Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tumbe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Spika, mimi nawaomba Waziri na Naibu Waziri wajitambue na watambue kwamba nafasi walizoaminiwa na Rais si nafasi za kazi bali ni nafasi za kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kimaendeleo katika jamii ya Watanzania, na ili mabadiliko hayo yaonekane na kila Mtanzania ni wajibu kufanya kazi zitakazobadilisha fikra za Watanzania hasa hasa wakulima; na ili fikra za Watanzania zibadilike, ni lazima Watanzania hao washirikishwe katika mambo yanayowahusu na wakati huo huo Mawaziri wanatakiwa washiriki katika shughuli za wakulima moja kwa moja katika maeneo wanayofanya kazi, waache kabisa maofisi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, wangeamua kuanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa kwenda kwenye maeneo wakawaomba wananchi kuchimba mitaro wenyewe akiwepo Waziri au Naibu Waziri na wataalam wa ndani ya Wizara. Jambo hili lingejenga ujasiri na ufanisi wa uongozi, lingewajengea heshima Serikali, lingewasaidia wananchi ambao ni wakulima na lingepunguza matumizi makubwa ya fedha za Serikali.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iwe na takwimu mahsusi ya wakulima wa kila zao linalolimwa Tanzania, kisha wafanye tathmini ya malengo ya Serikali waliojiwekea. Je, malengo na idadi ya wakulima italingana? Baadaye wafanye marekebisho yanayohitajika.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iweke mitandao ya masoko kwa kuweka wafanyabiashara wakubwa watano hadi kumi watakaoishi nchi mbalimbali ambao watauza bidhaa za Tanzania za kilimo na hata za viwanda nje ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, soko lingine lipo ndani, Watanzania ni milioni 65, Serikali iwatumie Watanzania hawa kama soko, hivi inakuaje Zanzibar wawe wanatumia mchele wa mapembe kutoka India na nchi nyingine ambao ni rahisi na isitumie mchele kutoka Tanga. Serikali iondoe mifumo itakayosababisha mchele wa Mbeya na bidhaa nyingine na bei kubwa huko Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali izuie vijana kucheza betting na badala yake Serikali iwaandae kuwa wakulima, fedha ambazo vijana wanazitoa kuwapa Wachina ni nyingi mno na iwapo vijana hao wangezitumia fedha hizo kwenye kilimo Tanzania ingepaa angani kwa utajiri.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nikiamini kuwa kilimo ni uti wa mgongo, kwa maana ndio axis ya maendeleo ya nchi yoyote. Ahsante.