Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote ambaye amenipa uhai wa leo hii kusimama leo na kuzungumza sekta yangu na sekta ya maisha yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii naomba nizungumze na umma huu wa Wabunge pamoja na Taifa hili. Sanaa ni maisha yetu vijana na kama Serikali ina mpango mzuri wa kuongeza ajira kwa vijana basi sanaa ni sehemu nzuri sana ya kuongeza ajira. Msanii kama msanii anayeimba, kuna anaye-produce, kuna director, kuna mpiga picha, kuna kila aina ya kazi, sasa hivi hadi mabaunsa wamekuwa wanaajiriwa kupitia sehemu ya sanaa. Kwa hiyo sanaa ni jambo muhimu sana na tukilizungumza hapa tuzungumzie kwa u-serious wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye upande wa mirabaha; mirabaha kwa wasanii ni jambo la muhimu sana, leo hii Keisha nitazeeka, siasa nitastaafu, lakini kupitia hii mirabaha tutaweza kupata pesa mpaka tunakufa na watoto wetu wataendelea kula hela, kama ambavyo mimi sasa hivi bado naendelea kula hela ya muziki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hii hela ya muziki tunayokula, tunakula kupitia caller tune, ringtones, lakini tunataka COSOTA wasimamie mirabaha. Hii mirahaba itatusaidia sisi ku-generate lot of money, yaani pesa nyingi sana ambazo hizi pesa zitatusaidia sisi wasanii kutengeneza kazi zenye ubora ili tuweze kushindina kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mirabaha ninayoizungumiza hapa kuna sehemu za starehe nyingi sana ambazo wewe huwezi kwenda kwenye starehe kama hauwezi kusikiliza muziki, kwa hiyo mirabaha hii tunayoizungumza sehemu za starehe, sehemu za mabasi, sehemu za hotels hawawezi kupiga muziki wetu bila kulipia pesa, ina maana tunapata pesa nyingi sana, lakini vilevile na Serikali inakusanya mapato mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna mapato mengi ambayo yanakosekana kwa Serikali kwa sababu ya kutokusimamia vizuri mirabaha ya wasanii katika hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine naomba nizungumze juu ya masuala ya maadili, mimi ni mfuasi mzuri sana wa maadili ya wasanii. Ni mfuasi mzuri sana na ni mfano mzuri sana kwa maadili ya wasanii. Leo hii mimi nisingefika hapa kama ningekuwa sina maadili, lakini maadili gani tunayozungumza hapa, maadili ya kufungia nyimbo za wasanii bila kujua hawa wasanii wanatakiwa waimbe nini?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeomba Wizara iwaite hawa wasanaii, ikae nao, iseme wanataka nini katika hizi kazi, lakini siyo wasanii peke yao hata hivi vyombo vya televisions, media zote wawaite, media ziambiwe ni nyimbo gani na nyimbo gani zinatakiwa kupigwa kwa muda gani, kwa sababu kuna muda ambao Watoto wamelala, hawasikilizi nyimbo zingine, lakini kuna hata kwa hawa watu wa filamu wanaigiza filamu na zinawekwa masharti pale chini ya miaka 13 hapaswi kuangalia hii filamu, chini ya miaka 18 anapaswa kuangalia, hivyo, kwa hiyo tuweke utaratibu ambao hawa wasanii watajua ni namna gani wao wanapaswa kuongoza kazi yao ili waweze kufanya kazi zao za sanaa kwa uhuru vizuri. Kwa sababu mwisho wa siku utamfungia huyu msanii ana familia yake, ana maisha yake, ana ndugu zake wanamtegemea hebu tuangalie hili suala kama Wizara ione namna gani ya ku-deal na wasanii katika masuala haya especially masuala haya ya maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimefurahi sana kuona kwamba katika hii hotuba ya Waziri imezungumza kuhusu masuala ya tuzo. Tuzo ni muhimu sana, mimi nimekuwa msanii kwa kipindi cha muda mrefu na nimekuwa nimeshika tuzo mbili za