Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa kuweza kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara, nianze kukupongeza kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, ninaamini utafanya vizuri kama ulivyofanya Bunge la Kumi na Moja, lakini sambamba na hilo nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa uandaaji mzuri wa hotuba ya bajeti na uwasilishaji mzuri wa Mheshimiwa Waziri ambao bajeti yao kwa kweli imeainisha maeneo mbalimbali na ukizingatia sekta hii ya viwanda ndio muhimili mkuu wa kukuza uchumi, kupambana na umaskini na kuzalisha ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri hotuba yake imeainisha maeneo mbalimbali, lakini kubwa imeanza kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipotoa hotuba yake ndani ya Bunge ambayo ililenga kuchukua hatua mbalimbali katika kukuza uwekezaji na kufanya marekebisho kadhaa katika sera, sheria na kanuni na kuondoa vifungu ambavyo vitabainika kusababisha vikwazo katika uwekezaji, lakini pia vikwazo kwa wafanyabiashara na ninapongea Mheshimiwa Rais tumeona namna ambavyo anaendeleza mafanikio ya awamu ya tano kwenye sekta hii ya viwanda lakini tumeona pia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wizara nyingine katika kuwezesha sekta hii ya biashara na viwanda kuona kwamba inafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tumeona Mamlaka ya TRA imefungua akaunti zote walizofungiwa wafanyabiashara, kwa hiyo, tumeona namna ambavyo wawekezaji nao wameanza kurejesha imani yao na mitaji mbalimbali, lakini mchango wangu utajielekeza kwanza kwenye utekelezaji wa mpango wa kuboresha biashara wa blueprint pamoja na mafanikio ya kupunguza tozo zaidi ya 232; lakini ningemuomba Mheshimiwa Waziri kama tunataka mafanikio katika sekta yake hii ambayo itawezesha sekta nyngine ni lazima hatua ya kupunguza muda wa gharama za kupata leseni na vibali ambavyo vimeainishwa kwenye mpango huu wa blueprint utekelezeke kwa dhati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema hivyo ukifanya mapitio ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwanza hata taarifa ya Kamati niipongeze wamewasilisha vizuri nchi yetu kuwa nafasi ya 141 kwa mwaka 2020 kutoka 131 kwa mwaka 2015 ni wazi imeshuka, lakini ninatambua mpango huu wa blueprint umeanza kutekelezwa 2019 lakini ninataka niseme taasisi kwa mfano TRA, Baraza la Mazingira Tanzania, Uhamiaji na masuala ya utoaji vibali vina mchango mkubwa katika kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika ripoti hiyo imeainisha namna gani Mamlaka ya TRA imetumia zaidi ya siku 182 mpaka siku 675 kujibu maombi ya vivutio vya kodi wakati sheria ya uwekezaji ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 imetamka kifungu 16(2),(3),(4) ndani ya siku 14 TIC inapopeleka maombi ya hawa wawekezaji mbalimbali wawekezaji hao wajibiwe, lakini utaona kwenye mamlaka zetu ucheleweshaji ni mkubwa. shilingi bilioni
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia baraza la mazingira uwekezaji wote wa viwanda lazima upatikane mchakato wa uhakiki wa mazingira. Sheria ya NEMC ya mwaka 2018 imeitaka baraza hili kuchukua siku 95 kwenye mchakato huo na kutoa vibali, lakini imekuwa ikichukua siku mpaka 133 mpaka siku 200 na kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni miradi 5,600 kati ya 13,000 ambayo ilipewa vibali vya maingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini pia kaka yangu Mheshimiwa Jafo Mheshimiwa Waziri katika Wizara hii anayo nafasi kubwa kama ambavyo alivyokuwa na nafasi za mamlaka nyingine ili kuwezesha kwamba mpango huu ukamilike na kwa kweli kama watajikita kwenye mpango huu vikwazo vingine vyote ni vyepesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nije kwenye changamoto vya wafanyabiashara, wafanyabiashara pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa lakini bado wanalalamika utitiri wa kodi katika biashara mbalimbali, kwa mfano Mkoa wetu wa Pwani sisi unaongoza kwa viwanda na ninachukua fursa hii kuupongeza uongozi wa Mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika maeneo mbalimbali kwa mfano Wilaya ya Mkuranga, viwanda vinavyotengeneza gypsum kwa mfano kiwanda cha KNAUF kinalalamika tozo kubwa ya karatasi ambayo imewekwa kwa ajili ya malighafi ya kutengeneza bidhaa ya gypsum, lakini sambamba na hilo tunavyo viwanda katika eneo la Kibaha, nikupongeze Mheshimiwa Waziri umeainisha namna gani Serikali imeenda kujielekeza eneo letu la TAMCO, lakini na mchango wake wa tozo mbalimbali wa zaidi ya shilingi bilioni tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo pia zipo changamoto za masuala ya miundombinu wezeshi kwa mfano suala la nishati, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ni siku tatu zilizopita alitembelea maeneo yale na kuwatia moyo wenye viwanda na kuwaambia mipango ya Serikali namna gani itawezesha umeme wa uhakika wa maeneo haya usio katika katika, lakini tunaomba hatua hii ifanyiwe haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo sisi wana Pwani tunaomba Serikali kwamba viwanda hivi pamoja na kwamba tunaongoza kwa kuwa na viwanda vingi lakini ajira hata zile ambazo zisizohitaji wataalam vijana wengi wamekuwa wakikosa ajira, lakini pia mazingira kazini ya wafanyakazi, pia ujira wa wafanyakazi hawa. Kwa hiyo tunaomba Serikali ishughulikie hayo naipongeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kuainisha eneo la uwekezaji la Bagamoyo, lakini pia kwa kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa sukari naomba niwakaribishe Wilaya ya Rufiji na Wilaya ya Kibiti yapo maeneo ya kimkakati kwa kutumia Bonde la Mto Rufiji na uwezo wa kujenga viwanda hivyo vya sukari, lakini pia niipongeze Serikali yenyewe kwa kutumia mifuko yake ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika viwanda mbalimbali, lakini katika hili kwa kuwa Serikali imewekeza kwa mfano Serikali imewekeza katika mradi wa Mkulazi CAG ametoa maoni kadri muda wa manunuzi wa mashine unavyochelewa, kiwanda hiki cha Mkulazi kinapata hasara. Niiombe Serikali jambo hili lipo ndani ya uwezo wao wajitahidi ili nchi yetu ijitosheleze kwenye uzalishaji wa sukari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ninatambua mkakati wa uzalishaji wa vifaa tiba. Ripoti ya CAG imeainisha namna gani Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilivyotumia fedha zaidi shilingi milioni 900 kuanzisha kiwanda hiki katika Mkoa wa Simiyu, lakini mpaka leo zaidi ya siku 500 kibali cha ujenzi wa kiwanda hiki hakijatoka, lakini sambamba na hilo pia kuna Kiwanda cha Chai Mponde kule Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wanataka kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwakuwa ndio yenyewe ambayo imeona iwekeze kwenye miradi ya uwekezaji basi ijitahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimepata maombi au utumishi wa wamiliki wa hoteli, kuna hii hotel levy mpango wa blueprint ulipendekeza kupunguza kwa asilimia mbili, lakini mpaka sasa hivi haijatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaunga mkono hoja, lakini niombe mpango huu utekelezwe mpaka ngazi za Halmashauri, ahsante sana na hongereni na kazi iendelee. (Makofi)