Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Mussa Azzan Zungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ilala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Kamati yetu hii, na kunipa nafasi ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, mimi nipo kwenye Kamati hii toka mwaka 2005 nilikuwa Makamu Mwenyekiti wakati wa Mama Anna Abdallah, Makamu Mwenyekiti kipindi cha Masilingi, Makamu Mwenyekiti kipindi cha Lowassa na Mungu amenijalia sasa kwa rehema zake na mapenzi yake nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni pesa za maendeleo ambazo zinatakiwa zije kwenye Wizara hii haziji. Tunatatizo kubwa sana za kutumia pesa kulipa pango katika mabalozi nje ya nchi, takribani kwa miaka kumi Serikali inatumia siyo chini ya shilingi bilioni 220 kulipa pango tu, pesa hizi zingeweza kuwa re-invested na tukawa tuna majengo yetu na ikawa ni heshima kwa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiwa na majengo yetu tuna nafasi ya kupata kodi na tuna nafasi ya kutokulipa kodi kwa nchi zingine, sijui kwa nini hii hoja Serikali wanaiona ni nzito kwao. Mwaka 2021 na tumeitoa kwenye taarifa pesa za maendeleo shilingi bilioni 20 hata senti tano mpaka leo haijatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeahidiwa kwenye kikao cha pamoja kwa mujibu wa kanuni zetu, Kamati ya Uongozi na Kamati ya Bajeti kwamba fedha zitalipwa by May na sina taarifa mpaka sasa hivi kama hizo fedha zimelipwa. Ni jambo ambalo linaturudisha nyuma. Kuishi katika nyumba za kupanga Balozi wa Tanzania ni kutoku-secure information za nchi huko tuliko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, usalama wa taarifa za Balozi na makao makuu ya nchi unakuwa na mashaka makubwa. Tulipangiwa mwaka 2019/2020 bilioni nne; fedha zilizotoka ni takribani milioni 300 tu. Sasa bila kuwa na fedha zetu au bila kuwa na majengo yetu hatuwezi kuwa na diplomasia nzuri ya uchumi. (Makofi)

Hoja yangu kubwa na Waziri wa Fedha yuko hapa, niombe waweke uzito mkubwa sana wa namna gani kuisaidia Wizara hii iweze kupata fedha za maendeleo. Tumeweza kununua nyumba New York naipongeza Serikali, nyumba ile sasa nayo tunakaa wenyewe bila kulipa kodi, lakini vilevile sasa tunatoza watu kodi kwa kuwapangisha katika eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna kiwanja Uingereza primed area, huu zaidi ya mwaka wa 15 mpaka kiwanja kile sasa kinaota magugu. Kuna gharama kubwa ya kutoa ile mizizi na inakuwa ni aibu na mpaka sasa mwisho, majirani kwenye kiwanja kile wanalalamikia kwenye Serikali yao, kiwanja kile tunyang’anywe na kiwe mali ya Serikali ya Uingereza na sisi tukose. Yote hatupeleki fedha za kujenga majengo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mengi tunayasema kwenye ripoti yetu sitaki kuingia kwenye mambo mengi sana niwaachie wajumbe wengine, lakini mimi nilitaka kujenga hoja kwenye nyumba tu, tuweze kununua nyumba zetu, tumiliki nyumba zetu na tuzikarabati ziwe mali ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashindwa sasa hivi mpaka na mataifa mengine madogo namna wanavyokuwa na majengo. Kuna nchi hapa Afrika Mashariki ukienda pale Mtaa wa UN, unaona jina lake inapendeza kuona pale House of Uganda. Kwa hiyo, mimi niombe sana Serikali, Waziri wa Fedha uko hapa, Chief Whip yuko hapa, tunaomba Wizara hii muipe fedha iweze kukarabati na muwape fedha ili tuweze kununua tumiliki nyumba katika nchi za mabalozi yetu nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)