonyesha kwamba, “kuna usambazaji wa pembejeo usiokuwa na ubora. Hii ni kutokana na kwamba Serikali mmeshindwa kudhibiti.” Haya siyo maneno yangu, ni maneno ya report ya CAG ameeleza. Sasa ni mambo ambayo yako chini ya uwezo wenu Wizara kuhakikisha mnadhibiti. Bila shaka hili hata kama linahitaji fedha, siyo nyingi sana. Ila tunaweza kuona namna gani tunadhibiti haya ili kuhakikisha kile tunachokusudia katika usambazaji wa pembejeo, basi ufanyike kwa kadri ambavyo inatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linguine, CAG amesema kwamba kwa mwaka 2016/2017 mpaka 2019/2020, ni asilimia 39 tu ya ugavi wa pembejeo ulifanyika kwenye mbegu, mbolea na viuatilifu. Sasa tuone kwamba kama tunaweza kununua kwa asilimia 39 tu; na inawezekana hii ni kwa sababu ya ufinyu wa bajeti, tusitegemee muujiza. Kama hatufiki hata asilimia 50 ya ununuzi wa hivi vitu ili viweze kumfikia mkulima, tusitegemee mkulima aweze kusaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri sana Serikali na Wizara, CAG ameeleza mambo mengi sana, mkifanyia kazi haya ambayo ameeleza kama ni changamoto, bila shaka tunaweza kuvuka hatua moja mbele kuhusiana na sekta ya kilimo kumkomboa mwananchi na mkulima wa Tanzania kuhakikisha kwamba kilimo chetu kinakuwa na faida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kwamba tunahitaji pia kufanya Watanzania wakipende kilimo. Vijana wetu wakimaliza shule wasifikirie tu kazi ni kwenda ofisini, waone pia kilimo ni kazi ambayo inaweza kumpatia kipato na kuendesha maisha yake kwa Serikali kujenga mazingira mazuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)