Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza kabisa ningependa kwa kuanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa ziara yake ya kwanza aliyofanya nchini Kenya ambayo imeleta matokeo makubwa sana katika economic diplomacy ambayo tunaihitaji na kama tutakuwa tunafuatilia weekend hii Serikali ya Tanzania na Kenya wamekubaliana kuondoa tozo za biashara 30 na pia kuna mchakato wa kuondoa tozo 34. Kwa hiyo, hii ni matokeo ya jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais na hapa pia nimpongeze Waziri wa Viwanda na Biashara kwa kufanikisha jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile ningependa kusisitiza kwamba, mtazamo wa Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kuhusu Kenya kwamba, Kenya sio adui yetu uungwe mkono, Kenya ni mshindani mwenzetu, Kenya wanatupa changamoto. Hivyo tusiwaogope, tunawaweza na tunaweza kuwakabili na ninasema hivi kwa sababu hata nchini Tanzania tupo Watanzania wengi ambao tumesoma nchini Kenya, kwa hiyo, tunawafahamu na tunaweza kushindana nao ipasavyo tusiwaogope. (Makofi)

Aidha, napenda niungane na Wabunge wenzangu ambao wametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusiana na kutengeneza safu mpya kwenye Wizara ya Mambo ya Nje iliyojaa wabobezi kwenye fani hii ya diplomasia chini ya uongozi makini wa Balozi Mwanamama Liberata Mulamula, Naibu Waziri Balozi Mbarouk, Katibu Mkuu Balozi Sokoine, Naibu Katibu Mkuu Balozi Fatma Rajabu lakini pia na Chief of Protocol Balozi Mndolwa ambao kwa ujumla wao wote tuna imani nao kubwa sana na sasa tunaendelea kuona diplomasia ya nchi yetu ikipaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kugusia suala la diaspora; hili jambo lilishajadiliwa sana na tulishapiga hatua ambapo diaspora hawa mikutano mbalimbali ilifanyika nje ya nchi kukusanya maoni ya diaspora lakini hata na diaspora walishirikishwa katika kutoa maoni kwenye Katiba mpya ambayo inapendekezwa. Sasa nimefurahi katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amegusia suala la diaspora lakini na hata katika mapendekezo ya Kamati nao pia wamegusia suala la diaspora.

Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2010 hadi 2015 zilifanyika ziara nyingi sana nje ya nchi kama ambavyo nimesema kukusanya maoni na hawa diaspora pia walishiriki kwenye huu mchakato wa Katiba mpya na yote haya yalipelekea kuanzishwa kwa Idara ya Diaspora ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ambapo kulikuwa na Mkurugenzi mwenye jukumu la kufanya co-ordination na ufuatiliaji. Hivi sasa jambo hili ni kama tumerudi nyuma kwenye hii ajenda nzima ya diaspora, kwa sababu hivi sasa kuna sheria ambazo zinamzuia Mtanzania anayeishi nje kumiliki ardhi, lakini zipo pia sheria ambazo zinamnyima Mtanzania anayeishi nje ya nchi haki ya msingi kwa mfano hata kurithi mali za wazazi wake, Mtanzania anayeishi nje ya nchi hawezi kurithi mali ya baba yake au mama yake kwa sababu sheria zimeweka hicho kizuizi.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo mimi ambacho ningependa kupendekeza ni kwamba Waziri au Wizara ya Mambo ya Nje ije na sera ya diaspora kwa sababu kama tunavyofahamu nchi za wenzetu wanatumia diaspora katika kuendeleza na kukuza uchumi pamoja na uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kusisistiza kwamba Serikali itunge sera ya diaspora na sera hii ni muhimu kwa sababu jambo hili haliwezi kuendeshwa na Wizara ya Mambo ya Nje peke yake, suala hili linahusu Uhamiaji, linahusu Ardhi na mambo kadha wa kadha.

Mheshimiwa Spika, Mbunge mwenzangu aliyetoka kuzungumza ametolea mfano wa India, lakini ningependa kufafanua kidogo India walichofanya wamewapa watu wa India wanaoishi nchi za nje kitu kinachoitwa Peoples of India Origin (PIO) na hii PIO inamruhusu yule mwenye passport ya PIO kuingia India na kutoka muda wowote bila visa, inamruhusu kuwekeza kwenye hiyo nchi, inamruhusu kufanya kazi kwenye sekta zote kasoro sekta ya ulinzi na usalama na jambo lingine ambalo hawaruhusiwi kufanya ni kujishughulisha na masuala ya kisiasa na kupiga kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa mantiki hiyo, na mimi ningependa kupendekeza na sisi kama Tanzania tufike huko, hatuwezi kwenda huko bila kuwa na sera ya diaspora na sheria ambayo itatuelekeza ni namna gani tutatoa fursa kwa hawa diaspora, na tusichanganye mambo mawili diaspora na uraia pacha, hili la uraia pacha tumeshalijadili na limeonekana lina ugumu, hivyo lisituchukulie muda, lakini hili la diaspora ninaamini lipo ndani ya uwezo wetu na hata sasa hivi diaspora wananunua viwanja, wanawekeza lakini wanafanya hivyo kwa kutumia njia ambazo sio rasmi kwa kutumia ndugu, jamaa na marafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunachotakiwa tufanye ni tuwe tu na sera ya kuweka hili suala rasmi na kupitia hiyo tutaweza kujua tuna diaspora wangapi tutaweza kujua mchango wa diaspora kwenye ukuaji wa uchumi wetu. (Makofi)

Kwa hiyo, kwa kumalizia ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie na atupe commitment ya Serikali ya kuja na sera ya diaspora ambayo itawezesha Watanzania wanaoishi nje kuchangia kwenye maendeleo ya nchi yetu na kutupa rasilimali fedha ambayo tunaihitaji kwenye uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)