Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii na mimi niishie hapo hapo alipoishia mzungumzaji wa mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuwa na timu ya Taifa madhubuti tukiziweka akili zetu kwa kutegemea kwamba Simba na Yanga ndio zitakazofanya timu ya Taifa iwe bora tutakuwa tumechelewa sana. Taifa lolote duniani linawekeza katika sera na katika michezo Taifa lenyewe na Taifa kama Senegal, Mali na mengine yote yaliyoko katika ukanda wa Magharibi yamewekeza katika tasnia ya ufundi, lakini pia yakawekeza katika academy. Hili ndilo jukumu la msingi la Serikali, lakini hatuwezi tukaviachia vilabu jukumu la kuendesha timu ya Taifa hiyo haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninachotaka kusema wakati Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita anahutubia Bunge lako Tukufu alieleza wazi hapa kwamba sasa ataanza kutenga fedha kwa ajili ya kuziwezesha timu zetu za Taifa. Huku ndio tunakopaswa kuelekea, hatupaswi kuelekea kuzisubiri Simba na Yanga kwamba ndio zitakuja kututengenezea timu ya Taifa, ni lazima uwekezaji ufanyike kwa maana kwamba tuandae wakufunzi waende wakapate mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuandae uwezeshaji wa kisera wa kuwezesha academy ziweze kufanya kazi, lakini pia na uwekezaji katika tasnia nzima ya michezo uweze kuwa wenye kueleweka kama ambavyo kwenye Klabu ya Simba sasa hivi tunaanza kuona matunda ya uwekezaji wetu baada ya miaka minne ya mwekezaji wetu Mohamed Dewji - Mo, ambaye sasa anatupeleka katika hatua ya champions league katika kipindi cha misimu mitatu, mara mbili tumefika hatua ya robo fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningetaka kuchangia eneo lingine ambalo limezua mjadala kidogo katika Bunge lako Tukufu. Nataka niseme katika historia ya mpira wetu tangu mwaka 1961 ambapo Taifa hili limepata uhuru, huko nyuma hatukuwahi kuwa na wachezaji wa kigeni hebu tujiulize ukiondoa mwaka 1980 ambao tumekwenda AFCON, ni wakati gani mwingine tumewahi kufika hatua hizo wakati huo hatukuwa na wachezaji hawa wa Kimataifa. Isije ikawa watu wanapaliwa na hili biriani ambalo Simba inacheza ndio wanaanza kuleta hoja nyepesi nyepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema kwamba mpira ni uwekezaji kuna mtu pale ataweka bilioni 20 kuwekeza ni lazima aoneshe mchezo wake katika uwanda mzima wa kibiashara. Kwa hiyo, hili jambo tuliweke katika mawanda hayo.

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Rashid Shangazi kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hassan.

T A A R I F A

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante napenda kumpa taarifa mzungumzaji anayeongelea kuhusiana na wachezaji wa kigeni. Wachezaji wa kigeni sio tu wanaleta ubora wa ligi yetu ya Tanzania bali wanaongeza kipato cha nchi. Mfano, mchezaji mmoja ambaye ni wa nchi za SADC ili uweze kumsajili maana yake unahitaji kutumia dola 4,700 ambapo ni sawa na shilingi 11,128,880 huyo ni wa nchi za SADC. Mchezaji wa Afrika Mashariki ili uweze kumsajili mchezaji mmoja unatakiwa utumie dola 3,260 sawa na shilingi 7,621,880. Kwa hiyo, kwa timu moja ikiweza kusajili wachezaji wa nchi za SADC kumi maana yake Taifa linakwenda kupata kipato cha shilingi 111,880,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ikiweza kusajili wachezaji 10 wa Afrika Mashariki maana yake Taifa linakwenda kupata kipato cha shilingi 76,218,800. Kwa hiyo, wachezaji waruhusiwe kuja kwa wingi kutoka nje ya nchi ili Taifa liweze kupata kipato. Ahsante kwa taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rashid Shangazi unaipokea taarifa hiyo?

