Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Nishati jioni hii ya leo. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametukusanyisha tena mahali hapa jioni hii tukichangia Wizara hii muhimu kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kipekee pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa namna ya kipekee kwa kazi nzuri anayowafanyia Watanzania, lakini pia kwa mikataba ambayo tayari tumeshaingia na wenzetu wa Uganda katika bomba hili la mafuta kutoka Uganda mpaka Mkoa wa Tanga. Kipekee pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya nishati pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara hii, wamefanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, natambua kwamba, Mheshimiwa Waziri wewe tangu umekuwa Naibu Waziri umeitendea haki Wizara hii, kipekee nitambue mchango wako mkubwa, natambua uipokuwa Naibu Waziri Wizara hii ilikuwa ina mapato ya bilioni 9 kwa wiki, leo hii Wizara inakuwa na kati ya bilioni 42 mpaka bilioni 47 ni hatua kubwa sana, lakini pia shirika lilikuwa katika hali ambayo si sawa kifedha, lakini hivi leo shirika linajiendesha lenyewe na baadhi ya miradi linaweza kusimamia lenyewe kwa fedha za ndani ni hatua kubwa sana hii Mheshimiwa Waziri, lakini jambo lingine pia nikupongeze pamoja na watendaji wako kwa kuchukua hatua; hivi karibuni umechukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote ambao hawafuati maelekezo ya Wizara. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine nataka nikupongeze kwa kusimamia vizuri miradi yote ya kimkakati ukiwemo mradi mkubwa wa Mwalimu Nyerere ambao utazalisha Megawatt zaidi ya 2,115 pamoja na miradi mingine mbalimbali ambayo Wizara inaanza kusimamia na kwa hakika mnastahiki pongezi nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nijikite zaidi katika umeme huu wa REA. Umeme wa REA umekuwa mkombozi mkubwa sana katika maeneo yetu katika nchi yetu ya Tanzania. Lazima tukiri Serikali imefanya kazi kubwa na kwa msingi huo Jimbo langu la Busokelo lina vijiji 56 na katika vijiji vyote 56 vimepata umeme vijiji 55, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. Na kwa msingi huo bado Kijiji kimoja tu cha Kilugu ambacho kipo Kata ya Itete, nikuombe katika awamu hii na mzunguko unaofuata nacho kipate umeme katika awamu hii inayofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, licha ya kwamba, vijiji 55 vyote vimepata umeme, lakini kuna changamoto katika kupeleka kwenye vitongoji. Katika kata ambayo ina vijiji vitano na katika kijiji kimojawapo inaweza ikawa na vitongoji sita na katika vitongoji sita vinaweza vikapata vitongoji viwili; tunahesabu kweli kwamba, kijiji kimepata umeme, lakini vitongoji vinne vyote vinakuwa havina umeme. Naamini katika mipango ijayo basi tuwekeze zaidi katika vitongoji, ili vitongoji vyote sasa vya Tanzania tuone kwamba, tuna umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila mmoja anafahamu kwamba, umeme ndio uchumi, umeme ni viwanda. Umeme ni nuru, umeme ni kila kitu katika maisha ya Mtanzania. Kwa maana hiyo, niipongeze pia Wizara kwa kuendelea katika kuratibu na kuzalisha umeme kwa kutumia njia jadidifu, hususan, renewable energies. Na nimeshuhudia miradi hii, geothermal, ikiwemo ambayo inaendelea kuchorongwa kule kwangu Jimbo la Busokelo tumechoronga vishimo vitatu na dalili zote za kuonesha kwamba, geothermal ipo kwa hiyo, lazima niipongeze sana Serikali kupitia Kampuni tanzu ya TANESCO, Tanzania Geothermal Development Company, ambayo inafanya kazi hiyo ya uchorongaji ni hatua kubwa sana hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote nataka pia nizungumzie Shirika letu la Petrol Nchini, TPDC. Tumeona gesi inavyozalishwa, lakini pili tumeona kutoridhishwa katika usambazaji wa gesi.
