Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema, naomba kushauri kama ifuatavyo katika hii bajeti ya Wizara ya Kilimo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, nashukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwa na wataalam wengi sana katika Wizara yao. Katika nchi hii ukiondoa Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, Wizara ambayo ina watu ambao ni maprofesa na madaktari ni Wizara hii ya Kilimo, lakini mpaka sasa hivi, pamoja na kuwa na elimu kubwa kiasi hicho, hawajaweza kutatua kilio cha wananchi katika nchi hii. Nchi hii asilimia 75 wanategemea kilimo; na hiki kilimo kimeshindwa kumsaidia mwananchi toka nchi hii ipate uhuru. Sasa linakuwa ni tatizo kubwa sana. Hatujui tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Spika, ili nchi hii iweze kupata maendeleo katika sekta ya kilimo, tunahitaji mjadala wa Kitaifa. Ufanyike mjadala wa Kitaifa tupate solution kwamba tufanyeje? Yaani tuwe tumeondoa matatizo. Bila kwenda na mjadala wa Kitaifa katika Wizara hii, watabadilishwa sana Mawaziri. Kwa sababu katika Wizara ya Kilimo kuna watu wana roho mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kukwambia, sijui tutafanyaje katika hii Wizara. Bahati nzuri wewe ni mtoto wa mkulima, unajua, umekaa huko Ushirombo, umeona ile hali iliyoko kule. Umekuja tena huku kwenu Ugogoni umeona hali iliyopo; lini wakulima wa nchi hii nao watakuwa matajiri? Sasa ujue kuna roho mbaya iko pale.

Mhehimiwa Spika, tunasomesha mtoto, anatoka huko kwetu kijijini na ameona hali ya wazazi wake ilivyo; anakwenda SUA. Akitoka SUA pale anaishi mjini, harudi tena kuja kumsaidia mzazi wake lima hivi, kama alivyosoma, haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa kwanza kabisa, naomba hii Bodi ya Kilimo ivunjwe. Bodi ya Pamba hii kwa sisi wakulima wa Mkoa wa Mwanza ivunjwe. Iundwe Bodi ya Pamba ya watu ambao wanajua kilimo cha pamba ni nini?

Mheshimiwa Spika, mimi nataka kuzungumzia pamba tu. Tuna Chuo chetu pale cha Ukiriguru, kimekuwa hakina tija. Pale Ukiriguru kuna TARI wako pale. Kwa mfano, Mheshimiwa Bashe, hivi ninavyozungumza na wewe, bahati nzuri nawe ni mtoto wa mkulima, lakini utachoka, yaani utazeeka kabla ya muda wako, kwa sababu umezungukwa na watu wenye roho mbaya. Mimi ndicho ninachotaka kukwambia, utatembea sana, lakini mpaka utatoka kwenye hiyo Wizara bila kuwasaidia wakulima wa pamba. Umezaliwa Nzega wewe, unajua kabisa pamba inavyotusaidia sisi. Haya maneno gani haya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulikuwa tuna tani 350,000, leo tunakuja kurudi kwenye tani 120, haya maneno gani? Tutafikaje kwenye Ilani ya Uchaguzi tunasema tuwe na tani milioni moja? Tunahitaji mjadala wa Kitaifa katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo mchezo, hili ni jambo ambalo ukisimamia nafasi yako hapa vizuri kabisa ndani ya hili Bunge, kutusaidia wakulima wa pamba, tukienda kwenye mjadala wa Kitaifa tutakuletea jibu sahihi tufanyeje ili tuweze kupata mapinduzi makubwa ya kilimo cha pamba? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Waziri, Profesa pale, hebu wakulima wa kilimo cha pamba, wasajiliwe nchi nzima. Wakulima wako katika mikoa 17, wako katika wilaya 54; wapeni vitambulisho tujue kwamba katika kilimo cha pamba tuna ekari ngapi zinalimwa mwaka huu? Hawa wakulima wa pamba wanahitaji kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe umekwenda kuona, bahati nzuri Mheshimiwa Bashe nilikuwa ofisini kwako juzi, nimekwambia kale kadawa kanaitwa heka pack peke yake kanauzwa shilingi 9,000/=, leo umekwenda kusema waagize kwa jumla, kamekuja kuuzwa shilingi 4,500/=. Hiyo shilingi 4,500/= bado ni kubwa. Tunakuomba uendelee kuwa mzalendo hivyo hivyo japo watakuchukia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo wanakuja kuagiza mbolea kwenye high season, kitu ambacho ni cha ovyo kabisa. Sijui nisemeje? Wakati wa low season hamuagizi mbolea, mnakuja kuagiza mbolea mwezi Septemba, mwezi Agosti, kwenye high season wakati kila nchi inataka mbolea. Leo Serikali ya India inaagiza tani 1,100,000, wewe una tani zako 50,000, unasubirije mpaka mwezi Septemba huko? Kwa nini usinunune mwezi Februari?

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge humu ndani, jamani mnielewe. Ni habari gani hii? Ninyi badala ya kuagiza kwenye low season mkatoa tender hiyo mkaagiza kwa bulk mbolea ikaja hapa ya bei rahisi, mnakuja kuagiza mbolea ambayo inafika hapa kwa bei kubwa! Sasa ukiwasajili wakulima, hapo hapo una haki ya kwenda kuzungumza na watu wa Wizara ya Ardhi mwapimie vipande vyao hivyo vya ardhi, tupime mashamba yote tujue tatizo ni nini ili wananchi sasa waweze kuja kupata tija na hiki kilimo chao.

Mheshimiwa Spika, leo Misri ekari moja inatoa tani moja na nusu mpaka tani mbili. Wenzetu wa Chad wanatoa tani mbili na nusu. Leo hapa tuliko pamba inalimwa hapa chini Msumbiji, wanatoa tani moja na nusu. Sisi iweje ekari moja inatoa kilo 150, kilo 300? Nani atapenda kuilima pamba? Ardhi imechoka, inalimwa toka mwaka 1960 mpaka leo bila mbolea, unawezaje ukazalisha hizi tani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa Maafisa Ugani wetu tulionao na wenyewe ni tatizo, wapelekeni pia kwenye semina. Sisi wakulima wa pamba tunaijua pamba. Bila hata kumleta Afisa Kilimo, mimi nailima pamba tu; nimekuta nyumbani inalimwa, mimi mwenyewe nimeilima, tena tunailima kwa jumla. Hili najua ni tatizo.

Mheshimiwa Spika, tatizo lingine liko kwenye ushirika. Wamekuja kuunda hizi wanaziita AMCOS, majambazi wakubwa kabisa. Yaani hatujawahi kuona ujambazi kama huu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashe amepita mwenyewe ameziona hizi AMCOS; mnakuja kuleta matatizo kwa wananchi tu wanakuja kudhulumiwa pesa zao. Badala ya kuimarisha ushirika, mnaleta maneno ya AMCOS, wajanja fulani watatu, wanne wanakaa kwenye kijiji wanajiita AMCOS. Hebu mzipitie hizi AMCOS zote katika nchi hii mje mwone. Hawa watu wanatakiwa kupelekwa Mahakamani. Hata sasa hivi tunashangaa bado wako huru. Hii ni hatari sana katika nchi hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, ninachotaka kuwaambia ninyi watu wa Wizara,…

SPIKA: Mheshimiwa Tabasam…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, yaani nina kamchango kadogo, kaendelee…

SPIKA: Mheshimiwa Tabasam, muda hauko upande wako.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, ninachoomba tu ni kwamba…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Ameshamaliza. Malizia Mheshimiwa Tabasam.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, lakini muda wangu umekuwa ni mdogo sana. (Kicheko/Makofi)