Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kunikumbuka na kunipa nafasi ya kuchangia sekta hii nyeti ya kilimo, ungetoa nafasi kwa kila Mbunge hapa angekuwa na jambo la kusema kuhusu sekta hii nyeti sana inayogusa maisha ya Watanzania na ni kwa sababu aidha kila mmoja hapa alikuwa na kura yake moja ya mkulima au mfugaji, na huenda karibu Wabunge wengi hapa ni wakulima.
Mheshimiwa Spika, sekta hii ya Kilimo inagusa maisha ya Watanzania wengi kwa asilimia zaidi ya 60 tukiongelea asilimia 65 hii ni kwa sababu ya wastani wa vijijini na miljini.
Mheshimiwa Spika, lakini ukienda kwenye Majimbo ya vijijini huko asilimia zaidi ya 90 ni wakulima lakini ndio sekta iliyokumbwa na changamoto nyingi tu ukiangalia katika hatua zote za mnyororo wa thamani katika sekta hii ya kilimo kwanza uzalishaji una changamoto nyingi kwasababu kuna uzalishaji mdogo kwa hekari, ukisogea kwenye usindikaji kuna changamoto ukienda kwenye masoko kuna changamoto kibao.
Mheshimiwa Spika, hatujaweza kuwekeza vya kutosha katika sekta ya kilimo ili kumtoa mkulima huyu katika hatua aliyonayo kumsogeza katika mapinduzi na kumtoa katika umaskini kwa sababu changamoto hizi zote zina dawa. Tunaongelea habari ya mbegu lakini kuna dawa, inatakiwa tutoe fedha katika mafiga matatu ya kuweza kutuletea mbegu bora wakiwepo TOSCI, TARI na ASA ili wakulima hawa wapate mbegu bora wanazozihitaji.
Mheshimiwa Spika, watu wanaongelea kuhusu habari ya alizeti, mbegu zinazotolewa na ASA ya record huwezi kufananisha na mbegu ya hybrid ambayo inauzwa bei ya juu takriban Sh.35,000 kwa kilo kwa sababu mbegu zinazotakiwa na wakulima ni mbegu bora na chotara. Ni kwa nini sasa tusitatue changamoto hii ya kutokuwa na mbegu bora wakati tuna fursa nyingi na za kutosha?
Mheshimiwa Spika, katika uzalishaji mdogo mimi naenda kugusa zao la ngano. Tabia ya ulaji ya Watanzania sasa imebadilika na kwamba ngano ni kati ya mazao muhimu ya chakula. Ngano sasa ni zao namba nne ikifuatiwa na mahindi, mihogo na mchele. Ukitaka kuhakikisha kwamba ngano utaona Tanzania sasa bakeries nyingi zimefunguliwa kila mtaa na ukienda kwenye vioski vya vijijini wanauza mikate na maandazi.
Mheshimiwa Spika, lakini inasikitisha sana kwamba Watanzania ngano tunayokula siyo ya kwetu, tunaingiza ngano kwa dola nyingi za Marekani. Sisi tunatafuta foreign currency kwa ajili ya kununua vitu vingine lakini kumbe tunaagiza chakula. Hii haikubaliki kabisa. Watanzania kwenye miaka ya 70 hadi 80 we were good producer of wheat…
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge wa Longido unakata katikati ya mwongeaji na Spika, endelea Mheshimiwa.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunilinda. Naendelea kuelezea masikitiko yangu kwamba kwa kweli si sahihi na haikubaliki kwa Watanzania kuingiza ngano kwa fedha za kigeni kwa sababu tulikuwa na mashamba makubwa….
T A A R I F A
SPIKA: Taarifa, nimekuona Mheshimiwa Asia.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, napenda tu kumpa taarifa mchangia hoja kwamba hata Wilaya ya Hanang ambapo ndiyo sehemu kubwa ya kilimo hiki cha ngano tunaiomba Wizara ije kuona kwa sababu mashamba mengine yamepewa wawekezaji lakini wawekezaji wale wanalima kiwango kidogo sana na eneo kubwa linabaki kuwa pori.
Mheshimiwa Spika, hata Serikali yenyewe ina eneo la ekari 12,000 ambapo halmashauri imechukua eneo dogo kwa ajili ya kukodisha wananchi lakini eneo lingine Serikali imeliacha limekuwa pori. Sasa tuombe kwa sababu Serikali ilishaamua kukikuza kilimo hiki cha ngano na kukifanya kuwa cha biashara basi waje wawekeze kweli kweli kuanzia kwenye mashamba ya wawekezaji lakini hata kwenye mashamba yenyewe ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Taarifa hiyo Mheshimiwa Yustina unaipokea?
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana mdogo wangu Asia, naipokea taarifa yake kwa mikono miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna historia kwa mfano kama alivyotoa mfano mdogo wangu Hanang tukishirikiana na Canada miaka hiyo yale mashamba yote sasa hivi yamegawanywa kwa wafugaji, wakulima wadogo wadogo na private sector wame-fragment mashamba yale makubwa katika vipisi vidogo vidogo hatuwezi tena kulima ngano. Kilimo cha ngano ni lazima kifanyike katika mashamba makubwa kwa sababu kilimo hiki ni mechanical agriculture kwa sababu ngano utapanda kwa planter, utapalilia kwa mashine na utakuja kuvuna kwa combine harvester, hatuwezi kuachia wakulima wadogo wadogo. Mashamba ya NAFCO yale wamechukua wawekezaji, yamekuwa privatized katika sekta binafsi na hatukuwapa incentive kwa sababu ngano ilikosa bei. Naishauri Wizara ije na mpango kwamba sasa hatutaendelea kulishwa ngano na nchi za nje na kwamba tutaokoa hela hizo za kigeni zinazoenda kununua ngano na kwamba mpaka miaka mitatu kuanzia leo tutakuwa tumejitosheleza kwa soko la ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu mwingine unaenda kwenye upotevu wa mazao baada ya mavuno. Ni kweli kabisa tumeacha wakulima hawa wakihangaika. Nashukuru Wizara na naipongeza kwamba imekuja na teknolojia ya kutumia vifungashio ambavyo haviingizi hewa (hermetic). Kuna serial za chuma, plastics lakini na mifuko hii ya PICS. Hii ni namna pekee ambayo wakulima hata sisi walaji wa chakula tutakuwa salama.
Mheshimiwa Spika, baada ya wakulima hawa kutumia viatilifu vingi vya unga mara nyingi wanakuta mahindi yao yamepekechwa na kwa ajili hiyo wanachanganya madawa mengi kina Actel, Duduba, unawakuta mahindi yako mazima sokoni kumbe tunaenda kula sumu. Kwa ajili hiyo hii mifuko ya PICS na vifungashio vingine ambavyo sasa vinauzwa ghali, serial ya chuma ya kuweka magunia matano inaenda mpaka laki na kitu, mifuko hii inauzwa Sh.5000, tunaomba sasa Serikali ifanye namna yoyote ya kuweza ku-subsidies ili angalau mifuko hii basi wakulima wapate kwa Sh.2,500 hadi Sh.3,000 waachane na kutumia viatilifu hivi ambavyo vina kemikali nyingi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.(Makofi)