Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ambayo kimsingi inagusa jamii kubwa ya Watanzania.
Kwanza kabisa kabla ya kwenda mbele ni lazima tuangalie huku nyuma tulifanya vizuri kiasi gani au vibaya kiasi gani ili tuweze kujisahihisha. Nikisema hivyo ninakwenda moja kwa moja kwenye mpango wa utekelezaji wa bajeti wa miaka ya fedha ya mwaka 2016/2017 ambayo bajeti ya Wizara hii ilikuwa ni asilimia 44; mwaka 2017/2018 ilikuwa ni asilimia 9.51 mwaka 2018/2019 ilikuwa ni asilimia 6.5; ukijumlisha kwa wastani wake miaka hii minne mfululizo unakuja kupata asilimia 20 tu ya bajeti katika sekta muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwendaje mbele katika kauli hii ya nchi ya viwanda huku tukiweka asilimia 20 miaka minne mfululizo. Hatuwezi kwenda kwa sababu mwisho wa siku mipango hii ni lazima itekelezwe, pesa ni lazima ziwepo ili maendeleo yawepo. Kwa tathmini hii ya mpango target yetu ni nini? Mpango wa Pili tulikwama wapi leo tunakwendaje mbele? N lazima tu-refer tulikotoka ili tuangalie tulikwama wapi twenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema haya kwa sababu hapo nyuma wakati wa kauli mbiu ya nchi yetu ya viwanda ilivyopamba moto, kuna Waziri alisimama kwenye matamko yake akasema tutakwenda kujenga viwanda 100 kila mkoa; alikuwa ni Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Jafo, akasema tutakwenda kujenga viwanda, hizi kauli hizi zisiwe mapambio zikawaponza Watanzania wakatuona huku tunapiga mapambio tu, haiwezekani. Hizi kauli ziende na vitendo, na alivyosema hivi nilikumbuka Kiwanda cha Tanganyika Packers nikasema kiwanda hiki kikifufuliwa wananchi wa Jimbo la Kawe na Dar es Salaam wanakwenda kupata ajira nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikasema kiwanda hiki kimebeba jina la Kawe maana ya Kawe ni njia ya kupita ngo’mbe (cow way) ni Kawe nikasema kiwanda hiki kikifufuliwa tutakwenda kupata ajira nyingi kwa sababu viwanda vingi vimekufa. Siweze kurejea haya kwa sababu viongozi na Wabunge wengi wameongea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje kufikia malengo wakati sekta ya kilimo tumeiacha nyuma, hawa ni mapacha ni lazima tuangalie kilimo tunatengaje bajeti yake inatekelezwa vipi hili twende mbele kwa sababu kama hatuna raw material hatuwezi kwenda na viwanda. Na ukiangalia kwa miaka mitano mfulululizo sekta ya kilimo wametengewa asilimia 17 tu; tunakwendaje kwa namna hiyo? Hatuwezi kwenda kwa sababu hawa ni mapacha bila raw materials viwanda haviwezi kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hayo najielekeza kwenye nafasi yetu ya kidunia ambayo wengi wameiongelea ya 141 kati ya nchi 190; tunakwenda hivyo tulikuwa tumejiwekea malengo kama Tanzania twende kwenye double digit position, hatuwezi kwenda kama malengo yetu hatuwezi kuyatekeleza vizuri wakati tunapanga. Nikisema hayo ninaangalia mazingra ya biashara na viwanda kwa Tanzania ni rafiki? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwama kwa sababu mazingira si rafiki, Tanzania kuna utitiri mkubwa wa kodi, ukileta uwekezaji anaaanza kujiuliza wazawa wameshindwa kuwekeza kwa sababu ya utitiri wa kodi. Nikianza kutaja hatutamaliza, ukitaka kufungua kiwanda au kuanzisha biashara ni lazima uende ukasajili BRELA kule ni pesa, ni lazima ulipe kodi ya zuio, hiyo ni pesa; ni lazima ulipe kadiri unavyopata hiyo ni pesa; ni lazima ulipe gharama za OSHA hiyo ni pesa; ni lazima ulipe kodi ya ujuzi hiyo ni pesa; bado Manispaa wanakusubiri ulipe leseni hiyo ni pesa; gharama za Zimamoto, ada za Mamlaka ya Chakula; hiyo ni pesa na gharama lukuki ambazo ziko hapa. Mlundikano huu wa kodi, mwananchi wa kawaida mwenye mtaji wa kawaida hawezi kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda namna hiyo Mheshimiwa Waziri nikuombe wakati unakuja na mkakati wako, una-wind up hapa, utueleze ni mkakati gani ulionao ili kuwezesha Watanzania waweze kuwekeza. Tusiimbe tu nchi ya viwanda kwa mdomo, tukatekeleze kwa vitendo kwa sababu…
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji anayezungumza anasema kwamba Serikali haijajenga viwanda kwa maana kauli ilipamba tu moto, lakini viwanda vingi havijaanzishwa. Nataka nimpe taarifa kwamba kutokana na Tanzania National Business Portal, ripoti inayozungumzia kwamba toka Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, viwanda 4,877 vimejengwa. Kati ya viwanda hivyo, viwanda 201 ni viwanda vikubwa, viwanda 460 ni viwanda vidogo, viwanda 3,406 na viwanda 4,401 ni viwanda vidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimpe taarifa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba mazingira ya viwanda yanakuepo na viwanda vingi vimeshajengwa nchini. Ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Felista unaipokea taarifa hiyo?
