Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kwa kunipatia fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia leo hii tupo wazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita zaidi, mara nyingi sana Wabunge wote waliosimama hapa wanazungumzia suala la vijana na mimi kama rika ya vijana bado ninayo haki ya kuzungumzia suala la vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii, imebeba taswira kubwa na dhana kubwa sana ya kumkomboa kijana wa Kitanzania sasa hivi. Ukweli usiopingika idadi kubwa sana ya vijana wa Tanzania ndiyo ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali, lakini ndiyo wanaochangia pato kubwa sana la Taifa hili la Tanzania. Ripoti ya dunia kwenye Benki Kuu inaonyesha kwamba Tanzania kila mwaka vijana milioni moja wanaingia kwenye suala la ajira, lakini vijana 200,000 tu ndiyo wanufaikaji wa ajira, lakini vijana 800,000 ndiyo ambao hawapati ajira mpaka muda huu tuliouzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukizungumza kama miaka mitano ijayo bado tunatengeneza wimbi kubwa sana la vijana ambao watakuwa hawana ajira. Sasa wazo langu, kwenye Wizara hii, lazima tuweke mipango mikakati namna gani tunaweza tukawasidia vijana kwenye Wizara hii. Isiwe Wizara hii kazi yake kubwa sana, kazi yake kufanya mipango mikakati kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, lakini hatuangili vijana namna gani tunaweza tukawasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mipango mahsusi ya kuweza kuwasaidia vijana, tunao vijana wa vyuo vikuu wanamaliza vyuo vikuu, lakini mwisho wa siku wanabakia hawana ajira, ni vijana tu wachache ambao wananufaika na ajira, lakini vijana wengi hawanufaiki na ajira. Kama Wizara imejipanga vipi na namna gani kuwasaidia vijana hawa ambao wanahitimu vyuo vikuu? Kwa nini tusitengeneze exemption at least miaka kama mitatu, minne tukawapa mikopo ya fedha ilimradi wakaanzisha makampuni wao wenyewe binafsi kama vijana ambao wamehitimu vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wapo wanafunzi ambao wamemaliza kada ya sheria, wanaweza wakaendesha kampuni zao za kisheria tukawa tuna mawakala wa-law wakawa wanatetea wananchi, leo hii Tanzania tunaweza tukajikuta hata mtu wa kawaida mkulima anawakili wake wa kuweza kumtetea kwenye mahakama. Leo hii tunaweza tukawa na mvuvi, lakini pia akawa na wakili wake wa kuweza kumtetea kwenyea mahakama endapo kutatokea matatizo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado hatujaona fursa ya kuweza kuwasaidia vijana wanaohitimu chuo kikuu, lakini wapo wanafunzi ambao wanamaliza kwenye kada ya IT ndiyo hawa hawa mwisho wa siku wanaweza wakaanzisha makampuni makubwa ya kufungua masuala ya website, ya kufungua masuala ya computer technician na mambo mengine kadhaa wa kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kufungua kwa kampuni hizi nazo zitawasaidia wao wenyewe vijana kupata ajira, lakini pia wapo ambao tayari hawakufikia level za vyuo vikuu nao watapata kufanya angalau ajira, japo kufanya usafi kwenye maofisi na kazi nyingine ndogo ndogo. Lakini bado hatujaenda kuwaangalia kuwasaidia vijana, Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye ukurasa wa nane hii ambayo tayari tunaizungumzia ya mwaka 2020/2025 imezungumzia kwamba namna gani Serikali inaweza ikatengeneza ajira kwa vijana milioni nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado hatujaangalia mkakati wa kuwasaidia vijana, bado kwenye Wizara hii hatujakaa kabisa. Tusiwe na dhana ya kuweza kuvutia wawekezaji, lakini pia tuwe na dhana ya kuwasaidia vijana wetu ndani ya Tanzania. Najua bado hatujawa na fedha na capital na wala hatujawa na wimbi kubwa sana la wawekezaji kuja ndani ya nchi. Lakini namna gani tunawasaidia vijana, kwa mfano wapo vijana ambao wamemaliza masuala ya business administration ndiyo hawa hawa wanaweza wakaandika ripoti tofauti tofauti kwa ajili ya investment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anaweza akaja mwekezaji, lakini akatafuta ripoti tunao vijana ambao tumeshawapa exemption ya kodi na tulishawapa fedha kwa ajili ya kujikwamu, lakini vipi wanaweza kutengeneza ripoti tofauti tofauti wakaja wazungu, wakaja ma-investor wakachukua ripoti baadaye zikawa applicable. Bado hatujawa tukafikiria lazima Wizara ya Viwanda na Biashara ifikirie namna gani sasa ya kutengeneza fedha kwa ajili ya kuwasaidia vijana kwa ajili ya kujikwamua na huu unyonge na umaskini ili uweze kuisaidia familia zao la sivyo hatuwezi kuwasaidia vijana kwa namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutabaki tuna propaganda za kisiasa tuna wasaidia vijana tunatengeneza, tunaandaa ajira kila mwaka, tutaandaa manifesto, tutaandaa Ilani, tutaandaa ripoti tofauti tofauti namna gani ya kuwasaidia vijana, lakini bado hatujawa practical kwa ajili ya kuwasaidia vijana, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nakuomba sana wafikirie vijana bado vijana wanateseka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo usishangae kumuona kijana ambaye amehitimu chuo kikuu anaendesha boda boda, usishangae kumuona kijana wa chuo kikuu yupo kwenye michezo ya ku-bet, usishangae leo kumuona kijana yupo kondakta ni muhitimu wa chuo kikuu. Serikali imetumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kumsaidia kijana ili aweze kufika chuo kikuu, lakini mwisho wa siku akimaliza miaka yake mitano au miaka mitatu ya kuhitimu degree anabakia mitaani anaendesha bodaboda. Unadhani kijana kama huyu mwisho wa siku tumemsaidia nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukae kama wizara kuweza kuwasaidia, ingawa tunasisitiza siku zote sisi hapa Bungeni kwamba Serikali itenge fedha kwenye Halmashauri asilimia kumi kwa ajili ya kuwasaidia vijana, sawa inafanya hivyo, lakini kwa nini tusitenge angalau asilimia kadhaa ambayo inatoka kwenye Wizara hii kuwasaidia vijana kuanzisha makampuni au kuanzisha shughuli yoyote ya kibiashara? Bado hatujakaa tukafirikia Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Juma.
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)