Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YUSTINA E. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu ya sasa ni kweli kwamba Tanzania ni ya pili katika Afrika kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia. Mifugo hii mingi hii, asilimia 90 ni kosafu ya asili; na kwamba asilimia 96 ya mifugo hii huchungwa na wafugaji wa kuhamahama na wafugaji wakulima. Hata hivyo, mifugo hii katika tasnia ya nyama inachangia asilimia 90 na maziwa inachangia asilimia 70; na kwamba takribani inatoa vipande vya ngozi milioni tano, kwa maana kutoka ng’ombe vipande milioni 2.6 na wanyama hawa wadogo mbuzi na kondoo vipande milioni 2.6. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na baraka ya namna hii, Tanzania ambayo ni ya pili Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, lakini ni ya tatu kwa utapiamlo wa udumavu. Inasikitisha, kwa sababu asilimia 45 ya Watanzania wana udumavu; na athari ya udumavu ni kuathiri ukuaji wa akili pamoja na ukuaji wa mwili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimehusisha hizi kwa sababu gani? Lengo la msingi la ufugaji halijaweza kutimizwa kwa sababu tunapofuga lengo la kwanza ni kujitosheleza kwa chakula, ni lishe; na lengo la pili ni ziada sasa ili tupate fedha kwa ajili ya kujipatia maisha bora; elimu bora, maji salama, makazi salama na afya nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukija kwenye lishe ndiyo tunaona, kwa mfano, Watanzania wanakunywa wastani wa lita 47 ya maziwa kwa mwaka, badala ya kiasi kinashoshauriwa cha lita 200 kwa mwaka. Watanzania hawa wanakula wastani wa nyama kilo 15 badala ya kilo 50 kwa mwaka kwa mtu mmoja na wanaweza kula mayai takribani 106 badala ya mayai 300 kwa mwaka kwa mtu mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ziko nyingi na changamoto. Unaona kwamba upatikanaji wa bidhaa hii ya mifugo ni mdogo, lakini kwa nini? Kwanza, tunakuja kwenye changamoto ya kosafu, hatuna sehemu yoyote ya kumlaumu huyu mchungaji au mfugaji. Atatoka asubuhi na mifugo yake ataenda kuchunga akirudi jioni anakamua lita moja au lita mbili ya maziwa. Atachunga ng’ombe wake huyu miaka mitano, sita akienda kuuza anaishia kwenye kilo 60, 70 anauza kwa shilingi 200,000/= pamoja na muda wote anaoupoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri sasa mkakati wa kwanza ni kwenye kwenda kubadilisha kosafu ya mifugo. Hii mifugo haina tija. Haya mambo yanawezekana. Nitoe mfano mdogo tu kwa wakulima. Hata hao wakulima zamani walikuwa wakitumia mbegu zao za kienyeji, lakini baada ya Serikali kuleta mbegu ya ruzuku kupitia vocha, wakulima wametoka kwenye kuzalisha ile gunia tano au nane kwa ekari, sasa wanazalisha gunia 15 mpaka 20, hawatarudi huko nyuma. Kubadilisha kosafu faida yake ni kwamba, wakulima watapunguza kundi kubwa la mifugo ambalo halina tija na linaharibu mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ziko nyingi za kuweza kuboresha mifugo; kuna magonjwa ya mifugo ambayo sisi tunaweza kuepukana nayo, ukiacha magonjwa ya milipuko. Kwa mfano, kupe na minyoo ni tatizo kubwa kwa mifugo, lakini kumbe mwarobaini wake ni kuwa na majosho. Tufanye proper dipping. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji siku hizi wengine wanapaka paka tu mifugo kwa kutumia spray, lakini ile sheria ya zamani kwamba ng’ombe wote wa Kitongoji, ng’ombe wote wa Kijiji wanaogeshwa kwa pamoja sasa hivi wameacha. Kwa hiyo, wakiogeshwa kaya fulani, kaya nyingine hawajaogeshwa, ina maana lile tatizo la kupe lipo na ndilo linalosumbua. Ndiyo maana tunaona asilimia ya vifo vya mifugo ni kutokana na magonjwa ya kupe. Kwa hiyo, tuna uwezo mkubwa sana wa kuangamiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majosho ya toka zamani ya wakoloni, yamechakaa huko vijijini, ni mabovu. Ni kwa nini sasa Wizara isihakikishe kwamba maeneo yote ya wafugaji wana majosho ya kuogesha mifugo yao ili kuachana na tatizo la kupe na kuondoa minyoo kwa mifugo ambayo pia inachosha mifugo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni hili la wafugaji wetu kuhangaika kwa ajili ya ukosefu wa wataalam wa mifugo. Mfugaji siku hizi anatibu mifugo yake mwenyewe, lakini tunatengeneza u-resistance wa magonjwa. Kwa sababu, wanapiga dose kubwa, wanachanganya madawa haya kwa ajili ya kukosa maelekezo. Kuna umuhimu sana wa kuboresha huduma za ugani na wataalam wa mifugo wakakaa karibu. Hili siyo kundi la kudharau, kundi la wafugaji ni wakubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ifikirie namna gani sasa kurejesha; kwanza tulikuwa na veterinary centers kwenye kata, zimekufa; mfugaji hawezi kujua hata mahali pa kwenda, anabahatisha tu. Marafiki wa karibu wa wafugaji sasa wamekuwa ma-agrovet. Akifika kwenye maduka ya wakala ndio ashauriwe dawa hii na dawa hii; na wale ni wafanyabiashara, anaweza akamshauri mfugaji dawa ni hii akachanganya dawa za aina nyingi pengine bila kujijua. Kwa hiyo, utaalam bado ni muhimu kama tunataka kuwasaidia hili kundi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatupati tija kwa sababu usindikaji unafanyika kwa kiwango kidogo sana. Tuna viwanda takribani 81 vya kusindika maziwa; na vingekuwa na uwezo wa kusindika lita hata milioni 276, lakini kwa sasa vinasindika lita milioni 56 hivi kama sikosei. Ni kwamba maeneo ya wafugaji ni maeneo yapo ndani, hizi lita mbili, mbili au lita tano, tano, kama tungeweka collection centers huko kwenye maeneo ya wafugaji vijijini au kwenye Kata, hizi zingeweza kukusanywa, zikapelekwa kiwandani na tukawa na maziwa mengi, tukaongeza hata hiki kiwango cha unywaji wa maziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu tuwaambie kuwa Halmashauri pengine kwa Wakurugenzi, maeneo ya wafugaji mara nyingi wanakaa mbali na soko. Soko ni miji ile midogo, hakuna mtu anaweza kutembea kilomita 30, 40 kupeleka lita mbili au tatu ya maziwa. Kungekuwa na collection center wapeleke maziwa, bado ingekuwa ni kipato kizuri tena hasa kwa akina mama. Maana anajua ukipeleka maziwa kuanzia Jumatatu, Jumanne, Ijumaa anapokea hela yake ya lita tano, tano; ni nyingi ingeweza kufanya kitu kikubwa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. JUSTINA E. RAHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizi collection centers ni muhimu kwa ajili ya… (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umeisha.
MHE. JUSTINA E. RAHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)