Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Itilima
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, hotuba muhimu sana kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mimi nitaendeleza tu kwa yale ambayo umezungumza kwa sababu mimi ni mkulima na mfugaji, nitazungumzia sana kuhusiana na pamba. Pamba inazalishwa katika Mikoa 17 na pamba inazalishwa katika Wilaya 56; kwa wale ambao hatuna biashara zingine kwenye Wilaya zetu tunategemea mapato kutokana na hilo zao la pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Simiyu inazalisha 60% ya pamba kwenye nchi hii na ndiyo maana Serikali Awamu ya Tano ilipokuja ikaona suala la pamba ikaja na mkakati wa kutengeneza kiwanda cha vifaa tiba pale Wilayani Bariadi. Sasa mkakati huu umekuwa wa muda mrefu takribani tangu mwaka 2016 leo ni miaka minne, Serikali tunakwama wapi? Lakini ukiangalia kwenye hoja za CAG katika mradi huo imetumika shilingi milioni 900 kwa ajili ya kumaliza upembuzi na vitu vyote kwenye mradi huo wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba tu Serikali kwenye mipango mikubwa hasa kwenye mikakati ya kimkakati kwenye zao la pamba hususan kwenye mkoa wetu wa Simiyu na mikoa mingine 17 ambayo nimeitaja. Mradi huu utakapokamilika utasaidia sana kwa wakulima wa pamba katika mikoa hiyo na wilaya hizo zinazozalisha na hii itaongeza tija kwenye uzalishaji wa pamba na itaongeza tija kwa wakulima wetu, lakini itaongeza ajira kwa vijana ambao wanamaliza shule, lakini na sisi vijana ambao tunaendelea na biashara zetu tutaendelea kuziendeleza vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri ningekuomba sana suala hili liwe kipaumbele kuhakikisha kwamba taasisi yako ya viwanda na biashara kusudi ambalo linalotarajiwa lifanyike na wananchi tuone kwamba kweli haya yanayozungumzwa na Serikali yanafanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo viwanda vya ushirika, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilisema tuwe na ushirika, ni jambo jema kuhakikisha tunamkomboa mkulima wetu ambao wanaushirika hawa wakiwa jumuiya ya pamoja wataungana na kukisemea kile ambacho wamekizalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto inayokuwepo sasa badala ya kwamba ushirika hawa waendelee kujiimarisha hatua inayofuata ushirika anakuwa sasa dalali wa kwenda kuwatumikia wenye viwanda private ambapo mimi naamini kabisa wangeanza na hatua ya kwanza tuko na viwanda. Hayati Mwalimu Nyerere alitengeneza nchi hii kimkakati, kila mkoa kulikuwa na kiwanda cha nyuzi, kulikuwa na viwanda vya pamba mfano ukiangalia kwenye mkoa wetu wa Simiyu tuna viwanda takribani viwanda sita vya ushirika lakini hakuna mkakati hata mmoja ambao Serikali inauleta sasa tunaenda kuzalisha kuweza kusimamia kiwanda kimoja cha ushirika tukiboreshe ili kusudi sasa uzalishaji wa pamba washindane na hawa washirika na private sector.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofuatia Serikali ni kuja na mawazo, wewe private sector fedha zako utapeleka pale kwenye ushirika watakununulia pamba, sasa unajaribu kujiuliza kwa njia ya harakahara.
KUHUSU UTARATIBU
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Njalu naomba ukae. Kuhusu Utaratibu.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni ya 68 naomba nisome.
