Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana, Wizara ya kimkakati, Wizara ambayo ina mchango mkubwa sana kwenye pato la uchumi wa nchi yetu. Mimi nitajikita kwenye maeneo matatu na eneo langu la kwanza, linakwenda kujikita kwenye eneo la bomba la mafuta ghafi la EACOP. Naomba nichukue fursa hii kwa moyo wa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha Host Government Agreement na kwa namna ambavyo anakuwa proactive katika kufanikisha masuala haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nimefurahishwa na shareholding structure iliyopo kwenye mradi huu. Ukiachana na masuala mazima ya namna ambavyo mgawanyo ulivyo, lakini pia mradi huu unakwenda kutunufaisha sana ukiangalia kwamba, unakwenda kupita kwenye mikoa 8, lakini wilaya ziko 24, kata 134, vijiji 257 na vitongoji 527. Ni kwa uhakika kwamba, watu wa maeneo haya ambao bomba hili linapita wanakwenda kunufaika, lakini mradi huu unakwenda kutengeneza ajira zaidi ya 10,000. Nilikuwa ninatazama taarifa mbalimbali za Wizara, ninaona vitabu vya Wizara viko silent kueleza suala la wafanyakazi ambao watakuwa skilled na unskilled. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ipo changamoto nyingine kubwa sana pamoja na yote ambayo nimeyazungumza juu. Kuna changamoto kubwa ambayo nitaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha hapa, utoe ufafanuzi kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu, utata huu kwa kweli unazidi kuwapa watu sintofahamu. Nina swali la kuuliza, mradi huu wa EACOP ni nani anakwenda ku-finance mradi huu? Ninajua kwamba Serikali inatenga bilioni 2.6 kwa ajili ya kulipa fidia lakini mradi huu wenye thamani ya USD bilioni 2.5, ni nani anakwenda kuilipa? Kwa sababu, mtu ambaye mlikuwa mnamtegemea ambaye ni Kampuni ya TOTAL, ambaye ni majority share kwenye mkataba huu, hana uwezo wa kulipa fedha hizo mpaka hivi ninavyozungumza sasa nitatoa sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mezani kwangu nina jarida la UK ambalo ni very prominent magazine la energy voice. Mapema sana mwezi wa 5 hata kabla ya mkataba huu kuingiwa, mabenki ya UK, mabenki ya Ufaransa ambayo yalikuwa yametoa ahadi kutoa fedha kwa Kampuni ya TOTAL, kwa ajili ya ku-facilitate mradi, ujenzi huu wa bomba la mafuta, mabenki yametangaza kwamba, hayatatoa fedha hata senti tano tena. Sababu ya mabenki haya kutoa tangazo hili, mabenki yamegoma kwa sababu, wamesema wanakwenda kuunga mkono kampeni ya ku-burn emission masuala ya carbon dioxide. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na naomba nirejee kwa ufupi sana eneo ambalo la magazine hii imeripoti wanasema hivi: “French banks have committed not to provide projects financing for the TOTAL East African Crude Oil Pipe Line – EACOP”. Ukiangalia kwamba kwenye makubaliano yetu, tumekubaliana kwamba mradi huu ujengwe mpaka kufikia 2024 uwe umekwisha kamilika. Lakini kampeni ambayo mabenki haya yanasema yanai-support, kampeni hii inakwenda mpaka kufika mwaka 2050. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kutuambia, kama hafahamu basi ninamuomba awatafute watu wa TOTAL wamuambie fedha hii au mradi huu nani anakwenda kuu-finance? Kwa sababu wao fedha waliyokuwa wanategemea kutoka kwenye mabenki ya Ufaransa, mabenki yamesema hayatoi fedha tena.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, lakini ninaomba.
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa, nakukubalia tuendelee.