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo kwa sababu sizungumzii viwanda vinavyofichwa chumbani, nazungumzia viwanda vyenye tija kwa wananchi, nazungumzia viwanda ambavyo vilikuwepo na hatujaviona. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Felista, viwanda vipi vinafichwa chumbani? Naomba uondoe hilo neno.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema huwezi kuwa na blender useme una kiwanda; huwezi kuwa na cherehani moja unaajiri watu wangapi?
MWENYEKITI: Basi tumia lugha nyingine, lakini siyo ya chumbani.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, blender hata ndani si unajua. Kwa hiyo…
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
T A A R I F A
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Naomba nimpe Mheshimiwa dada yangu taarifa kwamba hivi tunavyozungumza bajeti iliyoko mezani kwake hapo zimeshatengwa shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kufufua kiwanda kikubwa sana cha Kilimanjaro Machine Tools, kiwanda ambacho kilikufa miaka mingi, sasa kimeshatengewa hela. Kiwanda hiki kinatengeneza viwanda vingine vidogo vidogo, kazi yake ni kuunda vyuma na fedha imeshatengenezwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kumpa taarifa kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inaendeleza kujenga viwanda vikubwa vikubwa kama hiki ambavyo havipatikani kwingine duniani. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Felista.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kaka yangu Mheshimiwa Mafuwe, alikuwa anataka kuchangia kwa sababu hayuko kwenye list. Mimi niendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba maneno haya siyasemi mimi; kupitia Ripoti ya CAG anasema kwamba kumekuwa na utekelezaji mdogo wa bajeti ya maendeleo kwa viwanda vidogo vidogo katika ngazi zote za Serikali; mfano, kwa miaka minne ya nyuma mfululizo, Wizara ya Viwanda na Biashara imetumia asilimia 16 tu ya fedha za maendeleo zilizopelekwa kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vidogo vidogo. Maneno haya si ya kwangu, ni maneno ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hivyo ninasema tujielekeze kwenye ukweli, tunavyopanga hapa tuweke bajeti na ile bajeti iende na ikatekelezwe. Sisemi mapambio ya kuweza kumfurahisha mtu. Watanzania huko nje wanalia, akina mama huko nje wanalia kwa sababu hata akiwa na biashara yake ule utitiri wa kodi kwa miaka mitano iliyopita hii Watanzania wengi biashara zao zimefungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi mtakuwa ni mashahidi, hamuwezi kusema lakini mnajua kwenye majimbo yenu kilio cha Watanzania ni kikubwa kuliko tunavyofikiri. Twende tukarekebishe kwa sababu kazi ya Bunge ni kuielekeza Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kuielekeza Serikali ikaangalie utitiri huu wa kodi, ipunguze ili wananchi wetu wapate nafuu na waweze kuwekeza. Nia yetu ni njema kwa sababu Tanzania yetu ni moja, tunahitaji maendeleo, hatuhitaji malumbano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa hatuhitaji ahadi, tunahitaji utekelezaji. Utekelezaji ni jambo la msingi kwa sababu baada ya kutoka hapa tutakuwa na dhambi ya kujibu kwa Mwenyezi Mungu. Wale watu wenye imani kila siku unamwambia mtoto wako utanyonya kesho kama mtoto wa kuku halafu mwisho wa siku Watanzania wanakosa imani na Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tukatekeleze vile tulivyovipangilia ili tuweze kufikia azma ya Serikali ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, ninakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)