Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha wakati wa asubuhi najiandaa kuja kuchangia Wizara hii muhimu, nilimwomba Roho Mtakatifu anipe hekima na busara nichangie Wizara hii muhimu kwa maslahi mapana ya Taifa letu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza kwenye maeneo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni eneo la upangaji, upimaji na umilikishaji; Eneo la pili ni changamoto za sekta ya ardhi; Eneo la tatu ni ushiriki wa sekta binafsi; Eneo la nne ni mashamba yasiyoendelezwa; na eneo la tano muda ukiruhusu, ni Mabaraza ya Ardhi na mwisho nitahitimisha na Shirika la Nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la upangaji, upimaji na umilikishaji; labda nirejee historia kidogo. Mnamo mwaka 1896, kiwanja cha kwanza kilipimwa nchini wakati wa Mkoloni. Hali kadhalika, tangu Uhuru mpaka leo, upangaji ni viwanja milioni sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyosema upangaji, ni hesabu ya viwanja kwenye ramani za mipango miji katika mchakato wa uandaaji wa kiwanja. Ukipima hivyo milioni sita kwa mujibu wa utaalam, unaweza ukajikuta huwezi kupata milioni sita vyote vitapungua kwa sababu ya mokorongo na maeneo ambayo ni hazardous areas.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni upimaji wa viwanja. Viwanja vilivyopimwa tangu Uhuru ni milioni mbili na laki tano tu na viwanja vilivyotolewa umiliki ni takribani milioni moja na laki tano tu. Nilikuwa najaribu kuwasiliana na wenzetu wa Kenya, wenzetu sisi tunasema upangaji viwanja milioni sita, Kenya milioni sita ni hati miliki; mnaona kuna tofauti kidogo. Kwa hiyo nataka kujenga hoja ya namna gani hapa; hoja yangu ya msingi hapa ni kasi ndogo ya upimaji, upangaji na utoaji wa hati nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye ushauri; nitaeleza baadaye kwenye hoja hiyo ya namna gani sasa tunaweza kuongeza uwezo wa upimaji, upangaji na upatikanaji wa hati nyingi sana kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo la pili, kwa sababu ya muda naongea haraka haraka kidogo ila kuna pointi muhimu nitaongeza kidogo maelezo. Niende kwenye eneo la changamoto za sekta ya ardhi. Changamoto za sekta ya ardhi nchini ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya kwanza ni gharama za umilikishaji. Mheshimiwa Waziri atakumbuka alikuwa ukipiga simu kuwataka wananchi waje wachukue hati. Unajua changamoto kubwa inayotukuta ni nini? Kuna gharama inaitwa tozo ya premium, tozo ya mbele, hii gharama ni kubwa. Kwa hiyo wananchi wengi, hasa wa kipato cha chini, wanashindwa kumudu gharama hizi. Kimsingi, tukiziondoa gharama hizi za premium, na Waziri yupo hapa, mjamba wangu, Mheshimiwa Lukuvi, namwambia kwa dhati mwamko wa wananchi kutaka kupata hati utakuwa mkubwa sana na watajitoa kulipia kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la changamoto ni ukosefu wa kanzidata ya uhakika ya hati miliki za viwanja. Leo hii nina uhakika mjomba wangu hapa Waziri Mheshimiwa Lukuvi nikimuuliza anieleze takwimu sahihi ya viwanja vilivyopimwa nchini kidogo kutakuwa na mtihani. Kwa hiyo nishauri Wizara, sasa tuanzishe kanzidata na zaidi teknolojia imekua, tuweke mfumo tu wa teknolojia, watu waweze kujua na mtu yeyote nchini aweze kujua na kila mtu awe na access ya kujua, kwa hiyo ni jambo dogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee eneo lingine la uhaba wa watumishi; ni kweli changamoto kubwa Sekta ya Ardhi kama nitakosea Surveyors hawazidi 600 wa Wizara ambao ukiwachukua na wale wa kwenye halmashauri. Maafisa Ardhi hawazidi takribani labda 2,000 na kidogo. Sasa nchi nzima unaona namna gani kuna huu uhaba wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri na niombe Wizara ya Fedha pia, ione namna ya kuona kutatua kero hii ya watumishi. Pia, leo hii Wizara ya Ardhi imehamisha watumishi kutoka Mamlaka ya Serikali za Mitaa yaani TAMISEMI kwenda Wizara ya Ardhi tuwatengenezee utaratibu bora watumishi wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukienda kwenye mikoa hawana vitendea kazi, utamwambia Kamishna wa Ardhi aende kwenye halmashauri hana gari ataendaje? tutawezeshe ili wafanye kazi nzuri. Pia natarajia kuona hata kwenye wilaya tupeleke vitendea kazi ili kusudi hii kazi iendelee vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine la uwezeshaji mdogo wa shughuli za Sekta ya Ardhi; nishukuru sana, sasa nimeona kuna mabadiliko na niseme kwa dhati kitendo cha Serikali kuanza ku-finance halmashauri ni wazo jema sana, lakini fedha bado ndogo, ndogo sana. Sasa nitoe tu ushauri wangu Wizara ya Fedha tuki-finance Wizara ya Ardhi itatusaidia kupata pato la kutosha kabisa na nitaeleza