Mheshimiwa Spika, Bunge lililopita nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya PIC. Tulitembelea maeneo mengi ambapo TPDC imepeleka gesi, tunawapongeza sana, lakini kasi yake ya kupeleka kwa wananchi bado hairidhishi. Kupitia hotuba hii Mheshimiwa Waziri, naomba sasa watu wa TPDC wajipange namna ya kupeleka cubic nyingi zaidi kwa wananchi. Kwa sasa hivi wamepeleka zaidi ya 733,521 futi za ujazo wakati wananchi zaidi ya milioni 50 tupo Watanzania kwa hiyo, waongeze kasi zaidi katika kupeleka umeme maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri utakapokuja tunataka ueleze kinagaubaga Wizara imetoa miongozo kwamba, umeme ni kweli 27,000/= lakini kuna baadhi ya maeneo umeme hawatozwi 27,000/=. Hii imekuwa ni changamoto na Wizara kadiri mnavyotoa maelekezo mara nyingi watendaji wenu wa chini hawawaelewi. Nafikiri kuna namna ambavyo mnaweza mkafanya ili waweze kuelewa kwa sababu, kama Serikali inapeleka umeme kwa 27,000/= lakini watendaji hawafuati hayo basi kutakuwa kuna namna ambavyo inatatakiwa mchukue hatua zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka nizungumzie ni suala la EWURA. EWURA mwaka 2018 niliweza kuchangia namna ambavyo wanaweza kusambaza ama wakatoa miongozo na kanuni, niwapongeze kwamba, sasa hivi wametoa miongozo na kanuni namna ambavyo hata vituo au magari ya kuuzia petroli ama dizeli yanaweza kufanya kazi, lakini baadhi ya maeneo ambamo hakuna petroli ama dizeli imekuwa ni changamoto kubwa sana na ukiwafuatilia watu wa EWURA wanakwambia kanuni zimekamilika, lakini utekelezaji ndio umekuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba suala hili waharrakishe watu wa EWURA. Maeneo yote ambayo hayana mafuta, hususan peripherals, sehemu ambazo hakuna petrol stations, basi watumie njia mbadala ya magari maalum ambayo yana mita na yanaweza yakafanya biashara hii na Serikali ikakusanya kodi yake na pia tukapunguza gharama za wale watumiaji ambao wanatumia mafuta ya kwenye vidumu na wanaua magari yetu, hususan pump huwa mara nyingi sana zinakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nataka nizungumzie suala la umeme kukatikakatika sana. Katika Jimbo langu la Busokelo kwa siku unaweza ukakatika umeme zaidi ya mara 24 na sababu kubwa sana ya kukatika umeme kule ni kwa sababu upepo, mvua pamoja na miti mingi sana, lakini mwaka 2018/19 Serikali ilichukua hatua za kuweza kufyeka miti yote kwenye line. Hadi magimbi ya chini walifyeka, lakini tatizo hili mpaka leo bado lipo.
Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu kwa Serikali, ikiwapendeza kwa sababu, maeneo yale ni mvua nyingi sana kwa mwaka mzima. Basi mjitahidi mje na solution ya kuwa na nguzo za zege, lakini pia ikiwezekana nyaya badala ya kupita angani zichimbieni chini ardhini kama wanavyofanya wenzetu wa nchi nyingine zilizoendelea; lakini zaidi Waziri mkija na wazo la kuwa na nguzo za chuma katika maeneo yote ambayo kuna changamoto ya kukatika-katika umeme kwa sababu za kijiografia ya hali ya hewa, basi hii itasaidia na kupunguza hii hali kwa sababu, umeme unapokatika Busokelo, Tukuyu, Rungwe, Ileje, Kyela, lazima hiyo line iwe affected kwa kukatika kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala hili la back-ups ama systems ama mifumo ya teknolojia kwa TANESCO. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ulichukua hatua kubwa mara baada ya mifumo kusimama ama ku-stop kwa sababu tu back-ups hazikuwepo.
Kwa hiyo, nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na kama mdau wa ICT inasikitisha sana kuona kwamba, systems zinakuwa developed, lakini wanakuwa hawana back-ups. Na back-ups hizi kuanzia sasa, kitaalamu ama kitaaluma, inatakiwa isiwe katika jingo hilohilo la mifumo ilipo inawezekana wakaziweka hata Mwanza, hata Mbeya, lakini zikafanya synchronization ili ikitokea pengine any catastrophe ama janga lolote basi zile back-ups ziweze ku-take off halafu mifumo iendelee kufanya kazi kuliko kama ilivyotokea hivi karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho nataka nizungumzie jambo moja, ni muumini wa energy mix na Serikali yetu inafanya kazi hii ya energy mix. Ninachotaka kusema kwamba, tunaweza tukafikiri zaidi ya hapa, kuna mifumo mingi ya umeme duniani kwa hivi sasa; ukienda Japan kuna mfumo unaitwa co-diffusion new hydrogen energy, mfumo huu ni off grid. Inawezekana kwetu sasa tunaweza tukaanza kuufikiria hata kama hatujaanza kuutekeleza, lakini ni mfumo wa kutoa umeme kwa bei nafuu sana pasipo kutumia gharama ya kusafirisha nyaya kama tunavyofanya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naamini kupitia Wizara yako Mheshimiwa Waziri unaweza ukafanya tafiti kupitia wataalamu wako kwamba, umeme utoakanao na hydrogen energy ukoje kwa maana ya off grid kwa sababu, una faida nyingi. Kwanza hakuna nyaya kama tunavyofanya sasa, kwa mfano kama hivi Dodoma tungekuwa na umeme wa kwetu, Iringa wa kwao, hivyohivyo kwa hiyo, ingepunguza hizi distances za kusafirisha umeme umbali mrefu, lakini kukatikakatika, lakini zaidi mfumo huu unarahisisha kupunguza mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na mwisho kabisa nishukuru sana Serikali kwa kutuletea umeme wa Lumakali ambao utazalisha Megawatt 222 katika Mkoa wa Njombe, Jimbo la Makete pamoja na Busokelo. Nina hakika utakuwa na fursa nzuri kwa Watanzania kwa ajili ya kuwekeza, lakini pia kwa ajili ya kuongeza katika uzalishaji wa umeme na viwandani hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa fursa, nikutakie kila la heri Mheshimiwa Waziri katika kutekeleza bajeti hii na mimi naiunga mkono asilimia 100 ili mkafanye zaidi ya hapa mlipofanya. Ahsante sana. (Makofi)