Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kiukweli mimi kama mkongwe kwenye Bunge hili Wizara hii ilikuwa kati ya Wizara moto sana kipindi hicho palikuwa hapakaliki, lakini sasa hivi naona moto umepoa sana. Kwa hiyo hicho ni kiashiria kwamba Mheshimiwa Lukuvi na timu yake wamekuwa wakifanya kazi kwa viwango vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mwaka 2010 mpaka 2015 mimi nilikuwa Waziri kivuli wa Ardhi na nilitumia muda huo kufanya utafiti mkubwa sana wa migogoro ya ardhi na sikuwa mchoyo nika-share na Mheshimiwa Lukuvi ma-book yangu yale, akayafanyia kazi na anapata kiki kutokana na kazi ambayo nilitumia brain yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Bashiru yuko hapa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM na yeye nilikuwa namsaidia tafiti nilizokuwa nikifanya na yeye wakati huo akiwa ni Mhadhiri akifanya maandiko yake huko na atakubali kama hatakuwa mchoyo wa fadhila. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo nitakuwa local kidogo, nitakuwa Jimbo la Kawe, kwa sababu inaonekana kama vile kumepoa Kawe kidogo. Mheshimiwa Lukuvi, mimi na yeye wakati niko Mbunge wa lile Jimbo tulifanikiwa kutatua migogoro mingi sana na nimshukuru kwa hilo. Tulitatua Nyakasangwe, tukatatua Kunduchi, tukatatua Bunju kwa Somji, tukatatua kile kimgogoro cha miaka kumi na tano Basihaya pale, kuna Mtaa wa Chatembo, cha Chui na cha Simba. Hayo majina yenyewe yanaashiria watu gani wanakaa kule. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, lile eneo lina wakazi 4,000, lile eneo tarehe 13 Juni, 2015, tulienda pale kumaliza mgogoro, alikuwepo Waziri, alikuwepo Katibu Mkuu wakati huo Kidata ambaye sasa hivi ni Kamishina wa TRA, alikuwepo Naibu Waziri kipindi hicho, Anjella Kairuki, Wakurugenzi na timu yake yote walikuwepo. Tukatatua mgogoro husika na wananchi wa eneo lile na alikuwepo pia aliyekuwa Mkurugenzi wa kile kiwanda anaitwa bwana Alfonso Rodriguez kwa niaba ya kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tuna roho nzuri siku 60 ambazo wataalam wa Wizara walikaa pale, wananchi walijigharamia, wakahakikisha wanakaa sehemu nzuri hili upimaji ufanyike. Nini tulikubaliana kwenye kikao na nasema haya Mheshimiwa Lukuvi anajua yeye ni rafiki yangu, tumefanya mengi pamoja, lakini akiona nimeamua kuja kufunguka hapa nataka arekodiwe na Hansard sasa akijigeuka mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maazimio tulikubaliana nini? Kikao cha wananchi kilikuwa na maazimio saba, nitayasoma kwa ufupi:-

(i) Eneo ambalo limekaliwa na wananchi kwa muda mrefu libadilishwe matumizi kuanzia leo tarehe 13 Juni, 2015, kutoka matumizi ya uchimbaji wa madini na kuwa eneo la makazi;

(ii) Wananchi waliotambuliwa wakati wa zoezi la uthamini ndiyo watakaohusika na zoezi zima, wananchi ambao hawakuwepo na walikuja baada ya zoezi hawatatambulika;

(iii) Wakati wa umilikishaji Wizara itatoza tozo ya mbele premium kwa kila kiwanja itakachomilikisha. (Makofi)

(iv) Wizara imekubali sehemu ya malipo ya premium yataenda katika kiwanda na kitasaidia kujenga miundombinu na huduma za jamii kwa zahanati;

(v) Wananchi kwa kushirikiana na Serikali ya Mtaa wataunda Kamati ya Utekelezaji na Usimamizi wa Mpango huo;

(vi) Kazi za uchimbaji mchanga na kokoto hazitaruhusiwa na atakayefanya hivyo atakamatwa; na

