Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mulamula - Waziri wa Mambo ya Nje kwa taarifa yake nzuri aliyoiwasilisha hapa Bungeni nawapongeza watendaji wote, lakini pia nawapongeza mabalozi wote pamoja na UN agencies zilizokuja leo hapa asubuhi kuungana nasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuzungumzia suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki na muda ukiruhusu nitazungumza mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo ilianza toka mwaka 1967 lakini ika-collapse mwaka 1977, ikaanza tena rasmi mwaka 2000. Watanzania wengi ukiwauliza hata kule vijijini hawajui hii Jumuiya ya East Africa inafanyaje kazi, hawajui tumeungana nini na hawajui hata ile treaty/ule mkataba ambao Tanzania imesainiana na nchi nyingine ambazo ni Rwanda, Burundi, South Sudan, Kenya na Uganda hawajui kimeandikwa nini. Hivyo basi niiombe ofisi ya Mheshimiwa Waziri iweze kueleza ni kitu gani ambacho tumeungana kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa ningependa pia hizi nchi ambazo tumeungana ziweze kwenda kwenye treaty. Tuliona hapa juzi juzi kulipotokea na ugonjwa wa Covid kila nchi ilikuwa na mwelekeo wake, tuliona madereva wengi walikuwa wakikwama mpakani, lakini tuliona pia mahindi yakikwamba pale mipakani, tunamshukuru Mheshimiwa Rais alivyoenda haya mambo yalinyooka, lakini wananchi walikuwa tayari wameshapata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni nini; hoja yangu ni kwamba kama nchi nyingine ina mahindi mengi basi ile nchi inunue yale mahindi. Haiwezekani Tanzania tukawa tunaagiza sukari toka nje wakati labda Kenya kuna sukari na Uganda kuna sukari. Kwa hiyo, hoja yangu ni kwamba hizi nchi zilizoko kwenye Jumuiya zishirikiane kiuchumi, lakini pia ili kuleta nafuu kwa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilikuwa naomba wale wawakilishi wetu ambao wanatuwakilisha huko tunao Wabunge wa East Africa ambao kwa kweli sielewi uwajibikaji wao huwa ukoje, yale wanayoyapitisha kule wangekuwa wanajaribu kutuletea hapa tukaona kumepitishwa nini. Nalisema hilo kwa sababu tunawachagua hapa, lakini tungepata mrejesho kule wamefanya kazi gani kwenye Bunge lile la Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuzungumza suala ambalo limezungumzwa na wachangiaji wengi waliopita hapa. Napenda kuzungumzia suala la uraia pacha. Kama walivyozungumza wachangiaji waliopita ipo haja sasa ya kuangalia sheria yetu hasa ile Citizen Act kuangalia jinsi gani tutaweza kuwa-accommodate hawa Watanzania wanaoishi nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi walioenda nje ya nchi walikwenda kutafuta kazi, lakini wengine walikwenda kusoma, baada ya kusoma walipoona wamekosa kazi huku wakaajiriwa kule. Hivyo basi zile sababu ambazo zilikuwepo zamani labda za kusema kwamba hatuwezi tukawa na uraia pacha wakati ule dunia ndiyo ilikuwa bado haijawa kijiji, kwa sasa hivi dunia ilivyo kijiji ipo haja ya kuwa na uraia pacha. Lakini tunapokuwa na uraia pacha maana yake nini; tunapokuwa na uraia pacha kwanza tunamwezesha yule Mtanzania aliyeko kule nje ya nchi ambaye alikwenda kwa ajili ya kutafuta maslahi na pia kusaidia ndugu zake aweze pia kuwa na ule moyo mkunjufu wa kujiona kwamba na mimi bado ni Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wale watu wako kule wameoa na wamezaa na wengine mpaka wana wajukuu kuwaacha kukaa kule moja kwa moja kwa sababu wamechukua uraia wa nchi nyingine ni kama vile tunakipoteza kizazi cha Watanzania ugenini. (Makofi)

Hoja yangu nilikuwa nataka niishauri Serikali inaweza ikawa-accommodate huu uraia pacha, lakini ikawawekea masharti ya wale Watanzania na huu uraia pacha hauji kwa wageni kwa maana kwamba ya foreigners, uraia pacha uwe kwa Watanzania ambao wamezaliwa humu nchini Tanzania, lakini wameenda kule nje kwa ajili ya masomo na hii katika nchi nyingi za Afrika zinaendelea ku-accommodate hili suala kuna nchi karibu 24 zimesharuhusu uraia pacha. Kwa hiyo, na sisi tujaribu kuangalia sheria zetu na tuwawekee sheria ambazo zitaweza ku-accommodate.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo faida ya kuwa na uraia pacha kuliko kutokuwa na uraia pacha kwa sababu ya uwekezaji kiuchumi pamoja na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia leo ni suala la mabalozi walioko...

