Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo. Kabla sijachangia naomba ni-declare interest mimi ni muumini wa matokeo, yaani mimi ni mtu ambaye naamini kwamba maneno matupu yanachosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka na miaka tangu wazee wetu wako shuleni na pengine wengine wazee wetu baadhi walikuwa hawajazaliwa mpaka leo bado tunazungumza kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa. Nafikiri kauli hii ndio inayosababisha kutufikisha hapa leo. Unaweza kuvunja uti wa mgongo ukaendelea kuishi ila ukikosa oxygen utakufa.

Mheshimiwa Spika, nafikiri ipo haja ya kubadilisha kauli ya kilimo kwamba ni uti wa mgongo wa Taifa na tutafute kauli nyingine pengine inayofanana na kwamba kilimo ni oxygen ya uchumi wa Taifa. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa mmesikiliza hoja yake, hoja kubwa kweli hii. (Kicheko)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilimo kimesemwa ni uti wa mgongo wa Taifa, ndiyo maana bajeti ya Wizara ya Kilimo tangu mwaka 2016 mpaka 2021 imetekelezwa chini ya asilimia 50. Ukitafuta average ya utekelezaji wa bajeti mwaka ambao ilitekelezwa kwa kiwango kikubwa ni asilimia 42 mwaka 2018/2019, the rest ukitafuta average ni asilimia 19 tu. Kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo unaweza kuvunja uti wa mgongo ukaendelea kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa ndio maana sasa hivi ukienda Nane Nane Dodoma unakuta kuna pilikapilika za maandalizi ya Nane Nane, kikishafika kilele cha Nane Nane watu wanafunga biashara zao unakuta mapori. Hii ni kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, vijana wetu ambao wako Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), wanakaa miaka yote darasani wanakwenda field miezi saba tu, kujifunza kuotesha mbegu, kuweka mbolea na kuotesha kila kitu mpaka mwisho kwenda kwenye masoko. Kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo Tanzania tuna eneo linalofaa kwa kilimo hekta milioni 44, lakini hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini mpaka sasa tumetumia hekta 561,383. Target ya Serikali ni kutumia hekta 1,200,000 ifikapo 2025 kwa sababu kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, kwa hiyo unaweza kuvunja uti wa mgongo na ukaendelea kuishi.

Mheshimiwa Spika, kilimo chetu kina changamoto kubwa sana bado Tanzania tunalima kama Adamu na Hawa walivyolima Eden. Tunategemea mvua na kudra za Mwenyezi Mungu, katikati ya mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, katikati ya mabadiliko makubwa ya tabia nchi bado tunazungumza agriculture wakati dunia inazungumza agritecture. Dunia inakwenda kwa mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, tunaendelea kuvunja uti wa mgongo tukitegemea tutafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya uchache wa muda niende kwenye kutoa ushauri tufanye nini. Jambo la kwanza, nashauri kilimo kisizungumzwe kama sekta ya maendeleo wala kisizungumzwe kama mfumo wa maisha life style kizungumzwe kama big money-making business. Kilimo kwa ujumla duniani ni dhahabu ya kijani, tuzungumze kama money-making business siyo desturi kwamba ni jambo la kimaendeleo, ndiyo maana tunafanya haya tunayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, michango ya Waheshimiwa Wabunge inaonesha namna gani tunakwama sehemu. Hatuwezi kutatua tatizo hili kwa kuweka solution za pamoja ni lazima tuwe na solution za muda mfupi na za muda mrefu. Jambo la kwanza na la msingi, tuna watu ambao wako kwenye finger tips zetu, Maafisa Ugani, ni watu wako Waziri, nashauri tu-militarize sekta ya kilimo, tuibadilishe sekta ya kilimo iwe agricultural machinery. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma bajeti ya mwaka jana ya Mheshimiwa Japhet Hasunga wakati yuko Waziri, vitu vilivyobadilika ni kipaumbele kilichokuwa cha tatu kinakuwa cha pili kilichokuwa cha nne kinakuwa cha sita. Mimi ni muumini wa mabadiliko, mimi ni muumini wa matokeo, tunataka matokeo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)