Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ambayo hata mimi pia ni Wizara ambayo nimehusika kwenye kufanya kazi, kwa maana ya sekta ya michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo mawili ya kuchangia kwenye Wizara hii, jambo la kwanza ni suala la soka, lakini suala la pili ni suala la BASATA.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza mwekezaji mkubwa aliyeingia kwenye mpira wa miguu, kwa maana ya Azam Media Group kwa kile kitendo alichokifanya ndani ya nchi yetu. Azam Media Group wamewekeza zaidi ya shilingi bilioni 225 kwenye soka la Tanzania na ndio kitu cha kwanza kimefanyika kwenye East Africa, hakuna nchi yoyote ambayo haki ya matangazo imepata shilingi bilioni 225 kwa wakati mmoja ni Tanzania tu imetokea, lakini tu kitendo hiki hakiipi manufaa soka, kitendo hiki kinaipatia Serikali shilingi bilioni 34 kama kodi, kitu ambacho kwa miaka yote hakijawahi tokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kattika kufanya hilo nataka nizungumzie suala la viwanja. Mwekezaji huyu amewekeza fedha zote hizi kwenye soka la Tanzania; ana tv production yenye quality nzuri kama tunaangalia premier league Uingereza, lakini viwanja tulivyonavyo vinatimua vumbi. Inatia hasara sana kwa sababu gani, leo hii tunazungumzia shilingi bilioni 34 ambayo Bakhresa anaenda kuipatia kama kodi nchi hii, bajeti ya Serikali ni shilingi bilioni 54 ya mwaka mzima ya Wizara ya Michezo, lakini bado Serikali haioni haja ya kuhakikisha viwanja hivi vinaenda kuwekwa mikeka ambayo Tanzania nzima tungekuwa tunajivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikupe mahesabu machache tu; kiwanja kimoja kuweka mkeka ni shilingi milioni 300; kwenye shilingi milioni 300 maana yake unazungumzia shilingi bilioni tatu ni viwanja 10 na shilingi bilioni sita ni viwanja 20 ambavyo unakuwa umemaliza nchi nzima. Tuiombe Serikali na hapa Mheshimiwa Waziri na nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu na niiombe Serikali na nimuombe Rais, kama tumeweza kupata shilingi bilioni 34 kwa wakati mmoja tunashindwaje kutenga shilingi bilioni sita tu katika shilingi bilioni 34 tukaweka mkeka nchi nzima na tukawa tumefuta historia ya viwanja katika Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inatia hasira na inasikitisha sana. Utakuja na hoja hapa kwamba hivi viwanja vinamilikiwa na CCM, inawezekanaje baba ambaye ni CCM anashindwa kuongea na mtoto ambaye ni Serikali ili Watanzania waweze kupata nyasi nzuri kwenye Taifa hili? Inawezekanaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kubaki kwenye michakato, michakato, michakato kuhusu viwanja. CCM kwenye sera yake/kwenye ilani inasema; tutaboresha mazingira ya michezo nchini. Michezo ipi nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ukienda pia kwenye Sera ya Michezo ya mwaka 1995 inazungumzia suala la kuboresha viwanja nchini. Serikali inazungumzia kuboresha viwanja, CCM inazungumzia kuboresha viwanja, lakini nenda Jamhuri pale Dodoma angalia, Wabunge tunafanya mazoezi kwenye vumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuiombe Serikali na nimuombe Rais, shilingi bilioni 34 atupe bilioni sita tu. Haya mambo ya negotiation kati ya CCM na Serikali yabaki kwao sisi tuone nyasi zinacheza, watoto wa Kitanzania wacheze mpira sehemu nzuri. (Makofi)

Mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri una fursa ya kuandika historia kwenye Taifa hili, una fursa ya kufanya vijana wote wa Tanzania wakusifie, nenda ongea na Rais, ongea na Wizara ya Fedha wakupatie shilingi bilioni sita, weka viwanja…

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa. Endelea nimekuruhusu.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji katika hoja yake ya viwanja. Yaani hivyo viwanja vya mpira ndio vimegeuzwa pia sasa viwanja vya kila maonesho, viwanja vya bongo flavor kama anavyosema Babu Tale, viwanja vya gospel, yaani kila mtu anayetaka kufanya kitu chake anaenda kwenye hivyo viwanja vya mpira. Na matokeo yake ndio haya ambayo tunaona sasa fedha imewekezwa, lakini wapi tutachezea?

