Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chwaka
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kupata fursa nikawa miongoni mwa wachangiaji wa Wizara hii ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuniwezesha kufika hapa nikiwa katika hali ya uzima na pili niweze kuishukuru Serikali kwa kuweza kufanya kazi zake vizuri na baadaye kuweza kupata tija. Wizara hii inakazi kubwa ambayo inaifanya nchi hii iweze kutimiza yale malengo yake, ambayo yamejiwekea kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya nchi. Niseme kwamba nchi hii kwanza niwape shukurani kwa kuwezesha kuyatimiza yale ambayo wameahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja hapa Waziri wa Nishati alizungumzia kuhusu vinasaba kusema suala hili analihamisha kwa mwekezaji mmoja tu na baadaye kulipeleka kwa Serikali kwamba hili suala limeweza kutimia. Lakini pia kusema kwamba yale ambayo tulikuwa tunafanya uchunguzi wa magari (inspection) ambayo tulikuwa tunafanya nje leo tunaifanya hapa.
Mimi kwangu niseme hilo ni jambo jema kwa sababu Watanzania wengi wataweza kupata ajira. Ushauri wangu tu hapa niseme kwamba Wizara iweze kusimamia Watanzania wale wasije wakapata hasara kwa sababu ya kuweza kuleta kufanya uchunguzi katika nchi yao. Iwe ni tija lakini pia waweze kusomeshwa, kutolewe elimu watu waweze kupata elimu na wajue nini kinaweza kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niondoke hapo nije kwenye mfumo wa ukusanyaji kodi kwa njia ya electronic - ETS ambayo mwenzangu ameshaizungumza kwa hiyo, sitakaa sana kulizungumzia suala hili. Lakini tu niseme kwamba Wizara iweze kukaa na kujadili upya kuliangalia suala hili kwa kina kwa sababu wenye Viwanda ni suala ambalo wanalilalamikia na kama kitu kinalalamikiwa ni vizuri kikaangaiiwa tija inapatikana vipi? Hasa kwa sababu fedha zake ni za kigeni lakini pia fedha zile hazizunguki ndani ya Tanzania. Kwa hiyo, ningeomba Wizara wakaweza kuliangalia suala hili kwa umakini mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende tu pale ambapo hasa nimekusudia kusema maneno yangu leo hii. Niseme kwamba twende kuboresha huduma kwa sababu naamini huduma ni njia moja ya kuweza kufanikisha yale malengo yetu ambayo tumejiwekea. Huduma itakapokuwa haifikii pale ambapo tunapataka kwa hivyo, hii mipango yetu tunaweza tusifikie katika malengo ambayo tumejiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema kwamba tuweze kwenda kuboresha huduma; kwa sababu Wizara hii ya Viwanda na Biashara ndio ambayo inaweza kuangalia namna nzuri ya kuweza kuendeleza viwanda, lakini wakishaangalia namna hiyo nzuri ya kuweza kuendeleza viwanda wanaoshughulikia ni wengi. Kwa hiyo, ningemshauri Mheshimiwa Waziri kwamba wakae wadau wote ambao wataweza kuifanya biashara iende vizuri. Kwa mfano, hapo nyuma nilikuwa nikikaa kwenye tv namuona tu pengine Waziri kutoka Mazingira anaenda kufunga kiwanda, hii hapa tutakuwa hatuna huduma bora, ni vizuri tukafanya pale tukakaa pamoja na Wizara zote zinazohusika katika kuendeleza masuala ya kibiashara, ili tuweze kufika katika yale malengo ambayo tumekusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwa mfano TRA katika safari zetu ambazo tumepita, mimi ni mmoja ya Wajumbe kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara. Katika safari zetu tulikopita, kila mahali ukikutana na wafanyabiashara, ukikutana na wenye viwanda wanailalamikia TRA. Mwenzangu amesema hawa TRA ni nani, lakini katika sehemu moja tu ndipo ambapo tumefika pale watu wakaizungumza vizuri TRA. Lakini ukija ukimuangalia yule ambaye amezungumza vizuri TRA, amezungumza kwamba ameanza kwa Katibu Mkuu, akaja kwa Kamishna baadaye watendaji wakapewa maelekezo mahsusi, lakini wenyewe hawawezi kufanya kazi ile kuonesha namna ya huduma bora. Na tukikosa huduma bora hatuwezi kufanya biashara ile ambayo tumeilenga katika Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo. Kwa hiyo, niseme twende kuboresha huduma ili huduma yetu iwe bora zaidi, sasa hivi iko bora lakini iwe bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la VAT; nalo limekuwa ni kikwazo kwa wafanyabiashara na wenye viwanda kwa sababu tunawacheleweshea kurejesha fedha zao ambazo fedha hizi ziko kisheria. Lakini kuchelewa kurejesha fedha zao maana yake unaenda kuwakwamisha na unapowakwamisha wafanyabiashara, unapowakwamisha wenye viwanda maana yake unawakwamisha Watanzania. Kwa hiyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaliangalia vizuri…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekit, naomba dakika moja kuweza kuhitimisha suala langu.
MWENYEKITI: Malizia tu sentensi yako.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante niondoke hapo, niseme tu ushauri wangu…
MWENYEKITI: Usiondoke, yaani wewe malizia sentensi yako.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Ushauri wangu kwenye hili, ushauri wangu wale wenye viwanda pamoja na Serikali kufanya kiurafiki zaidi kwa sababu inaonekana kwamba mfanyabiashara anavutia kwake, Serikali inavutia kwake, maana yake hapa hatuwezi tukaenda tukatengeneza nchi ya viwanda. Ili tutengeneze nchi ya viwanda wafanyabiashara waone kama kulipa kodi ni haki yao ya kimsingi, lakini Serikali kukaa na wafanyabiashara na wakaona kwamba wafanyabiashara tunafikisha pale malengo ambayo Serikali inaitaka hili ni jambo zuri. Kwa hivyo, ningeliomba Serikali yangu ikaifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)