Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia na kutoa ufafanuzi wa hoja ambazo zimetolewa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniruzuku uhai na afya njema na kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Aidha, nichukue fursa hii kwa kipekee kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kwa kuniteua kwanza kuwa Mbunge na pili kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaahidi kuwa nitaitumikia nafasi hii kwa weledi na juhudi kubwa nikiongozwa na falsafa ya kutanguliza mbele maslahi ya Taifa na nitatumia uzoefu wangu wa muda mrefu katika diplomasia na uhusiano wa kimataifa kwa maslahi mapana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kukushukuru wewe binafsi na Mheshimiwa Spika kwa kuliongoza Bunge hili kwa umahiri, hekima, busara na umahiri mkubwa. Aidha, ninaomba kuishukuru Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa maoni na ushauri wao walioutoa kupitia taarifa iliyowasilishwa asubuhi hii. Hii ni Kamati makini kwani wajumbe wake wana uelewa mkubwa wa masuala ya kidiplomasia na hivyo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa ambao umeendelea kusaidia kuboresha utendaji kazi wa Wizara na diplomasia ya nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula, Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki kwa uongozi wake mahiri ndani ya wizara na ushirikiano mkubwa anao nipatia. (Makofi)
Pia ninamshukuru Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara na taasisi zote zilizochini yake kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuishukuru familia yangu kwa upendo na uvumilivu wao na kuendelea kuniunga mkono wakati wote nikitekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri nijielekeze katika kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge. Kwanza nitoe shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na kutoa maoni na ushauri katika kikao hiki ambacho kimejadili hotuba ya bajeti ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, michango ya Waheshimiwa Wabunge wote tumeipokea, na ninaahidi kuijumuisha katika utekelezaji wa mipango ya Wizara, naomba nitolee ufafanuzi wa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nichangie issue au hoja ya itifaki; hoja hii imeongelewa asubuhi hii kwa hisia kubwa, hapa bora nimtaje ni Mheshimiwa Jerry Silaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Wizara inasikitika sana na mapungufu yaliyojitokeza na ili kuepusha changamoto hiyo nakuhakikishia kwamba itifaki inazingatiwa katika shughuli zote za kitaifa ambazo zinawahusisha viongozi wetu wakuu, hususan viongozi na mhimili wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaandaa mkutano ambao utajumuisha stakeholders wote wanaohusiana na mambo ya itifaki na tutawajumuisha pia na Ofisi ya Bunge, Ofisi ya Waziri Mkuu, tutazungumza kwa pamoja ili kuboresha utendaji wa Serikali na kuimarisha uhusiano uliopo katika mihimili yote ya dola katika kuratibu shughuli za kitaifa. Na hiki kikao kitafanyika tarehe 14 mpaka 18 hapa Jijini Dodoma kwa ajili ya kujadili masuala haya ya kiitifaki ya viongozi na tunaahidi kwamba suala hili tutajitahidi lisitokee tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kukamilisha Sera ya Mambo Nje na kujumuisha masuala ya diaspora; Wizara ipo katika hatua za mwisho kukamilisha Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2021 pamoja na mambo mengine sera hiyo pia itatoa mwongozo wa utekelezaji wa masuala ya diaspora kisera na kimkakati kwa manufaa mapana ya diaspora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu wa kujenga Ofisi ya Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar ambayo ina hadhi, kwa sasa Wizara inamiliki jengo la Ofisi ambalo sasa hivi lipo katika ukarabati na ukarabati wake unaendelea kwa nguvu. Naona muda unakwenda sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa ufafanuzi hapa kidogo kuhusiana na issue ya Palestina ambayo imeongelewa na Wabunge hapa. Ni kweli kwamba hivi karibuni mgogoro kati ya Israel na Palestina umeongezeka na kusababisha madhara makubwa kwa pande zote mbili ikiwemo vifo na uharibu wa miundombinu katika miji ya Gaza, Tel Aviv, Jerusalem na Ukingo wa Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania muda wote imekuwa ikilaani mapigano hayo, dhamira ya Tanzania ni kuona mgogoro huo unatatuliwa kwa njia ya amani na utulivu na usalama unashamiri. Tanzania haijakaa kimya kwenye suala hili, tumeendelea kushiriki na kushawishi Jumuiya za Kikanda na za Kimataifa kuchukua hatua zaidi na za pamoja ili kuona mgogoro huo unatatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa mantiki hiyo Tanzania inaendelea kuunga mkono maazimio ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro huo ambao unazitaka pande husika kuheshimu makubaliano ya kuwepo kwa nchi mbili ikiwa ni Palestina huru na Israel salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Tanzania haijabadili msimamo wake kutoka hapo awali na kuhusu msimamo wa Tanzania kuhusu Sahara Magharibi haujabadilika pia. Serikali yetu imeendelea kutambua haki ya msingi ya watu wa Jamhuri ya Kiarabu wa Demokrasia ya Sahrawi kujiamulia mambo yake wenyewe kupitia kura ya maoni na tunaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha ufunguzi wa ubalozi wa Morocco hapa nchini si ishara ya kubadili msimamo wetu, bali ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kutoa fursa kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo suala la utatuzi wa mgogoro wa Sahara Magharibi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kidogo kuhusu ahadi ya msaada wa Falme za Kiarabu. Ni Wizara yetu kupitia ubalozi wake wa Abudhab imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha kwamba msaada wa fedha uliotolewa na mifuko hiyo miwili inapatikana mapema inavyowezekana. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba taratibu zote zimekamilika kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kinachosubiriwa sasa ni Khalifa Fund kutoa fedha hizo ambazo ni dola za Kimarekani milioni mbili kila mwaka kwa muda wa miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha kuhusu hospitali ya Wete mchakato unaendelea, ulikwama kutokana na Covid, lakini hii ni ahadi iliyotolewa na viongozi wa UAE na ahadi hii tunahakikisha kwamba inatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha kuhusu barabara ya Chakechake hadi Wete tayari Serikali imeshasaini mkataba na Saudi Fund tarehe 19 Aprili, 2020 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chakechake hadi Wete - Njia Kongwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine yaliyobakia tutayajibu na kuyawasilisha kwa Wabunge wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)