Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Balozi Mulamula kwa kuwasilisha vizuri sana na kwa umahiri mkubwa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Lakini pia naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru watumishi wote wa Wizara hii kwa ushirikiano walioutoa katika uandaaji wa bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa maono mazuri aliyonayo juu ya Wizara hii. Kwa mara ya kwanza Wizara hii inaongozwa na wabobezi wa diplomasia, hakuna atakayebisha Waziri wetu ni mbobezi hakuna atakayebisha, Naibu Waziri ni mbobezi hata Katibu Mkuu wa Wizara hii ni mbobezi katika masuala ya diplomasia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi sina mashaka na watu hawa na namshukuru sana, sana, sana Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo. Wakati Rais wetu analihutubia Bunge baadhi ya maneno ambayo aliyazungumza katika Wizara hii ni kama ifuatavyo na naomba ninukuu alisema; “tunafanya uchambuzi utakaobaini nafasi ya kila ofisi ya Ubalozi katika kukuza biashara, uwekezaji na utalii, uchambuzi huo ndio utakaotumika kupanga Maafisa kulingana na uwezo wa kila Balozi.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nakuja kwenye mchango, tunazo changamoto nyingi sana katika balozi zetu,
Mheshimiwa Rais ameeleza hapa. Bahati nzuri mimi nimewahi kufanya kazi katika balozi zetu, nilikuwa Ubalozi wa Tanzania New Delhi, India ni jambo la kushangaza Ubalozi ule una watumishi watatu ambao wanawakilisha ukiondoa India kuna nchi zingine za uwakilishi. Hapa unajiuliza diplomasia ya kiuchumi utaitekeleza vipi kwa idadi hii ya watumishi. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri maelezo yale ya Mheshimiwa Rais ayafanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie umuhimu wa India kimkakati katika kukuza biashara, kimkakati katika masuala mazima ya utalii. India ndio makao makuu au ndio soko letu kuu la korosho zote zinazotoka Tanzania. Kuna Jimbo linaitwa Kerera, korosho zote za dunia hii zinakwenda pale, kwa hiyo, lazima tuwe na watumishi wa kuhakikisha wanalikamata soko lile. India ndio makao makuu ya textile industry ukienda Jimbo la Gujarat, ndio pamba yote inayozalishwa duniani inakwenda kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, India ndio makao makuu ya matibabu, ukiwa na tatizo la kiafya usipopona India wewe ujue huponi tena. Kwa hiyo, kuna kila sababu kuhakikisha tunapeleka watumishi wa kutosha wa kuweza kuhakikisha kwamba tunaweza kupata wawekezaji wa kutosha ambao watakuja kuisaidia nchi yetu. Lakini hali ilivyo sasa inatia huzuni sana haiwezekani nchi kama India sub-continent unakuwa na watumishi watatu, ambao unatakiwa utoe huduma Srilanka, utoe huduma Bangladesh na utoe huduma na Napal jambo hili haliwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuna kila sababu ya kujipanga kimkakati katika kuhakikisha kwamba tunawapanga watumishi wetu kwa lengo zima la kukuza biashara zetu, kukuza utalii wetu na kukuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna suala la rasilimali watu, nimelizungumza upungufu wa watumishi na jambo hili kwa kila mahali ukienda China, kuna watumishi watatu Balozi na watumishi wawili, mwambata wa jeshi na mwambata wa fedha hauwezi ukafanya kazi kwa kuleta tija katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini suala la maslahi ya watumishi; unaweza ukawaona watumishi wa Ubalozini wanapata maslahi makubwa kweli jambo hili si sahihi. Bara la Asia watumishi hawa wamegawanywa kimatabaka, mtumishi aliopo New Delhi, India analipwa tofauti na mtumishi aliyopo China. Mtumishi aliyopo China analipwa tofauti na mtumishi aliyopo Malaysia, kwa nini watumishi hawa tunawapa allowance tofauti? Ningeshauri Mheshimiwa Waziri ili kulinda maslahi ya watumishi tuhakikishe watumishi wetu tunawapa maslahi yaliyosahihi na yanayolingana. Haiwezekani Balozi wa India analipwa tofauti na Balozi wa China, analipwa tofauti na Balozi wa Malaysia wakati hawa wote ni Mabalozi, hawa wote ni watumishi walioko katika nchi zetu kwa hiyo, naomba maslahi ya watumishi yaangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kingine watumishi waliopo Ubalozini hawalipwi stahili zao, takribani miaka kumi hakuna mtumishi wa Ubalozini anayelipwa fedha ya likizo, watumishi hawa inabidi wajitegemee wao wenyewe jambo hili kwa kweli linakwamisha sana ustawi wa kazi zao.
Mheshimiwa Spika, lakini imeelezwa hapa changamoto ya makazi ya watumishi, naomba niishauri Wizara naomba tutumie mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii tuliyonayo ikajenge nyumba katika Balozi zetu, kwa kufanya hivi tutakuwa tumefanya mambo mawili, kwanza tutaisaidia Serikali kutoa fedha kwa kujenga nyumba lakini pili, tutarejesha fedha zetu hapa hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama utawaambia National Housing waende Nairobi wakajenge nyumba, nyumba ambazo watumishi wa Ubalozi watakaa, maana yake Wizara ya Fedha itailipa National Housing. Kama utawaambia National Housing wakajenge nyumba India maana yake watumishi wa Ubalozini watakaa katika nyumba za National Housing na Wizara ya Fedha itailipa National Housing, kwa hiyo, tutaacha fedha zetu ndani ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivi tutajenga nyumba nyingi sana, lakini kama tutaendelea na utaratibu wa kumbana ndugu yangu Mwigulu atoe fedha Hazina, tutakesha hatutamaliza tatizo la nyumba.
Mheshimiwa Spika, kuna mjumbe hapa amezungumzia masuala ya raia pacha, niliwahi kuzungumza ndani ya Bunge hili kwamba tatizo hili liliwakuta wenzetu wa India, lakini walilimaliza kwa utaratibu mzuri sana. Badala ya kutoa uraia pacha, wao waliwatambua raia wao waliopo nje ya nchi kwa kuwapa kadi, wanaitwa Non-residence of India (NRI) na sisi tuwatambue Watanzania waliopo nje ya nchi tuwaachie na uraia wao lakini tuwape kadi Non-residence of Tanzania. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo…
SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa Mbunge wa Longido.
T A A R I F A
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nimpe mzungumzaji taarifa kwamba katika Taifa la Marekani pia wanawapa wageni green card kuwatambua kwamba wanaweza kuishi na kufanya kazi huko.
SPIKA: Unapokea jambo hilo?
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru naipokea taarifa hiyo. Kwa hiyo, ninachojaribu kueleza hapa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana bahati mbaya na muda wako umeishia hapo hapo.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)