Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia leo katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwa hotuba nzuri sana yenye malengo mazuri ya kuboresha vivutio vya uwekezaji katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimwambie Mheshimiwa Waziri mwaka 2017 aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara wakati huo Mheshimiwa Mwijage kuna kitu walikianzisha kinachoitwa blueprint. Chimbuko la blueprint lilitokana na muwakilishi wa World Bank baada ya kuwa ameongea na aliyekuwa Waziri Mwijage akamwambia bado ninyi Tanzania hamko vizuri kwenye vivutio vya uwekezaji na namna ya kuwekeza ndani ya Jamhuri ya Muungano, walibishana sana. Maana yake ni kwamba Mheshimiwa Waziri wakati ule alienda kufanya utafiti wa kina na kujua kweli Tanzania ni nini kinachofanya wawekezaji wasiweze kuja vizuri kuwekeza ndani ya nchi pamoja na wawekezaji wa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya utafiti mdogo nikaiona Tanzania katika easy of doing business in Tanzania report ya World Bank Group ya mwaka 2020 Tanzania ni ya 141 nchi ya kwanza kabisa ni New Zealand, nchi ya pili ni Singapore, nchi ya tatu ni Hong Kong kwa maana ya kwamba vivutio vizuri na namna ya uwekezaji mzuri ndani ya nchi hizo ni nchi za kwanza ambazo zinaongoza tatu bora duniani. Lakini Rwanda ni ya 38; angalia Rwanda wako 38 sisi tuko 141. Lakini ukiingia Kenya wenyewe wako wa 56 naongelea hii ripoti ambayo iko ndani ya World Bank Group, Uganda wenyewe ni 116, Zambia 85, Malawi 109 na nchi ya mwisho kabisa duniani ni Somalia ya 190.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini? Maana yake ni kwamba tafrisi yake hii ni kwamba Mheshimiwa Waziri unaweza ukawa una mipango mizuri sana, lakini blueprint ambayo iliandaliwa kama hutoifanyia kazi kwa maana kuondoa vikwazo ambavyo vinafanya uwekezaji visiwekeze vizuri, waone ni shida katika kuwekeza katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaongea sera nyingi sana, mambo mengi sana, huwezi kufanikisha. Ondoa vikwazo chukua hii blueprint lete hapa tupitishe futa kero zote zinazosumbua uwekezaji na moja katika sababu inayofanya Serikali isilete blueprint ndani ya Bunge hili wanaona kwamba TBS watawazuia mapato yao, wanaona NEMC tukitoa hii tutawapunguzia mapato yao, wanaona sijui mamlaka gani tutawapunguzia. Mamlaka iliyochini ya sheria ya kukusanya kodi ni TRA peke yake na siyo hizi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS kazi yake ni kufanya mazingira mazuri mwekezaji aendelee kuwekeza vizuri na aone nchi hii ni bora, NEMC ni mamlaka ya kumsaidia mwekezaji aone kwamba nchi hii ni nzuri, lakini hawa nao wamekuwa na regulate badala ya kurahisisha uwekezaji wao ndiyo wamekuwa wa kwanza kufanya uwekeaji uwe mgumu ndani ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha hapa nataka hili la blueprint utueleze vizuri tu utalileta lini ili tulifanyie kazi nchi yetu itoke kuwa wa 141 ipande sasa tuwazidi hata Rwanda tuwe katika top 20 na wanajua wawekezaji nje ya nchi kule wanatazama Tanzania iko rank ya ngapi, shida ni nini, wanatizama, ni kama vile ndege iko juu ya anga, anatizama sehemu bora ya kwenda kuwekeza ni wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji kuna ushindani mkubwa leo, Zambia wanataka wawekezaji, Ghana wanataka wawekezaji, Ghana ni nchi ya 116, Kenya wanataka wawekezaji, Tanzania tunataka wawekezaji, Rwanda wanataka wawekezaji, Uganda wanataka wawekezaji, wote wanavuta kila mmoja anatengeneza mazingira mazuri ya mwekezaji kwenda kuwekeza pale. