Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa wingi wa rehema kwa jinsi ambavyo alituchagulia viongozi kwa ngazi zote; nikianza na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Joseph Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu; na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa.
Pili, napenda kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Busokelo ni Jimbo ambalo tunalima mazao ya chakula na mazao ya biashara. Mazao ya chakula tunayolima ni kama yafuatayo: ndizi, mahindi, maharage, viazi mviringo na viazi vitamu, matunda mbalimbali kama maparachichi, matunda damu na mengineyo. Mazao ya biashara ni kama yafuatayo: mbao, chai, kokoa, kahawa pamoja na hiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazao hayo yote, hatuna hata kiwanda kimoja kwa ajili ya kuchakata mazao hayo yote. Inasikitisha sana kuona mkulima, tena wa jembe la mkono analima kwa taabu sana, pembejeo haziwafikii kwa wakati, zinakuja wakati muda usiofaa. Kwa mfano, mbolea za kupandia zinakuja wakati wa kupalilia na mbolea za kukuzia zinamfikia mkulima wakati anavuna. Mbaya zaidi mkulima huyu akifanikiwa kuvuna,hapati sehemu za kwenda kuuza ama kuchakata (viwanda vidogo) ili mazao yao yapate thamani kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri awakumbuke wananchi hawa wa Busokelo kwa kututafutia wawekezaji wa mazao kama kokoa, ndizi na mahindi pamoja na viwanda vya mazao ya ng‟ombe mfano, maziwa (kiwanda cha maziwa) Kata ya Bonde la Mwakaleli (Isange, Kandete, Lubeta na Mpembo).
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kutafuta wawekezaji kwenye viwanda vya gesi aina ya cabondioxide gase Co2, pamoja na umeme wa joto ardhi Geothermal eneo la Ntaba, Kata ya Ntaba ndani ya Busokelo Mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana tuwe na kiwanda cha kusindika kokoa kwa sababu wakulima hawa wanalima kwa wingi sana hasa maeneo ya lufilyo, Ntaba na Kambasegela ili thamani ya kokoa ipande na mkulima aweze kupata zaidi kuliko hivi sasa na itaongeza morali zaidi kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya Jimbo la Busokelo ni mibaya sana hasa kipindi hiki cha mvua na hivyo imepelekea zaidi ya tani nyingi sana za ndizi na maparachichi kuharibika na hivyo kusababisha umasikini zaidi kwa wakulima hawa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, ni muhimu sana viwanda hivi vikajengwa maeneo husika ili hasara ambayo inatokana na kuharibika kwa miundombinu iweze kuepukika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo hapo juu, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja.