Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi uliyonipatia niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo kuwasemea waajiri wangu hususan wakulima na wananchi wetu wa Mkoa wa Manyara na pia nichukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kupigania hii Wizara ya Kilimo, nimpongeze sana Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa waliyoifanya na kusaidia hasa Mkoa wetu wa Manyara kipindi ambacho tulikuwa tumepata janga la kuvamiwa na nzige kwa kweli walifanya kazi kubwa sana hawakulala walihakikisha wamelitatua jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba Wizara hii ya Kilimo inatakiwa sasa iweke jitihada za pekee kuhakikisha kilimo kinamkomboa mwananchi ambaye anayejishughulisha na kilimo. Mkoa wetu wa Manyara ni Mkoa uliobarikiwa sana ni Mkoa ambao una ardhi nzuri sana lakini ni Mkoa ambao unajishughulisha na kilimo cha mazao ya aina yote yanayolimwa Tanzania hii.
Mheshimiwa Spika, lakini kulingana na changamoto inayoikumba hii sekta ya Kilimo wananchi wetu wengi wamekata tamaa na hasa kazi hii ya Kilimo, ikiwepo baadhi ya mazao sasa hivi katika Mkoa wetu watu wengi wameacha kushughulika nayo kwa maana ya kwamba wanakosa vitendea kazi wanakosa pembejeo ikiwepo mbegu na mbolea. Mbegu na mbolea katika Mkoa wetu wa Manyara vinachelewa sana kufika kwa muda muafaka wa wakulima.
Mheshimiwa Spika, hii imesababisha wananchi wetu wameacha sasa hivi kujishughulisha na Kilimo cha Ngano, wameacha kujishughulisha na Kilimo cha Pareto wamekatishwa tamaa kabisa na kujishughulisha hata na kilimo cha vitunguu saumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata mbolea zinapofika au mbegu zinapofika katika maeneo yetu upatikanaji wake ni mgumu lakini pia gharama ni kubwa ukilinganisha na hali halisi ya wakulima wetu. Sasa hivi ukiangalia wananchi wetu wanaojishughulisha hata na Kilimo cha ngano wanaojishughulisha na Kilimo cha Pareto Kilimo cha vitunguu saumu wale wachache waliobaki wanalima kilimo ambacho hakiendani hasa na hali halisi au kilimo kinachowaletea tija wananchi hawa wameendelea kutumia mbegu ambayo haistahili kabisa mwisho wa siku wanafanya kazi kubwa na matokeo ni madogo mno. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi hawa wanalima wanatumia nguvu kubwa sana wanatumia gharama kubwa sana lakini hawanufaiki na Kilimo hicho. Niende sambamba katika kuelezea katika suala zima la masoko tunasema jembe halimtupi mkulima kiukweli sasa hivi kilimo kimekuwa ni kilio kikubwa sana kwa wananchi wetu, wananchi wetu wanatumia gharama kubwa sana katika kulima lakini wanapofika katika suala la masoko kiukweli mazao yao yananunuliwa kwa gharama ndogo mno kitu ambacho kinawakatisha tamaa kuendelea kufanya kazi ya kilimo lakini pia kuendelea kumdidimiza na kumgandamiza huyu mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna watu wanaitwa madalali hawa watu wanafika kwenye maeneo yetu kule mashambani wananunua mazao yakiwa mashambani, mkulima kwa sababu hana uhakika wa masoko anaamua kuuza kwa gharama ndogo sana na wanaofaidika ni wale madalali ambao wakishafanikiwa kununua kutoka kwa mkulima wanaenda kuuza kwa gharama kubwa kwa hiyo faida kubwa inakwenda kule kwa madalali. Sasa ni muda muafaka Wizara hii kuwahakikishia wakulima masoko yenye uhakika ili kama kweli tuna nia ya dhati kabisa kumkomboa mkulima, tuna nia ya dhati kabisa kufanya wananchi wetu na Watanzania na vijana wetu wafurahie kilimo ni kuwapatia soko la uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni namna gani sasa Wizara imejipanga kuangalia masoko ya uhakika ukizingatia kwamba katika ndani ya Afrika tuna masoko mengi ukiangalia kama nchi ya Congo, Zimbabwe.
Je, Wizara imejiandaaje sasa kutafuta masoko nje ili wananchi wetu wanapofika ule muda wakishavuna mazao yao waweze kupata soko la uhakika na kuuza mazao yao ili waweze kupata faida. Sambamba na hilo imeongelewa sana kuhusu kuamini kwamba tukitegemea mvua katika kilimo imekuwa sio njia sahihi na yenye uhakika kwanini sasa Wizara isione tuwekeze nguvu kubwa katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Regina.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi uliyonipa. Naunga Mkono hoja.