Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimwombe sana Mwenyezi Mungu niweze kuzungumza katika hali ya kawaida nisi-panic kwa sababu Wizara hii ilitaka kusababisha mimi nipoteze uhai kwa sababu ya suala la stakabadhi ghalani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naongea hapa kwa niaba ya wananchi wa Songwe, Wilaya ya Songwe ambayo takribani miezi miwili sasa tulipata kidogo mgogoro juu ya suala la stakabadhi ghalani. Cha kwanza, nataka nielezee Wizara ya Kilimo sijui kama wanafanya utafiti. Suala la stakabadhi ghalani Wizara ya Kilimo au Serikali kwa ujumla wanasema ni suala la mpango wa kumkomboa mkulima, si sawa kila suala hili ni zao la kumchanganya mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkulima hana amani kabisa na suala la stakabadhi ghalani. Ni kweli jambo hili lipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na naomba ikiwezekana kama tunaweza hata tukalirekebisha tulitoe kabisa kwa sababu kule vijijini haliji katika mfumo wa kubembelezana, ni jambo la lazima kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haiwezekani! Mkulima huyu wakati anaandaa shamba Serikali haipo wala haimwoni, mkulima huyu anapopalilia Serikali haipo wala haimwoni, anakopa fedha kwa wachuuzi wa zao la ufuta au alizeti Serikali haipo, halafu baadaye mwezi Machi au Aprili, ufuta umeshang’aa sasa umekomaa, Serikali ndiyo inakuja inasema, sasa ufuta wote huu tunaomba msiuze kwa huko mlikokuwa mmekopa hela ila mpeleke stakabadhi ghalani. Haiwezekani katika hali ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilihama Bungeni hapa sikuwepo takribani mwezi mzima, nilikuwa Jimboni nashughulikia wakulima wangu hapa. Ni kero kubwa, nimshukuru sana Mheshimiwa Bashe nilimpigia simu, Mheshimiwa Waziri nilimpigia simu alipokea baadaye akasema atanipigia na hakunipokea, nina jambo naye, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Bashe kwa sababu alipokea simu na kesho yake aliwatumia Mrajisi na Mr. Bangu, Mkurugenzi wa Stakabadhi Ghalani, akaja mpaka Songwe Jimboni. Nimewaona wale pale wamekaa, waseme wenyewe waliona nini kule jimboni. Haiwezekani mambo kama haya Serikali tunaangalia tu! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Wabunge wenzangu kesho waniunge mkono, kesho nitavaa suti nyeusi hapa kwenye kushika shilingi, kwamba stakabadhi ghalani tunaizika kesho, haiwezekani! Kesho ni msiba wa stakabadhi ghalani nchini Tanzania. Haiwezekani kabisa, nakataa. Jambo hili ukiwaona wale wakulima wanahangaika nalo.
Mheshimiwa Spika, kule Songwe kuna maghala matatu…
MHE. KIZITO J. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. KIZITO J. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mulugo kwamba stakabadhi ghalani inatamkwa kwa jina Tanzania, lakini practice ya stakabadhi ghalani Tanzania ni collection center ya mazao, inalenga kukusanya mapato ya Serikali, na siyo kuwasaidia wakulima wadogo. (Makofi)
SPIKA: Sisi Mkoa wa Dodoma, maeneo yaliyokuwa yanalima ufuta mwaka huu wameacha kabisa kulima ufuta. Wameacha kwa sababu ya kutotaka kugombana na Serikali kuhusu stakabadhi ghalani, maana ukishapata huo ufuta unaweza ukafungwa bure na zao la kwako mwenyewe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mulugo, endelea.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa kwa mikono miwili na miguu miwili. Kama nilivyosema, mkulima huyu tunasema eti tunamtetea mkulima huyu. Wilaya ya Songwe ni kubwa kuliko hata Mkoa wa Songwe wenyewe ukilinganisha Wilaya ya Mbozi, Momba na Ileje, lakini tulikuwa tumewekewa center tatu za ukusanyaji wa ufuta, Mkwajuni, Chang’ombe na Kanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutoka Mkwajuni mpaka uende nilikozaliwa mimi Kijiji cha mwisho kabisa karibu na Ziwa Rukwa kule ni kilometa 168. Mkulima huyu anyanyue debe mbili za ufuta alete Mkwajuni aje auze, nilikataa na nilimwambia Mkuu wa Wilaya utaniweka ndani bure. Haiwezekani katika mazingira ya kawaida, lakini Serikali inaendelea kulazimisha, Mrajisi yuko pale nimemuona aseme mwenyewe aliona nini Songwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mkuu wa Wilaya ya Songwe Ilikuwa ukiwa na ufuta akikukamata anakuweka ndani, mpaka ninavyosema hivi, pikipiki ziko ndani, alikuwa ameshikilia magari yote ya wakulima, haiwezekani tu katika mazingira ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo, wale watumishi wa Serikali wa Wilaya ya Songwe hasa Afisa Kilimo, alikuwa akienda vijijini anasema elimu imetolewa. Mimi ndiyo mfadhili mkubwa wa vikoba kwenye jimbo langu, wanakwenda kwa mwenyekiti wa vikoba wanasema, naomba uandike barua hapa nakupa shilingi 100,000/=, saini hapa, sema hiki Kikoba, ni Chama cha Ushirika cha Msingi, ni uongo mtupu. Haiwezekani katika mazingira ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kesho, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Bashe, tuseme kesho, stakabadhi ghalani ndio basi haiwezekani, ni jambo baya mno kwa mkulima, tuweke kama tulivyoweka kwenye ada elekezi. Serikali ilisema ije na ada elekezi kwenye shule binafsi, tukasimama kidete tukasema hivi, kila mtu ana fedha zake ampeleke mtoto anakotaka mtoto kusoma shule. Aende Kenya akasome shule, aende Marekani akasome shule, tumuache mkulima kwenye ufuta akauze anakotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nenda sasa hivi Wilaya ya Songwe wakulima wa ufuta wanauza Mbalizi, wanauza Mkwajuni, wanauza Tunduma, wanauza Mbozi they are free, tuwaache wawe free kwa sababu, ndiko wanakofaidika huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkulima katika maisha ya mwaka mzima anakopa fedha za kwenda kujitibu masikini ya Mungu, anakopa fedha kumpeleka mtoto shule mwezi wa kwanza, anakopa fedha kwa ajili ya kuendeshea mifumo ya chumvi, sabuni. Leo hii amechukua fedha pale kwa jirani yake ambapo amemuambia atamlipa ufuta wameandikishana, butter trade wameandikishana, leo Serikali inakuja kusema kwamba, ufuta wote mpeleke pale mkauze kwa stakabadhi ghalani, tunakupa risiti, tutakupa fedha baada ya masaa 48. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii Mbunge nalipa wakulima wangu wa pamba toka mwaka 1995 niko form six, watu walikuwa wanauza pamba hawajalipwa mpaka leo na risiti ninazo, nitakuletea Mheshimiwa Bashe risiti za wakulima wa Songwe wanaodai fedha za pamba, ilikuwa ni mambo ya stakabadhi ghalani. Nazungumza kwa uchungu mkubwa sana naomba ninyamaze. Siungi hoja mkono. (Makofi)