SPIKA: Mheshimiwa Sanga.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, naipokea Taarifa yake kwa sababu ni kweli na amesahau tu kusema pia hata gwaride la majeshi linafanyikia kwenye viwanja hivyo hivyo. Tungekuwa na viwanja ambavyo vina nyasi za bandia, mnazungumza viwanja vyenye nyasi za bandia visingekuwa vinaharibika kama ambavyo vinaharibika hivi. Leo hii ukipanda nyasi kesho kutwa JKT wameingia wanapiga gwaride, nyasi zimekanyagwa zote zimeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuiombe Serikali angalieni haja, michakato kati ya CCM na Serikali isituumize Watanzania tunaopenda mpira kwenye Taifa hili. Tunaomba shilingi bilioni sita katika shilingi bilioni 34 ambazo mmezipata Serikali mtuwekee viwanja carpet tumalizane na nyie endeleeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere alijenga viwanja Taifa hili kila kona. Leo wakikwambia utafute uwanja kama wa Jamhuri hapa Dodoma ujenge, utapata sehemu gani ya kujenga uwanja mkubwa kama ule? Nenda Mkwakwani, nenda Sokoine, nenda Ali Hassan Mwinyi pale Tabora, lakini nenda CCM Kirumba wakwambie leo jenga, Nyerere alijenga, sisi Taifa la leo tunashindwa? Watu milioni 55 tunashindwa kuweka nyasi za bandia kwenye Taifa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Nyerere ameweka majengo yote yale tunakaa. Kwa kweli, niombe Mheshimiwa Waziri, nitashika shilingi kama haya mambo hamtayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine nipende kuzungumzia, sitakuwa na mambo mengi; jambo lingine ni suala la BASATA. Ukiangalia BASATA ni Baraza la Sanaa la Taifa, lakini saa hizi imegeuka ni Mahakama ya Sanaa ya Taifa, kitu ambacho mimi niseme kitu kimoja, wasanii wa nchi hii asilimia 90 wamejipambania wao wenyewe hadi pale walipofikia na si kwa jitihada za sekta ya Wizara ya Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Diamond ametoka si kwa sababu alipita Chuo cha Bagamoyo, leo Ali Kiba ametoka si kwa sababu alipita Chuo cha Muziki Bagamoyo, ametoka kwa jitihada zake, lakini BASATA wanatengeneza urasimu wa kwamba waanze kuweka kwamba wimbo kabla haujatoka lazima upitie kwao, ukaguliwe ili waangalie ubora wa huo wimbo. Hiki kitu ni mlango, hili ni dirisha la kuwaumiza wasanii; ndio maana nasema ni mahakama, kwa nini?

Mheshimiwa Spika, leo hii kama kuna mtu ana bifu (ugomvi) na Ali Kiba, Ali Kiba akitoa wimbo huyo mtu anazunguka BASATA anawapa hela BASATA wanazuia ule wimbo. Tunatengeneza wizi, katika hili nimheshimu Mheshimiwa Waziri kwa sababu aliingilia kati akajenga heshima kwenye nchi, hali imetulia. Msingefanya vile mnataka kumgombanisha Rais na wasanii wa Tanzania hii kwa uzembe wa BASATA. BASATA kazi zake ilizonazo, kazi ambazo BASATA wanazo ni kusimamia maendeleo ya muziki wala sio kufungia wasanii na wala sio kufungia muziki kwenye Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapomfungia Diamond, diamond peke yake unapomfungia maana yake umefungia wasanii wengine walioko nyuma yake, maana yake umefungia producer wa muziki, maana yake umefungia bodyguards wake, maana yake umefungia shughuli nyingi asimame asifanye kazi.

Mheshimiwa Spika, sasa tutakuwa tunazalisha wasanii au tunaonesha? Ndio zile sheria ambazo ulisema ni za kikoloni, zimejikita kwenye kudhibiti kuliko ku-facilitate wasanii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuombe BASATA hawana jukumu lingine la kufanya Taifa hili zaidi kusimamia muziki uwe bora. Diamond amefika pale si kwa ajili ya nguvu ya BASATA, leo hii Ali Kiba amefika pale si kwa ajili ya nguvu ya BASATA, wala Harmonize alipo si kwa ajili ya nguvu ya BASATA. BASATA wasimamie tu maudhui kama wimbo ni mbovu wausimamishe, waurekebishe uendelee kufanya kazi, lakini hili jambo ambalo nyie BASATA mnalifanya hatutawaacha, hatutawaacha salama…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, nimekuruhusu Mheshimiwa Saashisha.

T A A R I F A

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka kumpa msemaji tTaarifa kwamba pamoja na mchango wake mzuri na kule kwetu Hai tuna vipaji vya kutosha, wasanii wa kila aina, lakini mpaka sasa hivi BASATA imeshindwa kutusaidia. Sasa nilikuwa namwambia tu kwenye hoja yake aiombe Serikali, BASATA wawekwe pembeni tutafute chombo ambacho kinaweza kutusaidia, ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Unapokea Taarifa hiyo Mheshimiwa Sanga?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, BASATA hawana manpower ya kuchunguza huo muziki ni bora au sio bora. BASATA hawana miundombinu yoyote ya kuchunguza huo muziki ni bora, wanatengeneza dirisha la kuwaonea wasanii wetu katika nchi hii na mimi naungananae kwamba tutafute chombo kingine ambacho kitakuwa na manpower inayojua muziki, imesomea muziki, kitakuwa na watu wataalam wanaojua muziki ili waweze kufanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini mambo mengine sina la kuzungumza, zaidi niungane na Mbunge wa Morogoro kwamba, nchi hii bila arena ni ukoloni. Bila arena nchi hii tunakuwa tumebaki sehemu ambayo haina maendeleo. Dare es Salaam tunahitaji arena ya michezo, sports arena, Dar es Salaam ya watu 60,000; watu 50,000. Rais akitaka kuongea na Taifa hili Uwanja wa Taifa, mvua ikinyesha watu wanaanza kukimbia. Tafuteni arena ambayo Rais akitaka kuongea na watu mnaingia mle ndani mvua inyeshe au isinyeshe Rais anazungumza na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pli, leo boxing inakua, mtafanya sehemu gani? Vikumbi vyenyewe vya watu 2,000/ watu 1,000. Tafuteni Tanzania Arena, andikeni hata JPM Arena au Samia Arena halafu mwisho wa siku Watanzania watawakumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante, lakini sitaunga mkono hoja hadi pale ambapo mtatupa majibu kuhusu BASATA na kile ambacho wanakifanya. Ahsante. (Makofi)