mwanamuziki bora wa kike Tanzania, lakini nimeshika tuzo ya albamu bora ya Zuku. Hizi tuzo zilinifanya mimi niwe motivated kufanya kazi sana. Kwa hiyo leo hii kama Wizara imeona umuhimu wa kuanzisha tuzo hizi basi ione umuhimu wa kuruhusu tuzo zingine za watu wengine kuendelea kufanya kazi kuliko kuwawekea vizingiti vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mtu akianzisha tuzo anaambiwa kipengele fulani usiseme, kipengele fulani usiseme, sasa hizi tuzo zitaendeshwaje, hizi tuzo mnataka ziwe nyingi ili zi-motivate wasanii wetu. Wasanii wapo kila sehemu na wanafanya vizuri na kila msanii ana ubora wake na katika kazi yake.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie jambo moja ambalo wasanii wanahangaika, wasanii wamepata bima za afya, lakini wasanii wanataka bima ya maisha. Tunashukuru sana Wizara, wameweza kutuwezesha kupata bima za afya, lakini wanataka bima za maisha ili wajihakikishie maisha yao hawa wasanii, tunaomba sana sana hili jambo liendelee, liwekwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naomba pia nizungumze juu ya masuala ya maadili ya mavazi, hili suala jamani naomba sasa Serikali ituambie ni mavazi gani msanii anapaswa avae. Je, akienda kufanya video kwenye swimming pool anatakiwa avae baibui au nikabu? (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tujiulize ni mavazi gani haya ambayo yanahitajika kwa wasanii wavae? Je, tuangalie asili ya Mtanzania vazi lake ni nini? Turudi tena huko kwenye tamaduni zetu, tuangalie Mtanzania anapaswa kuvaa nguo ya aina gani, ili akifikisha ujumbe ajue anafikisha ujumbe kwa namna gani. Wenzetu tunawaona nje wanavaa swimming costumes kwenye swimming pool kwa sababu ndivyo utamaduni wao unavyosema. Basi na sisi tuangalie kwenye swimming pool tuvae nini, tuvae nikabu au tuvae skin tight au tuvae nguo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni suala la uhalisia, leo hii tutawalaumu wasanii wanaenda kurekodi nje South Africa wapi, kwa sababu wanafuata facilities, hizi facilities zinawasaidia wao kuonesha uhalisia katika kazi zao. Sasa leo hii kama facilities hapa Tanzania haturuhusiwi kutumia nguo za polisi, haturuhusiwi kutumia sijui mahakama, sasa tutafanyaje kazi kama wasanii? Uhalisia utatoka wapi? Tutashindana vipi kitaifa na kimataifa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Diamond kusema kweli, Diamond anatuwakilisha vizuri sasa hivi Diamond anagombea tuzo ya BET. Ningeomba Wabunge wote hapa wam-support Diamond kwenye ma- group yao ya maeneo yao wapige kura kwa ajili ya Tanzania. Diamond hayuko pale kwa sababu ya Diamond au kwa ajili ya Wasafi au kwa sababu ya Babu Tale hapana, Diamond yuko pale kwa ajili ya Watanzania na anawawakilisha Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi naomba Bunge hili wahamasishe wananchi wao huko wanakoenda, wampigie kura Diamond aweze kuleta tuzo hii Tanzania proudly kabisa na sisi tuone kwamba tumepata hii tuzo ya mwanamuziki ambaye anaiwakilisha vizuri Tanzania hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo machache na Bunge lako hili Tukufu, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Lakini naomba niunge mkono hoja endapo haya mambo yatatekelezeka, lakini nilisahau jambo moja la mwisho samahani kweli muda wangu haujaisha. Kuna suala hili la arena. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, arena arena arena, Babu Tale umesahau kuwaambia kwamba…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Keisha muda wako umekwisha.

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)