T A A R I F A
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante nilitaka kumpa taarifa mzungumzaji, inawezekana kweli anachokizungumza anakijua, lakini sisi hatufungi mkataba na mabenki ya Ufaransa. Tunafunga mkataba na mkandarasi ambaye ni TOTAL, ambaye tayari kwenye mkataba alikuwepo anaweka. Yeye ana uhakika gani kwamba, mkandarasi ana fedha kiasi gani za kuweka hapo? Kwa sababu sisi hatufungi mkataba na yale mabenki, kama ameona hiyo document ni ya kwake na yeye, sisi tunakubaliana na mkataba unaoendelea sasa hivi. Mpaka siku mkandarasi atakapoamua kwamba, hana uwezo wa namna hiyo ndio tutaelewa jambo hilo. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa unapokea taarifa hiyo.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, siwezi kuipokea taarifa hii, labda nimuelimishe kidogo Mheshimiwa Mbunge. Mkandarasi na TOTAL ni watu wawili tofauti. Mkandarasi anayehusika kwenye ujenzi wa mradi wa EACOP sio huyo TOTAL unayemsema wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba niipe challenge Economic Intelligence System ya Taifa letu. Haya ndio mambo ambayo ni very sensitive katika Taifa hili ambayo tunategemea hawa watu watusaidie. Kwa maana taarifa kama hizi kama zimetokea toka Mwezi Mei mwanzoni kabla ya mkataba huu kuingia hizi nchi mbili ilikuwa ni vyema Wizara wakakaa chini na TOTAL wakakubaliana kwamba hizi fedha zinakwenda kutolewa wapi kwa sababu kimsingi toka mwanzo TOTAL walikwishaeleza kwamba fedha wanapata kutoka kwenye Mabenki ya Ufaransa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee, suala jingine ambalo ninaomba leo kauli ya mwisho kutoka Serikalini. Hivi hii itakuwa mara yangu nne ndani ya Bunge lako Tukufu kuzungumzia suala hili kwasababu nimelishazungumza Bunge lililopita na sasa nalizungumza kwa mara ya kwanza katika Bunge la Awamu hii. Suala la Mkataba wa SONGAS, nimelizungumza suala hili mara nyingi sana na nakumbuka hata Mheshimiwa AG amekuwa akisimama humu ndani akitoa ahadi kwamba wanafanyia review mikataba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumebakiza miaka miwili tu ili mkataba wa SONGAS uweze kuendelezwa na nina taarifa, nina taarifa watu wa SONGAS wameshaanza kufanya robbing hata kwa wabunge kutaka mkataba wao uendelee kuwepo. Ninaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu pamoja na Bunge lako Tukufu tuungane kwa pamoja tupinge mkataba huo kuendelea kama mkataba huu haujafanyiwa review. Kwa sababu kama Taifa hatunufaiki kwa namna yoyote na masuala haya yameanza kuzungumzwa toka mwaka 2009 na CAG; mwaka 2018 na CAG, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge mwaka 2005 wakati huo alikuwa Mheshimiwa Shelukindo amezungumza suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapoteza kila mwezi zaidi ya Dola milioni 5 kwa sababu ya mkataba huu mbovu. Ninaelewa, ninaelewa huenda wakati huo walikuwa wanataka ku-rescue nchi, kuitoa nchi kwenye giza lakini tunapokwenda sasa mwaka 2024 wakati mkataba huu unakwenda kuendelezwa, kukubaliwa kuendelezwa. Namuomba Mheshimiwa Rais, nakuomba na wewe kupitia Bunge lako Tukufu, tupinge mkataba huu kuendelea kama haujafanyiwa review ya aina yoyote ili wananchi wetu waweze kunufaika kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kama sisi tuliwekeza kwa sehemu kubwa kwasababu sisi tuliwekeza 73% kwenye Capital Structure halafu SONGAS waka-invest kwa 27% kwenye investment structure lakini kwenye shareholding structure SONGAS wao ndio majority kwa kumiliki 54% haiwezekani. Ninaomba suala hili litazamwe upya na tuangalie na tulitazame kwa namna ya kipekee.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa jambo dogo sana kwa ufupi najua dakika zangu zimekwisha, suala la umeme wa upepo. Leo tunazungumzia suala la energy mixing. Unazungumzia suala la energy mixing, tunajua kuna vyanzo mbalimbali; lakini ni kwa nini upepo umesahaulika?
Mheshimiwa Spika, natoka Mkoa wa Singida; Mkoa wa Singida ni miongoni mwa maeneo ambayo yanaongoza kwa upepo mkali East Africa nzima na inauwezo wa kuzalisha Megawatts za kutosha kutokana na umeme wa upepo. Lakini suala hili limekuwa likipigwa danadana miaka nenda miaka rudi na ninakumbuka mwaka 2017 nilisimama humu Bungeni nikamuomba Mheshimiwa Waziri na ninashukuru huyu huyu ambaye aliyepo sasa, nikamuhoji kuhusiana na suala hili na akasema ndani ya miaka miwili umeme wa upepo Singida mradi utanzaanza kutekelezeka. Lakini mpaka ninavyozungumza hapa hata nguzo hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba suala hili mkumbuke basi na chanzo hiki muhimu sana cha upepo ili kuweza kutusaidia wananchi wa Singida lakini pia na Taifa kwa ujumla kwa kuzalisha Megawatts za kutosha. Baada ya kusema hayo, nashukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki Wabunge wote Ahsante sana. (Makofi)