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska Mbogo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba jambo analolizungumzia la uraia pacha yaani yako mambo ya kufikiria sana, kwa mfano Mtanzania anakwenda kusoma MarekaniM ameenda kwa ajili ya masomo atazaa huko huko Marekani na kwa sheria za Marekani ukizalia Marekani anakuwa na uraia wa Marekani. Sasa kama huyu mtoto naye hatapata uraia wa Kitanzania tutakuwa tunapoteza watoto wanaenda Ulaya na mama anarudi nyumbani au baba anarudi nyumbani au baba anarudi nyumbani. Kwa kweli hili jambo ni la kufikiria sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Taska Mbogo unapokea taarifa hiyo?

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hiyo taarifa, ni taarifa ambayo ni sahihi, ni kweli kizazi cha Watanzania kinapotea kule ughaibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumzia suala la mabalozi, hawa mabalozi ambao wapo kwenye nchi zile zilizopo ambazo sisi tuna ofisi zetu za balozi kule nilikuwa naomba waitangaze nchi yetu, wanaitangaza vipi. Nilikuwa naomba iwasiliane na Wizara ya Maliasili na Utalii wachukue zile brochures ambazo zinatangaza vivutio ambavyo viko nchini kwetu Tanzania ili waweke kwenye zile ofisi za mabalozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia waweze kuchukua bidhaa ambazo tunazo huku nchini kwetu Tanzania waziweke kwenye ofisi za mabalozi. Nimeona kwenye ofisi nyingine za balozi nchini kule nje ya nchi unakuta kuna bidhaa, kuna kahawa, kuna majani ya chai, kuna nini, kila kitu wame-advertise/wanatangaza zile bidhaa ambazo zinatoka kwenye nchi zao.

Kwa hiyo. nilikuwa naomba hawa mabalozi waweze kufanya hiyo kazi. Lakini zaidi ya hapo wawe na mikutano ya kuangalia kwa mfano mtu yuko Ethiopia ajaribu kuita wale matajiri wa pale Ethiopia labda wenye viwanda vya ngozi au viwanda vya nguo aongee nao jinsi gani wanaweza wakaja nchini kwetu kununua ngozi zilizopo hapa. Ngozi za Tanzania zinatupwa tu, lakini kule Ethiopia wana viwanda wanatengeneza majaketi, wanatengeneza vitu vizuri sana vya ngozi mpaka viatu, lakini sisi ngozi zetu zinatupwa hata ukienda hapa Dodoma zinatupwa, ukienda Dar es Salaam zimetupwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe wale walioko kwenye hizo nchi waweze kuwasiliana na wale wafanyabiashara na wale wenye viwanda ili waweze kuja kuchukua malighafi zinazotokana huku nchini kwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuongelea ni suala la Sera ya Mambo ya Nje, haiwezekani tunakaa tunazungumza kumbe Wizara ya Mambo ya Nje haina sera, niiombe kwanza Serikali ilete Sera ya Mambo ya Nje ili pia wale Watanzania waliopo nje waelewe kwamba sera ya mambo ya nje ni ipi nah ii itawasaidia sana wale Watanzania wanaoishi nje ya nchi. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri alisema kwamba ameagiza Balozi ziwaorodheshe, kuwaorodhesha sawa waorodheshwe, lakini je, baada ya kuwaorodhesha Sera ya Mambo ya Nje inasema nini kuhusu watu wanaoishi nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii Watanzania wako kama nilivyosema mwanzo wako zaidi ya milioni moja, lakini hawana fursa pia ya kupiga kura, hatujaweka system kwenye balozi zetu za kuwaruhusu hawa Watanzania kupiga kura. Sasa inapofika wakati wa uchaguzi wale Watanzania walioko nje ya nchi hawapigi kura. Lakini kama mzungumzaji aliyepita alisema kunapokuwa na maoni ya kitu chochote cha Serikali huwa wanaulizwa yale maoni kwa sababu bado ni Watanzania na bado ni kizazi chetu tuweze kuwa-accommodate ili sera hiyo ikitoka nafikiri itajumuisha na hayo mambo mengine wataweza kupata haki zao za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda pia kuzungumzia suala lingine ambalo litakuwa ni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)