Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza sina budi kukushuru wewe kwa kunipatia hii nafasi, pia na kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wao wote wa Bara na Zanzibar kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka kuzungumzia hii diplomasia ya uchumi. Diplomasia ya uchumi ni wazo zuri walilotoa Wizara ya Mambo ya Nje ili kuisaidia nchi kukua kiuchumi. Lakini lengo walilolifanya bado halijafikia. Kwa sabababu lengo lilikuwa kutafuta masoko, masoko bado kitendawili, hamna masoko na hayo masoko, ilikuwa sisi kama Watanzania, tuweze kusarifu bidhaa zetu ziweze kwenda kuuzwa nje, ina maana bidhaa ziwe value added na hayo hatujayaweza kwa sababu hatuna viwanda. Sasa utakuta bado sera ya diplomasia haijakamata kasi.

Vilevile hii sera ilikuwa ihamasishe watalii ambao wana uwezo wa kuja Tanzania. Tanzania ni nchi nzuri, Tanzania Bara kuna Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama nzuri. Ukija Zanzibar kuna fukwe mwanana, kuna bustani ndani ya bahari ambavyo hivyo ni vitu vya maajabu. Lakini kwa sababu hii sera bado haijafanya kazi kikamilifu haya yote hayajaweza kufanyiwa au kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ukiangalia ilikuwa Wizara itoe sera mpya ya mambo ya nchi za nje na ilikuwa hii Juni, 2021 wawe nayo mkononi. Haijapatikana hadi leo na hatukui itapatikana lini. Sasa hii sera mpya ya mambo ya nje ingeshirikiana na diplomasia ya uchumi ina maana tayari tungekuwa tumejua nini tunachokifanya kwa sababu sera ilikuwa idhibiti diasporas wafanyiwe kanzidata ili tujue kila nchi tuna nani na nani wako vipi, lakini tumeshindwa. Balozi zetu kuwadhibiti wanashindwa na ilikuwa hawa diasporas ambao ilikuwa wao washirikiane na Mabalozi wetu, wawe muda mwingi kwa mazingira ya raha na shida wanakua nazo, lakini halitendeki.

Mheshimiwa Spika, utakuta tunawafanyakazi raia wa Tanzania nchi za nje wanapata manyanyaso, wanaharibikiwa, lakini wanashindwa kwenda ubalozi kutokana na sera hakuna inayowafanya wafike ofisi zetu za ubalozi. Sasa hili itabidi wazidi kuliangalia kwa mapana ili waweze kujua kwamba hawa vijana wetu wa Tanzania waliokuwepo nje ya Tanzania nao pia wanataka kusaidiwa. Tazama vijana wetu wale wanaofanya kazi majumbani nchi za nje wanavyonyanyaswa. Mtu anafika ananyang’anywa passport yake, mtu anafika halipwi, aende wapi? Hana pa kwenda, lakini kama hiyo sera mtakapokuwa mmeifanya na mkampa nguvu, atakuwa anakwenda kifua mbele hana matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuja uhaba wa wafanyakazi; Wizara ina uhaba wa wafanyakazi kutoka Makao Makuu, Kurugenzi ya Zanzibar na Balozi zetu. Hata wewe mwenyewe umelizungumza hilo ingawa unalifanyia kazi. Lakini kwa nini mkawa na uhaba wa wafanyakazi ndiyo unaosababisha majukumu yenu yote mshindwe kuyatekeleza kwa sababu mna desk zina majukumu, lakini hazina wafanyakazi. Makaimu ndiyo mmekuwa nao wengi, sasa ina maana hayo mnayoyapanga yatakuwa? Hayawezi kuwa, tatizo lenu ni uhaba wa wafanyakazi, uhaba wa vitendeakazi, hivi sasa hivi magari hakuna ya kutosha na kazi zenu zinahitaji gari, maana mnafuatilia.

Mheshimiwa Spika, ukija Zanzibar hawana gari, ukija Bara Makao Makuu hakuna gari, Balozi zetu hazina gari, sasa hilo pia tatizo. Najua kwa bajeti hii ndiyo mmeshachelewa, hakuna kitakacho. Lakini bajeti ya mwakani mkija haya angalau mawili/matatu mtuletee tuyapitishe angalau tuone yanafanya kazi na hayo ndiyo yatakayowasaidia na ninyi wakati mkishakuwa na sera mpya, ita-guide mambo yenu yote na mtajua ninyi mnafanya na mtafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuja na suala dogo la mwisho; najua mimi nikizungumzia Zanzibar na Muungano tu, tuna miaka 57, lazima nilizungumze na nyumbani. Zanzibar mnayo ofisi, lakini ile sio ofisi ni nyumba, ile imekaa kama rest house. Lakini pale kwenye ofisi yenu mliyosema ofisi, nafasi mnayo ya kutosha. Pale mngejenga kiofisi chenu ambapo mtaa mliokuweko mzuri Maisara, nyumba kuna ofisi za SMZ nzuri, ubavuni nzuri, pembeni nzuri na ninyi mngeteremsha kiofisi chenu pale na nafasi mnayo. Mkawa na rest house ambayo mmeifanya ofisi.

Siku moja mimi nilialikwa kwenye mkutano pale Mambo ya Nje, nimeenda sijui hata niingilie mlango gani. Nimeingia pale nimejikuta niko juu. Mkutano kumbe, daah naambiwa jamani mkutano naambiwa uko chini. Nipenye wapi nitoke huko chini kwenye mkutano kwa sababu ile nyumba mtu alijenga mwenyewe anavyotaka, haikujengwa kiofisi. Sasa inabidi hata utakapokuwa unakwenda kwa shughuli za Kiserikali, inabidi uhangaike. Nafasi tunayo na tutaweza. Ninajua Waziri akiwa mwanamke anakuwa msikivu na ninajua hili japo ofisi ndogo pale kaweke, unaweka alama alikaa Waziri mwanamke kafanya kitu fulani, hiki hapa kinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri kwa hayo machache naunga mkono hoja. (Makofi)