Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na ningependa kuanza kwa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, nampongeza Mheshimiwa Rais hasa kwa ile ziara yake ya majirani zetu Kenya. Ziara ile Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi imeendelea kufungua fursa za kibiashara sio tu kwa sisi ambao tunatoka tunakolima mahindi kama mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na hususani Mafinga, lakini kwa maeneo mengi mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza jitihada hizi kwa sababu katika maisha huwezi kuchagua jirani, lakini jirani ndio ndugu yako. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na hii kama yeye diplomat namba moja, hii ndio maana halisi ya diplomasia ya uchumi. Lakini pia naendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wa Mabalozi ambao miongoni mwao watakuwa ni Wakurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwa sababu kwa muda mrefu Wizara ilikuwa ukiacha Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Utawala na Fedha na Chief Accountant na mtu wa PMU, the rest walikuwa wanakaimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kitendo hiki cha kuteua kwa kweli ni jambo la kupongeza sana na linawapa watumishi wale confidence katika kufanya kazi. Lakini pia nitumie nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri kwa uteuzi na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu kwa kweli, yaani ninyi ni wanadiplomasia wabobevu na nikuambie tu Mheshimiwa Waziri, matumaini aliyonayo Mheshimiwa Rais kwenu ninyi na sisi Wabunge na Watanzania kwa ujumla, ni makubwa sana na sisi tunawaombea mfanye kazi kwa bidii na Mungu atawaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha sasa diplomasia ya uchumi yapo mambo ni muhimu katika kuwezesha jambo hili lifanikiwe kama alivyosema Mheshimiwa Zungu Mwenyekiti wetu wa Kamati. Baadhi ya mambo muhimu ni pamoja na watumishi katika Balozi zetu, lakini pamoja na vitendea kazi kama magari pamoja na nyumba kama ofisi, lakini pia nyumba kama makazi. Sasa katika suala la makazi na ofisi kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti pale. Nianze kwanza na yale maeneo ambayo ni muhimu kwa Serikali kutenga fedha, ili kuendana na mpango wa Serikali wa mwaka 2018/2019 mpaka 2030/2031; mpango kama wa miaka 10 hivi. Mpango huu lengo lake ni ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo na makazi na ofisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema mjumbe aliyetangulia, tunatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya ofisi na makazi na haikwepeki kwa sababu lazima tuwe na ofisi na lazima tuwe na makazi. Lakini hili pia ni eneo moja ambalo Serikali inaweza ikawekeza ikapata fedha. Nitatoa mfano, kwa mfano, Nairobi tuna kiwanja pale ambacho pakijengwa kitega uchumi, projection yake kwa mwaka tunaweza tukapata 2.3 bilion na hivyo tutakuwa tumeokoa pango ambalo tunalipa kwa sasa 1.4 billion.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kujenga kwanza tuta-generate income, lakini pili, tutapunguza gharama ambazo sasa tunaziingia katika kukodi majengo ya ofisi na makazi. Tukienda Congo DRC tuna kiwanja pale ambapo tunaweza tukajenga jengo la ofisi na kitega uchumi ambapo tunaweza tukapata karibu bilioni 13 kwa mwaka na tukaokoa gharama ambazo ni milioni 540 tunazotumia kwa sasa. Lakini vivyo hivyo tukijenga Comoro tunaweza tukapata mapato milioni 520, lakini tukawa tumeokoa milioni 420. Kwa hiyo, kiujumla kama unapata 520 na umeokoa milioni 420 umepata kama bilioni moja. Kwa hiyo, niombe kwa Serikali na hasa hususani Wizara ya Fedha kujenga majengo nje ya nchi sio luxurious, ndio uchumi wenyewe kwa sababu tutaokoa fedha lakini pia, tutakuwa tumeingiza fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika taarifa yetu ya Kamati, unaweza ukaona yako maeneo ambako mpaka sasa hivi yanatuingizia fedha nyingi sana mojawapo ni hiyo New York. Lakini katika mwaka huu wa fedha huu ambao tunaumaliza, tunatumia karibu shilingi bilioni 22 kwa makazi na ofisi. Bajeti hii tunayoenda nayo tutatumia bilioni 24 kwa makazi na ofisi, masuala ambayo kama tutajielekeza katika ule mkakati wetu wa miaka 10 kwamba tujenge na tukarabati baadhi ya maeneo na bahati nzuri viwanja vyetu viko maeneo ambayo ni prime, kwa hiyo, tutaokoa hizi gharama lakini pia tuta-generate income, lakini diplomatically unapokuwa na jengo lako mwenyewe nayo inaongeza hadhi ya heshima katika Taifa lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni suala la watendaji na maafisa katika Balozi zetu, ni muhimu sana Balozi hizi ili kuleta tija katika diplomasia ya uchumi zikawezeshwa kwa kupeleka maafisa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumezungumza hapa ndani nadhani ni miaka minne na kuna mwaka mimi nilishika mpaka shilingi, lakini mara zote Serikali ilisema watapeleka, watapeleka na mbaya zaidi maafisa wengi wamerudi. Nchi kama Marekani ina tofauti ya masaa baina ya West na East masaa matatu, sasa unakuwa na afisa pale mmoja au unakuwa na Balozi tu. Nchi kuna vituo nitatoa mfano hapa. Vituo ambavyo ni multirateral kwa mfano, Kituo kama Geneva pale kuna Mashirika makubwa ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Kazi, Shirika la Afya, WTO wako pale, lakini sasa unapokuwa tu na Balozi bila maafisa wa kumsaidia tija ya diplomasia ya kiuchumi haiwezi kupatikana. (Makofi)

