Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara kwa kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitazungumzia maeneo matatu, nitazungumzia katika Mamlaka ya Viwango (TBS), lakini vilevile, nitanzungumzia Liganga na Mchuchuma na nitamaliza kwa kuzungumzia malighafi ya parachichi katika kuchochea uwazishwaji wa viwanda vya kuchakata zao hili muhimu la parachichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Viwango (TBS) ninavyojua mimi kazi yake ni kuangalia afya za wananchi wa Tanzania kuwa salama kutokana na bidhaa zinazoingizwa ndani ya nchi. Hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko ya bidhaa zinazoingia ndani ya nchi kama magari yale ambayo used yanayoingia ndani ya nchi yakabadilishiwa mfumo wa ukaguzi kutoka kwenye ile system ya zamani ya pre-arrival inspection kuja kwenye destination inspection.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani TBS waliingia mikataba na makampuni ya Japan pamoja na Dubai katika ukaguzi wa magari haya na kazi ilikuwa inafanyika vizuri sana, lakini vilevile TBS haikuingia gharama yoyote katika ukaguzi huu wa magari zaidi ya kupokea percent ambayo waliokuwa wanapewa na makampuni yale na katika ukaguzi wa magari haya magari yalikuwa yanakaguliwa katika dola 150 mpaka 300 kwa gari moja inategemea na ukubwa wa gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ndani ya miaka 10 TBS iliweza kupata USD milioni 10 kama percent waliokuwa wanapewa na yale makampuni. Mimi najiuliza kwa kuwa kazi ya TBS ni kuangalia na kulinda afya za Watanzania kutokana na hizi bidhaa zinaingia ndani ya nchi. Leo imeamua kubadilisha mfumo wa ukaguzi wa magari haya yawe yanakaguliwa hapa nchini, mashaka ambayo niliyonayo, kazi ile ni ngumu na ni nzito. Lakini vievile inatakiwa tujiandae vizuri kuhakikisha kwamba tunaweza kuthibiti uingizwaji wa magari mabovu ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Nina wasiwasi na miundombinu ambayo inatumika kukagua magari haya, mfano kule Japan katika kampuni hizo tano walikuwa na uwezo wa kukagua magari 2,000 ndani ya mwezi mmoja, lakini nimefuatilia hapa Tanzania gari moja inakaguliwa ndani ya masaa mawili na kuna meli ambazo zinabeba magari zaidi ya 2,000, mashaka yangu hakutakuwa na mrundikano wa magari pale bandarini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile unapoileta gari hapa, mteja ameshanunua gari ameshaileta hapa Tanzania, inakaguliwa na TBS itakaposema hii gari ni mbovu hii gari itakwenda wapi? nina wasiwasi nchi yetu isijekwenda kuwa dumping country. Lakini vilevile huyu Mtanzania ambaye amejikwamua mwenyewe ameona gari mtandano kuna hawa watu wanaitwa Wapalestina wanauza magari mpaka dola 500 mpaka dola 1,000 bila kujali iko kwenye ubora gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtantanzia wa watu amejikwamua amenunua gari ameileta imefika bandarini hapa anaambiwa aikarabati ili iweze kukidhi viwango zaidi ya ile pesa aliyoinunulia, hatuoni kwamba tunakwenda kuwanyanyasa wananchi wetu wanyonge ambao yeye amependa kujikwamua aweze kuwa na usafiri wake wa kumpeleka kazini na kwenye shughuli zake. Leo anaambiwa kwamba hii gari haina ubora unabidi ugharamie kuikarabati na ataingia gharama kubwa. Wakati zamani zile kampuni zinazouza magari kwa mfano kama hawa wanaojiita Beforward ukinunua gari kwa Beforward yeye kule anaponunua kwenye mnada anaiangalia kabla hajaileta Tanzania ataipeleka kwenye zile kampuni za kuangalia ubora wa gari; akiipelekea kwenye ile kampuni akiona kama kuna changamoto zozote za kurekebisha ile gari Beforward ilikuwa inafanya yenyewe kwa niaba ya mnunuzi aliyenunua.