(vii) Kazi ifanyike haraka mwezi Oktoba, 2015, mambo yatakamilika, wananchi watakabidhiwa maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akafunga kikao, akadondoka signature hapa, Mheshimiwa Lukuvi pembeni, Mheshimiwa Kidata pembeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazungumza Mheshimiwa Jerry hapa, sisi Wanasheria katika nyaraka ukishadondoka ukaji-commit huwezi kuja uka-change kote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini kimetokea na majina haya signature za wananchi waliohudhuria kikao. Ameondoka Mtendaji Mkuu wa Twiga, akaja Mtendaji Mkuu mwingine, anaanza kuivimbia Serikali, anakuja na terms nyingine, wakati tulikubaliana hapa wananchi watachangia premium, premium kidogo itaenda kwenye kiwanda na nyingine itakuja kurekebisha miundombinu. Mheshimiwa Waziri alienda juzi, Mheshimiwa Tibaijuka alienda akaondoka akasahau kiatu, nashukuru Mheshimiwa Waziri walimstahi, anawaambia wananchi kutoka premium ambayo kawaida ni one percent kama ikiwa Serikali imesimamia mpaka three percent haiwezi kuzidi hapo ya thamani ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wanaenda wanawaambia wananchi watoe 35 percent ya thamani ya ardhi. Kwa sababu, wamethaminisha wakasema square mita pale ni Sh.20,000/=, wakasema wananchi walipe Sh.6,500/= kwenda Sh.7,000/= mwanzoni ilikuwa Sh.8,000/= wakapunguza kidogo kwamba walipe Sh.6,500/= hii nyingine watafidiwa na mwekezaji. Square mita moja Sh.7,000/= wakati tulikubaliana tunalipa premium ambayo ni asilimia moja ya thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kile alichokifanya ni kutaka wananchi wanunue ardhi almost upya. Wananchi wanaokaa eneo lile ni wananchi wa kipato cha chini, wananchi maskini, inakuwaje leo Mheshimiwa Waziri anageuza maneno yake na nimwambie tu kama hafahamu, wananchi wamesema hivi nikufikishie ujumbe, hawatatoka ila wako tayari kulipa premium tuliyokubaliana. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Mheshimiwa Waziri ana burasa ya kuamua kulimaliza hili kwa sababu tulienda vizuri tukagota.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba la Taifa; juzi niliuliza swali hapa, Mheshimiwa Naibu Waziri akajibu, akasema mradi huu utakuwepo kwenye bajeti mwaka huu wa fedha tunaoanza kuutekeleza. Sasa mwaka wa fedha Wizara si lazima kwenye maandishi huku nione. Waziri alisema utekelezaji wa Mradi 7111 ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 142; na Mradi 7112 shilingi milioni 103, miradi yote miwili ina thamani ya shilingi bilioni 245 ambazo Shirika la Nyumba la Taifa liliingia mikataba na wakandarasi wawili toka mwaka 2014. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mradi mmoja umetekelezwa kwa asilimia 20 na mwingine asilimia 30. Mkataba wa kwanza ulikuwa 2014 mpaka 2017 waka-extend mpaka 2019, leo kazi imelala. Mheshimiwa Naibu Waziri atakwambia tulihamishia Makao Makuu Dodoma tukagota. Waziri akasema kulikuwa kuna mikataba haijakaa vizuri tunaifanyia kazi toka mwaka jana hawajajibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na watu wa PAC wako hapa ni mashahidi, anasema ule mkataba na sababu ya nini kukwama, Shirika hivi linavyojiendesha kibiashara limegota limeshindwa kupewa fedha kwa sababu, wamekopa, mwisho wa ukomo wao shilingi milioni 300, wakaenda kuomba kibali Wizara ya Fedha toka 2017. Kwa sababu mradi huu ni viable, unakaa eneo ambalo ni prime, tunaomba mtupe kibali mradi huu utalipa. Toka mwaka 2017 mpaka leo hakuna ambacho kimetokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wananchi wamewekeza zaidi ya shilingi bilioni tatu pale wameshanunua nyumba kabla hazijajengwa, Waziri anatuambia kuna process, ni kweli? Tafiti zinaonyesha tuna upungufu wa nyumba kwenye majiji zaidi ya milioni tatu na kila mwaka nyumba laki mbili zinahitajika, halafu wanakaa hapa wanasema hatuna mapato, yaani hatuna mapato wakati pale Kawe New City iliyokuwa inatarajiwa kuwa na wakazi 50,000, wangeingiza property tax mpaka Mheshimiwa Waziri angekimbia. Hivi kwa nini tunafikiria kimaskini (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie; tusipotekeleza huu mkataba Wizara inaenda kulipa bilioni 100, wakati wamekataa kuipa ruhusu Shirika la Nyumba yaani shilingi bilioni 100 unaenda kumpa mkandarasi bure kwa kuvunja mkataba jamani hii ni akili ama nini? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Halima kengele ya pili imeshagonga.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe Waziri anipe majibu yenye mantiki kwa maslahi mapana ya nchi na Jimbo la Kawe. (Makofi)