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hilo namba moja nataka tu utueleze kuhusu blueprint haya yote haya kama hutorekebisha print mipango yote Mheshimiwa Waziri sidhani kama utafanikisha kwasababu vitakwaza na hii blueprint ambayo sisi tumeishauri vizuri Serikali kwenda kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya kimkakati kanda ya ziwa tuna pamba inayoajiri watu milioni 21; ukija hapa Dodoma inajulikana kwa zabibu, ukienda Singida na Dodoma pia inajulikana kwa mafuta pamoja na Kigoma. Sasa tusipokuwa na mikakati kama Mheshimiwa Nyongo alivyosema, tusipokuwa na mikakati ya makusudi kabisa kwani shida iko wapi Serikali ikiingilia chini ya Shirika letu na NDC wakatoa bilioni 50; tukafanya business plan tukaona tukiwekeza kiwanda kikubwa ndani ya Mkoa wa Shinyanga, ndani ya Mkoa wa Mwanza ambayo itakwenda kununua pamba yote ya wakulima hapa tukawekeza zaidi ya bilioni 100, 150 baada ya hapo mkatangaza kuuza kama mpango walivyokuwa wakifanya National Housing walikuwa wakichora michoro, wanaweka pale, wanatangaza, wenye fedha walikuwa wakileta fedha zao wanajengewa wanapewa nyumba. Kwa hiyo NDC wanaweza Mheshimiwa Waziri unaweza ukachukua mpango huu wa Serikali kujenga viwanda vikubwa vitano vya kimkakati ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baada ya hapo unaiuza tu kwa mwekezaji yeyote kwamba sisi tumejenga hii, faida yake hivi, tumemaliza lete bilioni 150 unauza NDC inaendelea kujenga kiwanda kingine Kigoma cha mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo tunakwenda kuwasaidia wakulima ambao wanapata matatizo ya masoko ya kilimo chao kwa mfano Kigoma hawana masoko mazuri ya mawese, ukija Shinyanga hatuna masoko mazuri ya pamba; na ni kweli kabisa pamba ni zao la kisiasa ndani ya mikoa tunayolima sisi pamba. (Makofi)

Mimi katika Jimbo la Solwa mpaka wakulima bahati nzuri mimi katika Jimbo la Solwa wakulima wengi wanalima dengu wamechukua zao mbadala la biashara katika Jimbo la Solwa wameona hii pamba hii ni shida wameachana nayo, tumewaachia Mkoa wa Simiyu wao wameendelea na pamba sisi tumeendelea, lakini kwa sababu kubwa hatuna masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija Urafiki kiwanda cha Urafiki ilikuwa ni joint venture baina ya Serikali na Serikali ya China leo mashine pale zote zimeuzwa. Mimi nilikuwa kwenye kamati ya viwanda na biashara tumeenda pale wamesema wameuza kama scrapper, mimi sidhani kama imeuzwa scrapper; zile mashine ziliuzwa kabisa kwa makusudi kukibomoa kile kiwanda na sasa hivi wanataka kufanya complex ya soko la bidhaa zilizozalishwa China kuja kuuzwa finished product ndani ya nchi yetu ni hatari na siyo nzuri kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushauri Mheshimiwa Waziri umshauri Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu fanya mazungumzo na Serikali ya Kenya; Wachina hawa ambao wako Joint Venture katika kiwanda hiki cha Urafiki waondoke watuachie sisi ili tuone namna bora ya kiwanda hiki tuwekeze kwa namna gani, tuendeleze hiki kiwanda cha pamba, tuendeleze kama kwenye mikakati yako uliyojiwekea hapa, kwamba tuwe na kiwanda ambacho kinaweza kikaunganisha magari au vifaa vya kilimo kupitia JKT na kadhalika. Hayo yatakuja baada ya kwamba China imekubali kutuachia sisi kumiliki Kiwanda cha Urafiki kwa asilimia 100; lakini ukienda pale roho inakuuma sana na mimi siamini kama zile mashine ziliuzwa kama scrapper.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiunda task force utakuta zile mashine ziliuzwa tu nchi fulani hivi wameamua kukivuruga vuruga Kiwanda cha Urafiki kwa maslahi kwamba tutengeneze ajira China sasa badala ya sisi nchi ambayo tunajikongoja kwenye uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIC wanafanya vizuri, lakini hawana maamuzi palepale yaani wanakwenda wanakupokea vizuri mno, wanafanyakazi nzuri mno, lakini unapopeleka maombi yako ya usajili wa certificate au kupata approved au msamaha wa bidhaa kwa ajili ya uwekezaji wa kiwanda mpaka tena iende tena Makao Makuu, ikubaliwe, wakae kikao kiendelee, siku zinaenda tu uone tu namna bora kwamba TIC iwe mamlaka kamili. Sasa hivi imepelekwa chini ya Waziri Mkuu, iwe mamlaka kamili kabisa pale unapo-log document zako, wawe na mamlaka ya kisheria ya kufanya maamuzi hapo hapo bila kuchelewa ili tuondoke kwenye hii rank ya 141 tuende sasa kwenye top 20 katika uwekezaji duniani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umemalizika tunaendelea na…

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga hoja mkono ahsante.