Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu kwa ustawi wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha hoja yake kwa umahiri mkubwa. Sambamba na hilo niwapongeze wasaidizi wote ambao wameifanya hii kazi na ikawa nzuri. (Makofi)
Sasa mimi nataka kuchangia katika maeneo makubwa mawili; eneo la kwanza la michezo na eneo la pili ni kuhusiana na suala zima la lugha ya Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikianzia na michezo, Wabunge wengi na kila Mbunge ambaye amesimama hapa anazungumzia suala zima la michezo na lazima tukubali kwamba michezo ndiyo inayowapa raha Watanzania na ndiyo inayowapa raha watu mbalimbali duniani kote. Kila aliyesimama hapa amezungumzia Simba na Yanga. Hata humu kwenye Bunge letu hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, timu kubwa ambazo tunazungumzia, zinazungumziwa kama sio Simba, itazungumziwa timu ya Yanga. Kwa hiyo, niwapongezeni sana, tena sana kwa hoja nzito ambazo mmezitanguliza kuzitoa. Tunafarijika sana Watanzania hasa Yanga na Simba zinapoingia uwanjani. Hatimaye mmoja akashindwa na mmoja akashinda au mmoja akashinda na mwingine akashindwa, lakini baada ya hapo tunakuwa kitu kimoja udugu wetu unaendelea kustawi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie suala la michezo kwenye suala la vifaa na wataalam. Tunajua kwamba kuna kitu kinaitwa UMISETA na kuna kitu kinaitwa UMITASHUMTA. Sasa tukianzia na UMITASHUMTA, ni ngazi ya mwanzo kabisa kule kwenye shule za msingi hasa zile shule zetu za awali. Sasa tukienda kule kitu ambacho ni changamoto kubwa ni vifaa, vifaa kule hakuna. Hakuna mipira, hakuna mikuki kwa ajili ya kurusha, hakuna visahani kwa ajili ya kutupa, hata viwanja vyenyewe ni mtihani mkubwa sana kwenye eneo la michezo. Kitu kikubwa na cha kushangaza mpira wa miguu ndiyo mpira unaopendwa, ukienda kwenye zile shule hata magoli hakuna. Ukienda wewe kama Mbunge unaambiwa sasa Mbunge tuletee magoli, Mbunge tuletee mipira, sasa mipira hiyo hata ukipeleka, magoli hakuna. Wanacheza nini? Hakuna cha kucheza. (Makofi)
Kwa hiyo, kwenye bajeti hii ambayo imeidhinishwa, kwa ushauri wangu ni lazima tuangalie kwenye shule zetu za msingi na za sekondari kupeleka mipira pamoja na vifaa vingine vitakavyowasaidia watoto au wanafunzi kucheza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hiyo ukiachana na vifaa vya michezo wa mpira, hakuna wataalam. Kwenye shule zile za msingi hata sekondari hakuna hata mwalimu wa michezo, yaani mwalimu tu mtafute huko mtaani au wapi sijui ndipo aende. Tunazungumzia leo timu ya Taifa, kama wale wasingekuwa na wataalam, hiyo timu ya Taifa ingeweza kupatikana? Au timu ya Yanga isingekuwa na wataalam wangefikia pale walipofikia? Au timu yetu ya Simba isingekuwa na wataalam wangefikia pale walipofikia? Isingewezekana! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitaka kujenga kitu, anzia kwenye ngazo ya shina kule. Hata Cchama chetu cha Mapinduzi watu wako shinani kule mpaka huko Taifani. Sasa tuanze kwenye shina kule kujenga hii michezo ili tuibue vipaji kwa ajili ya watoto hawa waendelee mbele ya safari. Hili ni muhimu sana katika ustawi wa michezo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kuchangia kwenye hilo eneo la michezo nataka nizungumzie kwenye suala la lugha. Tulizungumza hapa, lugha ni sauti za nasibu zinazobeba maana na zilizokubaliwa na jamii ya watu ili zitumike katika mawasiliano. Kwenye lugha hakuna lugha iliyokuwa bora zaidi ya lugha nyingine, isipokuwa lugha huongeza msamiati wake. Lugha inakua na lugha inakufa, kufa kwa lugha ni kwa kutotumiwa na watu wengi duniani na kupunguza msamiati wake. (Makofi)
Leo tukizungumzia suala la Kiingereza, sio lugha bora kulikoni lugha ya Kiswahili isipokuwa watu wengi wanazungumza. Tukizungumzia hali kadhalika Kifaransa, Kifaransa sio bora kuliko lugha nyingine isipokuwa Kiswahili chetu ni lugha bora na ziliwekwa hizo lugha kwa sababu ya kututawala. Sasa kama tuna lugha yetu kwa nini tusiitumie hiyo lugha yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni muhimu kutumia lugha ya Kiswahili na tujisikie tuna raha, amani kwamba tuna lugha yetu ambayo itazungumzwa ndani ya Bara letu la Afrika na watumiaji wa lugha hii ni wengi kweli. Siku hadi siku wanaongezeka duniani kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa mantiki hiyo au kwa muktadha huo kuna suala la wakalimani. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri hapa anatueleza, wakalimani waliopo wote jumla yake ni 45 tu na kati ya 45 hao 20 ndiyo wataalam, 25 wanahitaji usaidizi. Kwenye eneo hili ni lazima tutengeneze mkakati muhimu kuhakikisha kwamba wakalimani hawa wanaongezwa. Kwa mfano leo, Afrika nzima ikisema tunahitaji wakalimani wawili kila nchi, au hata mmoja tu ina maana kwamba hatuwezi kutosheleza mahitaji ya wakalimani kwa sababu tuna nchi zaidi ya 56 na wakalimani waliopo ni 45. Tutafika kweli? Lugha ni biashara, wakalimani hawa ni biashara. (Makofi)
Kwa hiyo, tukiongeza wakalimani bado tutaongeza fursa ya biashara ndani ya lugha yetu ya Kiswahili. Naomba hili lizingatiwe kwa umakini mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, nimesema nitachangia katika maeneo mawili tu wala sio mengi; la mwisho, kama tunavyofahamu na tunavyotambua Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisisitiza sana suala la lugha na sasahivi tunae Mama Samia Suluhu Hassan.
Ninachoomba na kushauri, katika wasaidizi wake, Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan kuwe na msaidizi maalum wa lugha ya Kiswahili kama walivyo washauri wengine katika eneo la siasa, uchumi na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana. (Makofi)