Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza sana Wizara, kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara kwa kazi kubwa waliyoifanya katika uandaaji wa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nielezee kwa ufupi faida za korosho. Korosho tunapata tunda, katika lile tunda tunaweza tukatengeneza juice na wine. Lile bibo lilikauka unaweza ukatengeneza spirit, viwandani, hospitalini na kwenye maabara tuna shida kubwa ya spirit. Wenzetu wa Naliendele wamekwenda mbali kutengeneza spirit kwa kutumia bibo. Sasa hivi wamefikia asilimia 82 ya spirit kwa tunda lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, korosho yenyewe unaweza ukala, wengi wenu mnajua kazi yake lakini unaweza ukatengeneza siagi. Wenzetu wa Naliendele wana siagi ya korosho na imekuwa approved na TBS. Pia ile korosho ukisaga, unaweza ukatengeneza chapati. Aidha, korosho ni tui, unaweza ukapika mboga kwa tui la korosho na ukikutana na mwanamke wa Kimakonde hutamuacha. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nutshell ya ile korosho ni mafuta yanayotumika katika dawa. Unaweza ukapaka kwenye mbao kama alivyosema mwenzangu na ile haitaliwa na mdudu yeyote. Lile bibo ukishakamua ni mashudu na ni mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niiulize Wizara, mambo haya walikuwa wanayajua? Viwanda vingeitumia korosho hii leo tungekuwa wapi? Nina uhakika tungetengeneza wine…

T A A R I F A

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mhata.

SPIKA: Ndiyo Mheshimiwa Cecil.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa kwamba pamoja na hayo anayoyasema, Serikali hii ilikamilisha utafiti wa haya yote anayoyasema ambao unapatikana pale Naliendele kinachosubiriwa ni kufanya implementation. Kwa hiyo, sasa awaulize utekelezaji wa haya yote ili kuongezea wakulima mapato kutokana na zao la korosho utaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampa taarifa hiyo.

SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea Mheshimiwa Yahya?

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, huko ndiyo nilikokuwa nakwenda, namshukuru sana mwenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba wenzetu wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ule Mfuko wa export levy ndiyo ulitakiwa ufanye kazi hizi. Tuna kazi kubwa ya kufufua viwanda vyetu vya wine, kutengeneza viwanda vya mbolea na juice. Kama tungeutumia Mfuko ule vizuri kwa kuwatumia wataalam wetu wa Naliendele, miaka hii mitatu tuliousimamisha tungekuwa tuko mbali sana. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara tutumie Mfuko ule wa export levy ili kuwezesha wenzetu wa Naliendele wafanya utafiti wao wa dhati kutafuta mazao mbadala ya korosho hatimaye viwanda vingi viweze kutekelezwa ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili, kule Jimboni kwetu kumeingia mtafaruku. Kuna barua iliyoandikwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho inayowataka wakulima wote kukatwa Sh.110 kutoka katika mauzo yao ya korosho baada ya kupewa sulphur. Barua ile inachanganya sana. Inasema hata mkulima akipewa mfuko mmoja akienda kuuza tani 20 atakatwa Sh.110 kwa kila kilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mtendaji huyu amekwenda mbali kwa kujiamini kabisa kwa kuwaandikia Wakurugenzi kwamba hayo ni maagizo na lazima yatekelezwe. Hili jambo halikubaliki. Kama mwananchi anakopeshwa mfuko mmoja, kwa nini usimkate kwa mfuko mmoja? Unamkataje kwa idadi ya korosho alizoleta kwa ajili ya kuuza go-down? Hii kitu hakikubaliki.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri, ile barua ifutwe. Mtendaji yule anasema baraka hizi amezipata kwa Wabunge, Wabunge wapi? Ni nani aliyempa idhini ya kuandika barua hiyo? Kwa kweli anatuchanganya na anawachanganya wananchi. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri, Mtendaji huyu usipomuangalia ipo siku tutamtoa ofisini kwake kwa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la minada, Mheshimiwa Waziri amezungumza vizuri sana asubuhi kwamba takriban minada 70 imefanyika ndani ya nchi hii kwa msimu uliopita na minada ile ni mizuri kabisa na mimi naiunga mkono. Hata hivyo, kuna upungufu kwenye minada ile.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Tandahimba imetokana na Wilaya ya Newala lakini utashangaa bei za minada zinatofautiana. Unaambiwa korosho za Tandahimba ni bora kuliko korosho za Newala ambapo jana walikuwa Wilaya moja. Leo kwa kugawanywa tu, bei zinatofautiana. Wilaya ya Nanyumbu, wilaya yangu mimi imetokana na Wilaya ya Masasi. Mwanzo, bei ilikuwa moja kwa kugawanywa tu, bei zinatofautiana, hii ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri uwaangalie watendaji wake kuna hujuma inayofanyika. Haiwezekani korosho za Nanyumbu zikawa na bei ndogo kuliko korosho za Masasi. Wakati tulikuwa wilaya moja bei ilikuwa sawa, leo tunagawanywa, unasema kwamba bei tofauti. Hili jambo halikubaliki. Kwa hiyo, kuna hujuma inayofanyika na haitakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Wizara, pamoja na mazuri yote wanayoyafanya, naomba muwaangalie watendaji wenu wa chini. Wenzangu wamezungumza kuhusu Bodi ya Korosho, mtendaji amepewa mamlaka makubwa sana kwa sababu hana mtu anayemdhibiti. Naomba huyu mtu aangaliwe kwa macho mawili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Yahya.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, mwisho naishukuru sana Wizara naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)