Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Bismillah Rahman Rahim.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuchangia nami katika hotuba hii ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambayo ni muhimu sana kwa maslahi ya wananchi wetu, hususan wanyonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kukushukuru wewe, vile vile nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na Naibu Waziri na baadhi ya watendaji wa Wizara hii. Kwa nini niseme baadhi ya watendaji, nitatoa ufafanuzi mbeleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wakati tunapochangia sekta tatu, lazima tuoneshe hisia za ukaribu zaidi; Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwa sababu sekta hizi zinawagusa asilimia kubwa sana ya Watanzania na hususan wenye kipato cha chini ambapo wengi wa Wabunge tunatoka katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitagusia kwenye Sekta ya Uvuvi. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, kwa kweli ameanza vizuri. Kwa nini ameanza vizuri, amekuwa tofauti na wale wengine ambao wanawachukulia wavuvi kama maadui zao. Baadhi ya wengine waliopita tuliwaona, walikuwa wanahisi kwamba kutekeleza majukumu yao ni kuwanyanyasa, kuwaadhibu wavuvi wetu, jambo ambalo siyo sahihi. Mheshimiwa Waziri huyu amekuwa msaada mkubwa sana kwa wavuvi wetu, Mheshimiwa Waziri hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hongera hizo, lakini bado kuna changamoto kwenye Sekta hii ya Uvuvi na tunapozungumzia changamoto hizi, ni kwenye suala la kanuni. Kwa kweli kanuni ambazo zimetungwa hivi karibuni haziko rafiki na wala haziwasaidii wavuvi wetu. Kwa mfano, kuna kanuni ambayo inakwenda kuzuia uvuvi wa ring net kwamba uvuvi huu unaharibu mazingira. Nataka kusema kwamba siyo kweli kwamba uvuvi wa ring net unaharibu mazingira. Ila inaonesha kwamba kuna shirinikizo fulani, kuna watu ambao wanajaribu kuwaonea wavuvi kwa kisingizio cha uvuvi haramu au cha kuharibu mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubaliane kwamba shughuli zote za binadamu kwa njia moja ama nyingine zinaharibu mazingira. Tukizungumzia kilimo, kinaharibu mazingira, tukizungumzia uchimbaji madini, unaharibu mazingira, viwanda vinaharibu mazingira, utalii unaharibu mazingira, shughuli zote za binadamu zinaharibu mazingira; lakini hatuwezi kutumia kigezo hiki kuwadhalilisha wananchi. Licha ya kwamba shughuli za binadamu zinaharibu mazingira, lakini lazima maisha ya binadamu yaendelee. Ni lazima binadamu afanye shughuli zake za kujipatia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa ufafanuzi atueleze ni lini kanuni hii inakwenda kufanyiwa mabadiliko? Vinginevyo hapa patachimbika kwa sababu wavuvi wetu wanapata dhiki kubwa sana kutokana na kanuni hii. Lazima niseme kwamba tunapotunga kanuni au sheria lazima tuzingatie utekelezaji wa sheria hizo. Hivi unatunga kanuni ya ring net kwamba wavuvi wakavue maji mita 50, wapi na wapi? Ukiangalia wavuvi zana wanazotumia ni duni, au tunataka tupate mayatima wengi na wajane wengi? Kwa sababu mvuvi anapokwenda maji mita 50 ni kutafuta kifo tu, hakuna kingine, kutokana na zana wanazotumia, ni duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ukisema labda ring net wafanye uvuvi wa usiku, haiwezekani kwa sababu samaki wengi wanapatikana muda wa mchana, usiku huwezi kumvua samaki kama aina ya jodari, lazima uvue wakati wa mchana. Vilevile wakati wa usiku unapomvua dagaa, mpaka asubuhi tayari ashaharibika; na ukizingatia ring net ndiyo uvuvi ambao unabeba wavuvi wengi. Boti moja ya uvuvi wa ring net wa mchana inachukua wavuvi kati ya 40 mpaka 100, lakini uvuvi wa usiku unachukua wavuvi 10 mwisho wavuvi 15. Hebu tuangalieni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, tunapozungumzia Sekta ya Uvuvi, wananchi walio wengi wamejiajiri katika sekta hii. Mfano ulio hai, hebu tuangalieni soko la ferry, umati ambao uko pale; wote wale wanategemea Sekta ya Uvuvi. Nenda Mafia ukaangalie akina mama wanaojiajiri kwenye Sekta ya Uvuvi. Tunaweza kuiangalia Sekta ya Uvuvi kwa kuangalia mchango kwenye pato la Taifa, hii haiko sahihi. Pamoja na mchango ulioko kwenye pato la Taifa lakini Sekta hii ina tija kubwa kwa maslahi ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mifano iliyo hai. Nenda katika Soko la Ferry, pale pana akina mama ntilie wanategemea Sekta ya Uvuvi, pana bodaboda wanategemea hii, pana daladala, hata Ferry inayovusha, abiria wengi wanakwenda kwenye Soko la Ferry kutokana na Sekta ya Uvuvi. Hata ukienda Kisiwa cha Mafia, akina mama walio wengi au wananchi walio wengi wa Mafia wanategemea Sekta ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tujiulize tunapokwenda kuzuia uvuvi wa ring net, tunategemea wananchi wetu waishi katika maisha gani? Lazima tuzingatie. Kanuni hizi, nikwambie ukweli, inaonekana kuna shinikizo fulani. Watendaji wako Mheshimiwa Waziri wa ngazi za juu mara nyingi wanatuambia kwamba umeunda Tume ya kwenda kufanya utafiti, nakupongeza sana lakini katika Tume ikija kufanya utafiti inaonekana kuna vitu vitatu. (a) Tume hii haina elimu ya kutosha juu ya uvuvi huo. (b) kama siyo hivyo, Tume hii haishirikishi wadau ipasavyo; na kama siyo hivyo, Tume hii haielezi ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi wa ring net hauvui samaki walio chini, wanavua samaki ambao wako juu. Isitoshe, uvuvi wa bahati kuu kama Bahari ya Hindi, hatuwezi kuzungumzia ufugaji wa samaki kama unayefuga samaki kwenye bwawa. Kwa sababu samaki wanatembea masafa ya mbali. Unaweza kufuga samaki Tanzania akaenda kuliwa Kenya. Sasa lazima tuangalie vizuri tunavyozungumzia masuala ya ufugaji wa samaki kwenye bahari kama Bahari ya Hindi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Omar Issa Kombo kwa mchango mzuri.

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. Ingawa muda umekuwa mfupi, tutakutana na Waziri tuongee vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)