Maeneo kama Rome kuna mashirika pale ya Kimataifa, lakini hata pale New York kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unafanya kazi kwa kutumia Kamati zake zile sita ni kama hili Bunge Waheshimiwa Wabunge, tunakutana kwenye Kamati tunakubaliana tunakuja hapa tunayahitimisha, vivyo hivyo Umoja wa Mataifa ndivyo unavyofanya kazi, kwa hiyo, kama huna staffing ya kutosha ina maana kuna Kamati itakaa, itajadili mambo, itayapitisha, wewe utakuwa umekosa mchango wako ama kwa namna nyingine utakosa kitu ambacho kingeweza kukunufaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, masuala ya peace keeping, Umoja wa Mataifa umeendelea kupunguza budget ya peace keeping, lakini sisi ni moja ya nchi ambayo inashiriki sana katika masuala ya peace keeping.

Sasa kama hukuwepo kwenye ile Kamati ina maana ile bajeti itapita, lakini kama ungekuwepo au masuala kama ya wakimbizi kama ungekuwepo ungejenga hoja kwamba jamani jambo hili ni la muhimu lisipite, tulirekebishe kwa mtindo moja, mbili, tatu. Kwa hiyo, huu ni umuhimu mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunapeleka maafisa ili kusudi hiyo diplomasia ya uchumi iweze kutimilika na iweze kuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi kama China unakuta Balozi yuko peke yake na wale waambata tu, hana maafisa wale ambao ni foreign service officer wa kumsaidia na ni nchi kubwa, lakini ni rafiki na ina uchumi mkubwa. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali kama ni Wizara ya Fedha kama ni Wizara yenyewe ilione hilo.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, baada ya kuwa nimepongeza uteuzi wa Wakurugenzi niombe pia Wizara, tuweze kushirikiana na Utumishi wapatikane Wakurugenzi Wasaidizi ambao ndio wanakuwa head of section ili kusudi kuwe na succession plan isiwe kama sasa hivi ambapo watu wamekaimu karibu miaka minne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe na hii Mheshimiwa Waziri ni jukumu ambalo liko ndani yenu ninyi kama Wizara, kisha mnashirikiana na Utumishi mnawapandisha watu na Mheshimiwa Balozi Mulamula wewe watu wengi pale ni matunda yako.

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe ni sehemu ya matunda yako, kwa hiyo, unawajua nani ana weledi, wana uwezo kiasi gani, wapatieni watu hizo fursa wawe Wakurugenzi Wasaidizi, diplomasia ya uchumi iweze kuthibitika kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno haya Mungu atubariki sote, Mungu aibariki Tanzania, kazi iendelee, ahsante sana. (Makofi)