Sasa leo kubadilisha mfumo ule ina maana sasa tunamuongezea gharama mnunuzi ambaye ni mwananchi mnyonge Mtanzania. Mimi nilikuwa naomba suala hili mliangalie kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile Serikali imekwenda kuwekeza bilioni 20 kwa ajili ya kutengeneza miundombinu hii ya ukaguzi wa magari, wakati bilioni 20 hii si mngetuletea sisi Njombe, Mbeya kule, Rukwa maeneo tunayolima parachichi tukaweza kufungua viwanda vya kuchakata zao la parachichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Liganga na Mchuchuma; naiomba sana Serikali sana iongeze kasi ya majadiliano yanayoendelea ili mradi huu uanze mara moja. Sisi wananchi wa Mkoa wa Njombe na wananchi wa Nyanda za Juu Kusini na Kusini kwa ujumla pamoja na Watanzania wote mradi huu utakwenda kuwa ni kichocheo kikubwa sana kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini vilevile Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekuwa tukizungumza miaka mingi sana ndani ya Mbunge tangu mwaka 2010 tunazungumzia Liganga na Mchuchuma. Nilifikiri kipindi kile tumeanza kutengeneza standard gauge mradi huu ungekuwa tayari umeshaanza kufanya kazi ili raw materials za chuma ziweze kutumika katika vile vifaa ambavyo vinatengeneza reli, lakini vilevile tuna miradi mingi inayoendelea madaraja hii malighafi ya chuma ingeweza kutumika katika kutengeneza standard gauge pamoja na reli zingine ambazo zinaendelea na ambazo zinatakiwa kutengenezwa na madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukizungumizia makaa ya mawe juzi hapa nilimuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wana mkakati gani kuhakikisha kwamba NDC kuachia baadhi ya vitalu ili wananchi waweze kuchimba makaa hayo kwa sababu kuna uhitaji mkubwa sana wa makaa haya ya mawe. Na Serikali ilikubali kwamba wananchi sasa waanze mchakato wa kuomba ili waweze kupewa vitalu hivyo. Sikupata nafasi ya kushukuru, nashukuru kwa majibu hayo na wananchi wa Ludewa pamoja na Njombe na wadau wengine wa maeneo mbalimbali ambao wanajishughulisha na biashara hizi za wachimbaji wadogo wadogo wapo tayari na wataanza kuleta maombi hayo ili muweze kuyafanyia utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitojisikia vizuri kama nitamaliza kuchangia bila kugusa malighafi ya zao la parachichi. Kama tunavyojua malighafi ya parachichi inalimwa mikoa mingi takribani mikoa 12, jirani yangu hapa anatoka Jimbo la Hai naye ameniambia Hai wanalima sana zao la parachichi. Hebu hii Wizara sasa iangalie ni namna gani inakwenda kuwakomboa vijana katika suala zima la ajira katika kuhakikisha kwamba wanaleta wawekezaji wengi ndani ya nchi ili waweze kuanzisha viwanda hivi vya kuchakata parachichi kama ni takribani mikoa 12 ina maana tuna uwezo wa kuanzisha viwanda vingi sana vya kuchakata zao hili la parachichi na hii itakwenda mkombozi kwa Taifa letu kwa sababu vijana wetu watakwenda kupata ajira, lakini vilevile tutawasaidia wakulima hawa wa zao la parachichi kuweza kuboresha malighafi hii iwe na thamani zaidi baada ya ku-export parachichi kama parachichi, sasa tuanza ku- export mchuzi wa parachichi, lakini vilevile majani, mbegu zile zote zifanye kazi na wananchi wetu waweze kupata mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda nakuomba sana ukae na Waziri wa Kilimo muone namna bora ya kuweza kulipeleka mbele zao hili la parachichi. Ulimwenguni wanajua zao hili la parachichi inaitwa green gold, kwa hiyo, ni wakati sasa kuhakikisha kwamba mnaweka kipaumbele na mnaweka mkakati mahususi na mnaweka jitihada kubwa katika kuhakikisha kwamba mnapeleka zao hili mbele hili kuweza kumkwamua mkulima mmoja mmoja na vilevile kuweza kuchochea uchumi na kuongeza mapato ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndio njia za kuweza kuongeza mapato,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Neema.
MHE. NEEMA W. MGAYA: …siyo kwenda kuongeza mapato kwa TBS. TBS haina kazi ya kuongeza mapato, kazi yake ni kuangalia afya ya Mtanzania, kuzuia bidhaa ambazo zitakwenda kuathiri afya ya Mtanzania sio kazi ya TBS kuongeza mapato. Ahsante sana. (Makofi)