Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia katika Wizara hii ambayo kimsingi ndiyo inaakisi uchumi tunaoutaka. Kimsingi ndiyo inaakisi tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda kwa kiwango gani. Nishati ya umeme ndiyo inahitajika katika kuendesha viwanda lakini je tumewekeza kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, nimepitia Mpango uliopita wa Taifa wa Miaka Mitano ambao ilikuwa 2015 – 2020, tulikuwa na lengo kwamba tunavyofika 2020 tunahitaji kufikisha megawati zaidi ya 4,000 ambayo ni 4,600 plus; kutoka kwenye megawatt 1,500 kuja mpaka megawatt 4,000 plus. Sasa katika hii miaka mitano tumeweza kufika megawatt 1,600 plus ambayo ni ongezeko la megawatt kama 100.2 ambayo sasa ukii quantify kwenye percentage unakuta ni asilimia 2.1 au tumefeli kwa asilimia 97. Kwa hiyo, ni kweli kwamba hatujafanya vizuri kwa sababu kama tunahitaji uchumi wa viwanda ni lazima tuwekeze kwenye nishati ya umeme na hayo ndiyo yalikuwa malengo yetu ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kusaidia viwanda kuweza kutumia gesi asilia, kupitia TPDC tulikuwa tunaona mipango mizuri kwenye makaratasi na kwenye maelezo ya Mawaziri kwamba wanaenda kuunganisha viwanda Dar es Salaam na maeneo mengine ili waweze kutumia gesi asilia na wazo lilikuwa zuri sana. TPDC walikuja na mpango mzuri kabisa wa miaka mitatu na miaka mitano na wakaonyesha kabisa tutapata faida kiasi gani lakini ukweli ni kwamba kazi kubwa haijafanyika. Hata viwanda tu 11 ambavyo walijiwekea kwa Mkoa wa Pwani kwamba vitaunganishiwa nishati ya gesi asilia iweze kutumia hiyo nishati havijafikiwa; viwanda viwili tu wamemaliza kufanya uchambuzi na kila kitu lakini umeme wa gesi haujaanza kutoka. Kwa hiyo, naamini kwamba kama tunahitaji kufanya vizuri ni lazima nguvu iwekezwe TPDC kwa sababu gesi asili inabaki kuwa cheap lakini pia tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kulikuwa na mipango kabambe ya wakazi wa Dar es Salaam na mikoa mingine kuanza kutumia gesi asili majumbani kwamba watatengeneza miundombinu hizo gesi asilia sasa zianze kupatikana kwenye majumba ambapo itasaidia gharama kuwa chini. Waliweka pilot kwamba wataunganisha viwanda 1,000 na makazi 300 leo ni zaidi ya miaka minne hakuna kilichofanyika. Kwa hiyo, nadhani TPDC inahitaji kufanya kazi kubwa kama tunataka tuone mabadiliko kwa macho.

Mheshimiwa Spika, pia walieleza kwamba maeneo ya Kawe, Tegeta na maeneo ya viwanda yataweza kuunganishwa na umeme wa gesi asili lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika. Jambo ambalo limenisikitisha TPDC kuanzisha deposit ya mafuta kwamba wataweza kuwa wana-retain petroleum wakachukua zaidi ya milioni 675 wakakarabati tank Na. 8, walivyoanza kukarabati wakagundua kumbe gharama ya kukarabati ni kubwa kuliko kujenga upya wakaahirisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata CAG kwenye ripoti yake amesema haya ni matumizi mabaya ya fedha kwa sababu feasibility study ilipaswa kufanyika na kuona kipi kifanyike. Nadhani milioni 675 ni fedha nyingi sana. Hata hivyo, lakini bado lengo liko pale pale, naendelea kuishauri Wizara ni lazima tuimarishe TPDC na ifanye kazi kwa sababu tunaihitaji. Tayari tumewekeza vya kutosha katika gesi asilia hebu tuitende haki tutaona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze kwamba kuna kazi imefanyika na inaonekana imefanyika hasa kwenye suala nzima la REA. Mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa vimeunganishwa na umeme vilikuwa 2,018 lakini leo tunaongelea vijiji 10,018, ni kazi ya kuigwa. Hata hivyo, hakuna mafanikio yasiyokuwa na changamoto, kuna maeneo mengine kinahesabika kijiji kimeunganishwa umeme lakini ni wakazi 20 tu. Nadhani hapa changamoto inabaki kuwa namna ya kuunganisha umeme.

Nitoe ombi kwa Serikali kama inawezekana, kupeleka umeme vijijini tayari mmetumia gharama ya kutosha, mkandarasi yuko site anapaswa kuunganisha umeme kwenye majumba lakini watu hawako tayari kuunganisha umeme. Nadhani ile gharama ya Sh.27,000 ikiwezekana Serikali iibebe, iwaunganishie watu umeme halafu waanze kukatwa kwenye ankara zao, hapo tutaweza kuona matokeo ya kuunganisha umeme. Otherwise umeme utakuwa unafika kijijini watu hawawezi kuunganisha, ndiyo ushauri naoutoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye Halmashauri yangu ya Kyerwa. Sisi Kyerwa tuna vijiji 99, tunaipongeza kabisa Serikali vijiji vyetu 70 vina umeme, lakini bado tuna vijiji 29 havijapata umeme na REA sasa hii Awamu ya Tatu inaonyesha kwamba mtaunganisha vijiji 19, kwa hiyo vinabaki vijiji 10 ambavyo havijui hatima yake. Niombe sana Serikali hebu muiamini Kyerwa muwape umeme, haya ni maeneo ambayo yalibaki pembezoni, ni maeneo ambayo yamekuwa hayana maendeleo kwa mudu mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ni lazima tuangalie na umeme tunaopata, tumekuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme kiasi kwamba mtu anaona bora nisiwashe umeme kwa sababu itaenda kuniaribia kila kitu kwa sababu kila baada ya dakika tano umeme unakatika. Kwa hiyo, naomba nivitaje hivi vijiji, kuna Vijiji vya Rwakabunda, Kagu, Omswekano, Ibale, Muleba, Rwamashaju, Kishanda, Ruita, Kishanda, Rurama, Omkitembe, Ibamba, Ruko, Kitoma, Nshunga, Rushe, Kakerere, Nyamweza, Kitega, Bugara, Mugaba, Businde, Nyakasheni, Nyakatera, Kibale, Kigorogoro, Kijumbura, Mgorogoro na Mkombozi. Hivyo ni vijiji vyetu 29 ambavyo havijafikiwa na nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, vilevile nimeeleza kwenye muhtasari wangu kwamba bado vijiji vilivyowekewa umeme ni wakazi wachache sana wana umeme. Nikatoa rai kwamba hebu tubebe hii gharama na tuwe tunawakata kwenye ankara kidogokidogo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, hayo ndiyo nilitaka kuongea. (Makofi)