Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia maandiko nichangie bajeti ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nibainishe kwanza muhimu ya kuzingatia kwanza tunao mpango wa muda mrefu wa kufufua viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi vizuri au vimekufa kabisa. Naomba na kushauri Serikali ifanye tathimini ni kiwanda gani kinaweza kufufuka na kuzalisha kwa tija kubwa. Viwanda ambavyo haviwezi kufufuka tuachane navyo au maeneo hayo kama yana miundombinu wezeshi na saidizi basi maeneo hayo yatumike kwa viwanda vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijikite katika kujenga uchumi shindani kwa kutanguliza lengo kuu ikiwa ni kutengeneza ajira, ikifuatiwa na kuzalisha bidhaa na mwisho kwa umuhimu huo kukusanya mapato. Ni katika mfuatano na umuhimu huo ujenzi wa uchumi wa viwanda shindani utaweza kufikiwa. Kwa maana rahisi shughuli yoyote inayoweza kutengeneza ajira, maslahi ya kukusanya kodi yasitukwamishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujenga viwanda tubainishe ni viwanda gani tusijihusishe navyo hasa pale penye uwekezaji wa umma ili kuepuka kupoteza rasilimali adimu za wananchi. Pia ni muhimu Serikali kuchangamsha re-export business na biashara hapa nchini ili kutengeneza ajira na kukusanya mapato lakini muhimu kulinda viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ifanye utafiti ili kujua ni kwa namna gani korosho na pamba izalishwayo nchini inaweze kuongezwa thamani hapa nchini na bidhaa zake kuwa shindani hapa nchini au na kuingia kwenye masoko ya nje na kufanya vizuri. Hoja hapa ni kuzalisha kwa tija na kuingia kwenye masoko mazuri ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ichukue jitihada zaidi kuelimisha wananchi na hasa Wabunge juu ya dhima ya mipango mitatu ya miaka mitano mitano. Hii italeta uelewa wa pamoja hali itakayoongeza kasi ya kutekeleza dira ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.