baadaye namna gani tunaweza kupata fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nijielekeze katika migogoro ya ardhi; unajua migogoro ya ardhi ikiwa mingi ni miongoni mwa indicator za failure ya Wizara. Kwa hiyo namwomba mjomba wangu suala hili la migogoro ajitahidi tulimalize kwa kutumia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya hadi Wenyeviti wa Vijiji kule kwenye ngazi ya wilaya, wafanye kazi hiyo vizuri, ili awe Mamlaka ya Rufaa tu, kwenda kwenye kijiji, ataenda vijiji vingapi, kwa hiyo tuwaachie wale wafanye kazi hiyo kwa uhakika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine la ushiriki wa Sekta Binafsi; hapa naomba nijielekeze kwenye makampuni ya upimaji. Hapa nitulie kidogo, mimi nina success story hapa ya Dodoma, nazungumzia Mbeya na wapi, jamani mbona Dodoma hamsemi, Dodoma hata hela haikupewa imefanya maajabu hapa na sisi tunakaa hapa. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana tu Manispaa ya Dodoma ilivyokabidhiwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu yaani CDA, tulikabidhiwa Mamlaka ile na deni la bilioni 12 na fedha kwenye akaunti ya milioni 400 tukapewa maelekezo na Serikali tupime watumishi wapate viwanja, hatuna fedha, mimi ndiyo nilikuwa Mtendaji Mkuu kama Mkurugenzi wa Manispaa by then. Tulichokifanya tukashauriana ndani ya Jiji la Dodoma tukasema tukitumia watumishi wetu hawa ambao wapo wachache hatuwezi kufanikiwa, tukaalika Sekta Binafsi, mimi nilifanya majaribio, nilitumia pale Michese viwanja 2,000 nikapeleka watumishi wangu wa halmashauri waliniletea vile viwanja baada ya miaka mitatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha tunazoweka kwenye halmashauri tuwaachie wasimame wenyewe bila Sekta Binafsi tunakwenda kufeli asubuhi kweupe. Sekta Binafsi nilivyo-engage makampuni haya yametusaidia Dodoma tukapima viwanja 200,000; sikupata fedha Serikali Kuu, sikwenda kukopa mkopo benki, hii ni success story tukitaka kujifunza tusiende Ulaya mje Dodoma hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua wakati mwingine huwa tunaamini ngozi nyeupe, Kunambi ningekuwa ngozi nyeupe hapa wangeamini, sasa kwa sababu ni Mtanzania huwa hatutaki, lakini tujifunze tu na sisi ni wadau, kwa sababu tuna uwezo wa kufanya maajabu ndani ya Taifa hili. Kwa hiyo Dodoma ni success story na nadhani Wizara ya Ardhi wachukue kama model.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nimpongeze Waziri juu ya suala la mfumo ILMIS - Integrated Land Management Information System. Kengele?

MBUNGE FULANI: Bado.

GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa mfumo ule, kwa sababu ukienda Dar es Salaam kuna mafanikio, ameuleta Dodoma na nimwambie kwa dhati, Dodoma viwanja hivi 200,000 vinaenda kupata hati kupitia ule mfumo, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu Mheshimiwa Waziri ule mfumo sasa aupeleke kwenye halmashauri zote nchini, kwa sababu gharama ya ule mfumo Mheshimiwa Waziri, Afisa Ardhi mmoja anaweza akatengeneza hati 300 kwa siku. Kwa hiyo kwa sababu ya uhaba wa watumishi tulionao, ukimtumia Afisa Ardhi mmoja ukampa server, akawa integrated akawa na communication na Kamishna na Msajili kule na ana computer yake, ana-server na printer, yeye kazi yake ni kubofya tu taa, hati 300 zinatoka. Leo hii tunatengeneza hati bila mchapa hati yule anachapa hati 10 kwa siku, tutafika 200,000 kweli hapa Dodoma. Kwa hiyo, niishauri Wizara kwa dhati kabisa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo la mashamba yasiyoendelezwa, pale jimboni kwangu Mlimba kuna Shamba la Kambenga ekari 1,000 hazijaendelezwa Serikali ipo. Pale Mlimba kuna Shamba la Serikali hekta 5,000 Kata ya Mgeta hazijaendelezwa, mwaka wa tano Serikali ipo. Kuna Shamba la Balali ekari 2,000 halijaendelezwa lipo. Waziri anapokuja kuhitimisha hapa bajeti yake anieleze mjomba wangu kwa dhati nini mpango sasa wa Wizara kwenda kuyaondoa mashamba darasa haya ili wananchi wa Mlimba wapate maeneo na mashamba walime.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine niende haraka haraka, ni eneo hili na kwa dhati kabisa juu ya Mabaraza ya Ardhi, ukienda kwenye level ya Mabaraza ya Kata wale siyo Wanasheria na bahati nzuri uliyekalia kiti wewe ni Mwanasheria utanisaidia kwenye eneo hili, wale hawapaswi kutoa maamuzi kwa sababu bahati mbaya zaidi maamuzi yao yale yanakuwa ni rufaa kwenye Mabaraza ya Wilaya. Ushauri wangu wawe wasuluhishi tu, wale wanaosuluhishana wakishindana basi rufaa iende kwenye Baraza la Ardhi la Nyumba na Wilaya ndiyo lifanye maamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa dhati kabisa niombe, Mungu atubariki sote. Ahsante sana. (Makofi)