Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na awali ya yote naipongeza Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia kuhusu jinsi Tanzania tulivyoshiriki ukombozi wa Bara la Afrika hasa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waasisi wetu Mwalimu Nyerere na wenzake waliamini kabisa kwamba uhuru wetu Tanzania hautakuwa na maana kama nchi za Kusini mwa Bara la Afrika hazitakuwa huru na ndiyo maana ilikuwa ni ajenda kubwa ya wakati ule. Hivyo basi, kwa nchi hii ya Tanzania tulivyoshiriki kwa kiasi kikubwa na wakati ule hasa kwenye Mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ikawa ndiyo base kubwa ya wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi imekuwa kama historia, lakini nakumbusha kwamba maeneo ya Lindi ikiwepo Nachingwea kulikuwa na maeneo ya Matekwe, Kwamsevumtini na kule Mtwara maeneo ya Samora na Lindi Vijijini, Lutamba, Ruvuma maeneo ya Namtumbo yale sehemu ya Seka Maganga na kwingineko ili kuwa ndiyo base na ma-camp ya wapigania uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale pamoja na kuwa base tu lakini bado jamii husika ilikuwa nayo iko katika harakati zile, wanaotoka maeneo yale wanafahamu sana. Hivyo basi, wakati ule sasa, wakati wote wa harakati wa kupigania uhuru mikoa ile ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ilikuwa ni vigumu kwa wawekezaji kwenda kuwekeza kule kwa sababu wakati wowote Mreno anaweza akaja akaleta vurugu kule na wengine, kwa hiyo, hakukuwa salama. Hivyo tukaja kujikuta kwamba maeneo yale kwa namna fulani yakawa nyuma kimaendeleo, huo ni ukweli usiopingika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya harakati zile kwisha maeneo yale sasa Halmashauri husika zikaendeleza maeneo yale, wakaanzisha Sekondari zile za Matekwe na kwingineko, lakini ni juhudi za Halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya kufanya hivyo nini ushauri wangu. Nashauri hivi tunaomba kwa Wizara hii ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa wizara hii naamini kabisa inaongozwa na Mheshimiwa Mama Mulamula na Naibu Waziri na timu yote ya Wizara ya Mambo ya Nje naamini kabisa wanavyofika wakuu wa nchi hizi za Kusini mwa Bara la Afrika tulizopambana kwa kiasi kikubwa kuwakomboa tunaomba muwaambie na muwalete maeneo ya Nachingwea na kule Ruvuma ili waje waone yale makambi, waje waone jitihada zile tulizozifanya sisi wenyewe ndani ya halmashauri husika bado hazitoshi tunaomba mchango wao, tunaomba waje waweke wafanye jambo fulani kama ni la maendeleo ili tuone kumbukumbu kubwa ifanyike kama inavyofanyika sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia hii kwa uchungu kweli, tumeachwa hivyo na ndiyo hiyo naona kama vile historia inajiendeleza vile kwamba kila kitu tuko hivyo tuko nyuma tu…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Zuberi Kuchauka.
T A A R I F A
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe Taarifa mama yangu anachokizungumza ni kweli kabisa na ndiyo maana Mikoa ya Lindi na Mtwara miaka ya nyuma ilikuwa mikoa ya adhabu kwamba mtu akifanya makosa anapelekwa mikoa hiyo na mikoa hiyo haikuendelezwa ni kwa sababu tu ya hayo makambi ya hiyo vita za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele, malizia mchango wako.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napokea hiyo taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo jambo geni kwa watu uliowafanyia hisani wakashukuru na kama mtu hashukuru basi kama kunauwezekano wa kumkumbusha. (Makofi)
M imi naamini kabisa watakapoletwa wale viongozi kule wakaona wakasema hapa ndiyo ilipokuwa camp fulani, hapa ndiyo ANC walikuwa hapa, watakuwa na uchungu fulani wa kuweka jambo fulani vinginevyo wala hawafahamu kwa sababu wako kwenye neema sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ndiyo ombi langu na hii imeshatokea na kwingine na kwingine, siyo ajabu hili ninalolizungumza, wakipelekwa kule wakaja kuona hali halisi ninaomba, ninaomba, ninaamini kabisa Mheshimiwa Mulamula ninakuaminia, ni mama, una uchungu wa nchi hii, ninaomba hilo uliweke katika priority naomba utuangalie kwa kila hali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)