MWENYEKITI: Isome.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa majadiliano Bungeni au kwenye Kamati yoyote ya Bunge, Mbunge hataruhusiwa kuzungumzia jambo lolote ambalo yeye mwenyewe ana maslahi binafsi nayo ya kifedha, isipokuwa baada ya kusema jinsi anavyohusika nalo na kutaja kiwango cha maslahi hayo na kwa sababu hiyo itakuwa ni lazima kwa Mbunge yeyote anayetaka kuzungumzia jambo hilo Bungeni au kwenye Kamati yoyote ya Bunge kusema kwanza jinsi anavyohusika na jambo hilo na kutaja kiwango cha maslahi ya kifedha aliyonayo kuhusiana na jambo hilo kabla ya kuanza kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hili, kwa sababu imekuwa ni udamaduni hapa Bungeni lakini imenibidi niseme tena sasa kwa sababu anayezungumza ni rafiki yangu, mosi; yeye ni mkulima wa pamba, pili yeye ni mfanyabiashara wa pamba, ananunua pamba kutoka kwa wakulima na tatu yeye ana ginneries za pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu kanuni zetu zinatupa huo utaratibu nilikuwa nashauri tu umpe mwongozo ili kutuwezesha tusiende hatua za mbele zaidi za kikanuni ambazo nadhani ni kali zaidi. Ili vilevile na Wabunge wengine siku nyingine wakiwa wanachangia masuala ambayo wana maslahi nayo binafsi kuanza wa-declare baada ya ku-declare sasa waendelee na mambo mengine, tunafundishana tu ili mwenendo mzuri wa Bunge uweze kwenda nashukuru. (Makofi)
MWENYEKITI: Sawa Mheshimiwa Halima ametoa Kuhusu Utaratibu kwa Mheshimiwa Njalu, lakini nafikiri Mheshimiwa Njalu anaelewa vizuri utaratibu huo na angekuwa na maslahi ya kifedha ambayo yanatakiwa kikanuni angeweza ku-declareinterest kwa vile hakusema na haku-declare ina maana hana maslahi ya kifedha. Tunaomba tuendelee. (Makofi)
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru japokuwa alitaka kunichokoza, unajua ndugu yetu naye ana changamoto zake, nimemsamehe. (Makofi/ Kicheko)
Mimi nazungumza kadri ya maslahi ya nchi yetu na ningekuwa nimetaja maslahi yangu binafsi nisingeeleza haya yote kwa sababu lazima ufahamu unapokuwa kwenye biashara ni kuzungumzia masuala yako binafsi, lakini nimezungumza mjadala wa umma, nimezungumza Mikoa 17, Wilaya 56, nimezungumza habari ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni sehemu ambayo nafaidika nisingeelezea hayo, kwa hiyo ni suala la kujifunza na kuendelea naye kuelewa kwamba tunajifunza kitu gani, lakini na mimi nimeshakuwa senior humu ni mwaka wa saba niko Bungeni humu sasa, kwa hiyo, suala ambalo lazima ujuwe una form one hapa wala siyo njuka. (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zetu za Serikali mfano; TIRDO tulitembelea sisi kama kamati tumeona ufanisi wake, lakini bado uwezo hawajajengewa kifedha. Mimi ninaamini kabisa yote tunayoyazungumza haya TIRDO tukiijengea uwezo wanauwezo mkubwa sana wa kutengeneza viwanda vidogo vidogo ambavyo vinazalisha alizeti, mpunga na kadhalika. Kwa hiyo, haya yote tukiyachukuwa tunaweza tukapiga hatua na nchi yetu ikaongeza ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kusema kwamba suala hili ni muhimu sana kwa nchi, lakini vilevile suala hili ni muhimu kwenye kodi kwa sababu unapotengeneza wafanyabiashara ndiyo unazalisha kodi unazalisha walipa kodi wengi nchini hasa sehemu sekta ya viwanda na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuomba sana Mheshimiwa Waziri, nadhani Mheshimiwa Waziri ulitembelea kule Katavi uliona kwamba watu wanavyowekeza kwenye viwanda kwenye mikoa hii mipya, kwa hiyo, ni imani ya kwamba shughuli zikienda sambamba itatusaidia sana na wewe Mheshimiwa Waziri na Serikali sehemu kubwa ninyi ni kuhakikisha wafanyabiashara mnawawezesha kwa miundombinu, mnawezesha kila jambo ili kusudi nchi yetu iendelee kufanya mapato ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge lililopita nilishawahi kusema kwamba Waziri wa Viwanda na Biashara, Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara hawa ni sehemu kubwa sana ya kuiwezesha Serikali kukusanya mapato yake makubwa sana bila hata bugudha yoyote ile, lakini kulingana tu na sera sijui mipango au kwa sababu ni kutimiza wajibu, kila mtu akiamka anaamka na analolifahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko changamoto nyingine moja kwenye suala la nchi zetu hizi wanazofanya biashara kwa kuingiliana mfano Zambia na Tanzania kuna sheria imepitishwa Zambia asilimia 50 wanataka wao mzigo wabebe Wazambia kupita malori yao, lakini asilimia 20 ibebwe na Watanzania, asilimia 30 iende kwenye train. Sasa jambo hili siyo afya sana. Sasa kwenye mjadala huo hatujui umeanzaje mpaka Waziri wa Zambia akafika mahala hakatoa huo waraka wake kwenye nchi zetu za Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeshauri na lenyewe Mheshimiwa Waziri ulichukuwe mjaribu kulifanyia kazi ili kusudi biashara hizi zifanyike vizuri zaidi na watu waendelee kupata mapato kwenye nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)