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Zidadu ambaye ndiye Mwenyekiti wa timu ya Namungo, anaelewa hiki ninachokizungumza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa taarifa hii pia nimuombe Mheshimiwa Zidadu, juzi wakati lile goli la Bernard Morrison linafungwa wanafunzi wa shule ya Nyangao walishangilia sana, tumepata taarifa kwamba wale wanafunzi wana kesi kidogo kule kwa hiyo, wanafunzi wale wasamehewe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza ni kuhusu TFF. TFF hii tutende haki imefanya kazi kubwa sana, nadiriki kusema ukiondoa TFF ya Leonard Chila Tenga hii ndio inayofuata kwa kusimamia mpira. Sasa hivi timu zote under 17, under 20, timu za wanawake pamoja na ligi ya wanawake inachezwa hapa nchini ni kwa sababu ya TFF hii chini ya Karia pamoja na Wilfred Kidau wanafanya kazi nzuri sana. Huwezi ukafananisha na FAT ambayo ilikuwa na Mheshimiwa Mhata pale na hii TFF ya leo, wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rashid Shangazi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kakunda.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Shangazi kwamba kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe Tanzania imetoa mchezaji wa mpira wa miguu mwanamke kwenda kucheza mpira wa kulipwa nje ya nje. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rashid Shangazi unaipokea taarifa hiyo?

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili na hiyo ndio kazi ambayo anaisimamia Wallace Karia pamoja na Wilfred Kidau.

Waheshimiwa Wabunge lazima tujikumbushe tunapokimbilia kwenye kanuni, haswa tukizingatia mchezo namba 208 ambao kuna watu wanajificha kwenye kanuni; kanuni hizi hizi katika msimu wa mwaka 2016 kuna timu moja ililipa nauli kwa timu ya Ndanda FC itoke Mtwara ije icheze mechi ya mwisho uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Wakati kanuni inataka kwamba mechi ikachezwe uwanja wa ugenini kule Ndanda wakati ule kanuni hazikuwepo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna timu moja imemsajili mchezaji wa timu ya Taifa Kelvin Yondani akiwa kwenye jezi ya timu ya Taifa kwenye hoteli ya TANSOMA pale gerezani kanuni zikiwepo. Kuna mchezaji anaitwa Mbuyu Twite amesajiliwa kwa kanuni hizo hizo kwa milango ya uani na Mheshimiwa Tarimba, yote hayo unayajua leo mbona tunamhukumu Karia kwa kuvunja kanuni? (Makofi)

T A A R I F A

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rashid Shangazi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tarimba Abbas.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba afute kauli yake kwa sababu mimi habari hizo sizitambui, ili zisiwepo katika Hansard tafadhali sana. (Makofi/ Kicheko)

NAIBU SPIKA: Haya, Mheshimiwa Rashid Shangazi uzifute taarifa zinazomhusu Mheshimiwa, ama ufute jina la Mheshimiwa Abbas Tarimba kwa sababu yeye hizo taarifa unazosema hana taarifa nazo.

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, hizi taarifa anazo na anafahamu kwamba wakati Mbuyu Twite anasajiliwa yeye alikuwa wapi na ni mdau mkubwa sana wa michezo. (Makofi)

Sasa nilitaka tu niseme kwamba TFF kama kuna mapungufu ni mapungufu ya kibinadamu, lakini kazi inayofanyika pale ni kazi nzuri tunapaswa tuwapongeze. Hata hii hatua ya Simba na Namungo kufika hatua ya robo fainali hatuwezi tukazipongeza hizi vilabu bila kuitaja TFF, wala bila kugusa tasnia nzima ya michezo kwa namna ambavyo imeshiriki. (Makofi)

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge taarifa zimeshakuwa nyingi sana na muda wangu unakimbia taarifa hii itakuwa ya mwisho. Mheshimiwa Katani Katani.

T A A R I F A

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, najua wewe ni mtaalam wa sheria na kwenye sheria wanasema kutenda kosa ni kosa kurudia kosa ni uzoefu wa makosa. Sasa kilichofanywa na Klabu kubwa ni kuwanyoosha watu wasimamie sheria, nampa taarifa mzungumzaji. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rashid Shangazi unaipokea taarifa hiyo?

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa vizuri kwa sababu Bernard Morrison alisajiliwa na Yanga tarehe 17 Januari wakati dirisha la usajili limefungwa tarehe 15 Januari, amepita dirisha gani kusajiliwa ndio maana ilikuwa rahisi kutoka Yanga kwenda Simba. Kwa hiyo, mpokee haya machungu wakati tunaendelea kuboresha, lakini ukweli ndio huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana ahsante kwa nafasi hii. (Makofi)