Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu niliotumwa na wananchi wa Jimbo la Kwela na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, kuhusu sekta hii muhimu ambayo inagusa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa. Sitakuwa nimewatendea haki wananchi wa Jimbo la Kwela na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla kama sitaongelea hali halisi ya zao la mahindi ndani ya mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Mheshimiwa Aida amesema hapa na naomba nisisitize kwa umuhimu wake, leo hii inaonekana Mkoa wa Rukwa tumekuwa kama kichwa cha mwendawazimu. Mwaka jana nilipata masikitiko makubwa katika hotuba yake alivyokuwa anahutubia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI wakati huo Mheshimiwa Jafo, akawa anasema kati ya mikoa ambayo yamechangia na kupata mapato ghafi kidogo sana na ya mwisho katika mikoa yote Tanzania ulikuwa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sababu kubwa iliyopelekea tukae mkiani, sio kwasababu sisi hatufanyi shughuli, ni wavivu, hatulimi wala hatujielewi, hapana, wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanajituma sana, tunalima na sisi ndio katika top two katika kilimo cha mahindi nchi hii, Mkoa wa Rukwa ni mmojawapo. Nimekuwa nikifuatilia sana mijadala hapa Bungeni, mwezi Februari nilisimama katika Bunge hili Tukufu, nikaongelea suala la zao la mahindi, lakini pia kuna Wabunge mbalimbali akiwepo Balozi Dkt. Pindi Chana aliuliza swali katika Wizara hii, lakini majibu ya Naibu Waziri yalikuwa ya kukatisha tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakumbuka wakati huo katika Bunge la Kumi na Moja mtu ambaye nilikuwa ninam-rank kama the best of Rukwa Region alikuwa ni Mheshimiwa Naibu Waziri Bashe, alikuwa ni front liner na champion mkubwa wa kupigania zao la mahindi, alikuwa anatoa takwimu unit cost ya production per heka na mauzo anayouza mkulima kwa heka moja. Alikuwa anasema gross loss ilikuwa ni Sh.150,000 kwa mkulima kila msimu. Bahati mbaya wakati huu hiyo gross loss anayopata Mkulima kwa heka moja imeenda mpaka Sh.300,000 yaani unapofika wakati wa mavuno, akijumlisha gharama zake za uzalishaji mkulima wa Mkoa wa Rukwa anapata hasara ya Sh.300,000, hapo hajatunza mazao, afanye hedging asubiri bei itakapopanda, hivi ninavyoongea Sh.18,000 gunia moja, heka moja Sh.700,000…
SPIKA: Mheshimiwa Deus Sangu mimi shahidi yako, nilikuwa nikikaa hapa Mheshimiwa Bashe yupo pale nyuma anashuka jinsi wakulima wa mahindi ambavyo hawatendewi sawasawa kwa hesabu kwa takwimu, sasa leo yupo wapi? (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Yuko hapa.
SPIKA: Haya endelea kuchangia Mheshimiwa.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniunga mkono. Kwa hiyo Mheshimiwa Bashe ni msalaba wake huu, is your baby, naomba leo wakiwa wa Waziri hapa Profesa waje watuambie wananchi wa Mkoa wa Rukwa na Nyanda za Juu Kusini, wanawapa habari njema. Habari ya kusema kwamba mipaka ipo wazi, hiyo sio stori brother, lazima waanzishe marketing intelligent system waende kwenye nchi hizo ambao wanadhani ni masoko, mpaka unaweza ukawa wazi, lakini sio wazi kwa Tanzania pekee, Zambia wanaangalia hiyo mipaka iliyo wazi; Kenya wanaangalia mipaka iliyo wazi; DRC wanaangalia mipaka iliyo wazi na Burundi hivyo hivyo.
Mheshimiwa Spika, sasa wakikaa kwenye madawati huko Wizarani wanasubiria tu kwamba mipaka iko wazi you will wait until the next coming of Jesus Christ. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa Mkoa wetu wa Rukwa, leo hii halmashauri zetu zime-paralyze, hazina mapato, sisi hatuna migodi ya dhahabu, hatuna jambo lolote tunalotegemea zaidi ya zao la mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya hadi mpunga sasa umeshuka bei. Mwaka jana hali ilikuwa ngumu. Halmashauri zetu zote katika Mkoa wa Rukwa zimeshindwa kukusanya mapato. Tumeshindwa kujenga madarasa, tumeshindwa kujenga zahanati, tumeshindwa kuboresha vituo vyetu vya afya, maisha ni magumu watuonee huruma wananchi wa Mkoa wa Rukwa, tumechoka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna solution zinatolewa kwamba substitute, twende tupeleka mikorosho na wakituletea mikorosho its good initiative, lakini haitoshi, wakileta mikorosho ina maana tuache kulima mahindi. Tukiacha mahindi maana yake nchi itaenda kwenye baa la njaa, baadaye wataanza kuhangaika kutafuta mahindi sehemu nyingine. Kwa hiyo, hatutaki korosho iwe ni replacement ya mahindi, tunataka iwe ni alternative tu, anayetaka ku-jump kwenye korosho ataenda, anayetaka ku-jump kwenye mazao mengine ya kimkakati ataenda, lakini hatutaki mahindi yawe replaced, tunataka mahindi yabaki kuwa pale pale, kwa sababu wakati wa njaa sisi ndio mkombozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi ikiingia kwenye matatizo ya njaa, Wizara inakimbilia Rukwa, sasa hivi mazao tumefanya over production wanaanza kutukimbia wanatukwepa na sababu ndogo ndogo. Nilienda front line, tukaenda mpaka wa Waziri Mkuu tukamwambia huu ni mwezi Februari Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba na akaja kusema ndani ya Bunge hili Tukufu kwamba tayari tutaunda timu itakayoenda huko Kongo na Burundi ili ku-secure hayo masoko.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa na dhamira njema na safi, lakini naona watendaji wake hawaendi na sauti ile, ilitakiwa tamko la Waziri Mkuu hapa liwaamshe, waje tukae Wabunge wa Mkoa wa Rukwa na management ya Mkoa wa Rukwa, twende huko, baadaye tutakuta yale masoko yameenda, hatuna soko la mahindi, confidence ya wakulima imepotea, wamekata tamaa.
Mheshimiwa Spika, nawaheshimiwa sana Mheshimiwa Bashe na Mheshimiwa Waziri, sitaki kesho niendeshe mgomo wa Wabunge wa Nyanda za Juu Kusini, tuwawekee mgomo wa Bajeti yao mpaka waje na kauli thabiti, kauli ambayo sasa tukirudi mwezi Julai kwenye ziara kwa wananchi, tuwe tunawaambia jambo linaloeleweka sio stories. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, naomba tu niseme hayo kwa uchache, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)