Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa rasilimali tulizonazo za watu, mazao ya biashara tukiamua kwa dhati, tunaweza tukapiga hatua kubwa hasa tukijipanga vizuri. Ndani ya miaka mitano tuliyofunga mkataba na waliotuchagua, fursa zipo tukiamua hasa kwa kuanza na viwanda vidogovidogo ambavyo tunaweza kuanza navyo. Ili kuvilisha viwanda vya kati na baadaye viwanda vikubwa, kinachotakiwa ni kuundwa kwa mazingira mazuri ya uwekezaji, katika miradi mbalimbali kutokana na jiografia ya nchi yetu. Miradi hiyo ndiyo itakayounda ajira kwa Watanzania walio wengi na hao ndiyo watakaokuza uchumi wetu.
Kama nilivyoanza hapo juu kuwa tunayo rasilimali yetu ardhi, siasa safi na wajasiliamali. Hivyo tukiwatumia vizuri wajasiliamali, tukawawezesha tukawawekea mazingira mazuri kwa kila eneo, kufuatana na uzalishaji wao hasa katika mazao yanayotokana na ardhi, mito, maziwa, miti, mifugo na kadhalika huko waliko, ile idadi ya vijana kukimbilia mijini itapungua. Hebu tuisome ile Sera ya Taifa ya Biashara ndogo, na viwanda vidogo na tuitekeleze kwa kuisimamia. Sote twajua kilimo ndiyo kinachotoa, mapato kwa watu waishio vijijini, tukiamua kuanzisha viwanda vidogo vijijini vitaleta mabadiliko chanya, katika uchumi wa nchi yetu. Hasa vijijini kwa mazao yetu kuongezewa thamani, badala ya mkulima kuuza mazao yao kama yalivyo, viwanda vidogovidogo vitatumika kuyasindika mazao hayo. Mfano badala ya kuuza mahindi vijijini viwe na mashine za kusaga na kukoboa unga badala ya kuuza mpunga wauze mchele uliofungwa katika pakiti ndogo za kilo moja, mbili au tano huko huko vijijini tayari kupelekwa mjini kwa walaji, badala ya kuuza karanga na alizeti kama zilivyokuwepo, na viwanda vya kukamua mafuta, badala ya kuuza matunda kama yalivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujengwe viwanda vya kukamulia juisi, viwanda hivi mbali na kuongeza thamani katika mazao hayo, vitaongeza ajira huko huko vijijini na itasaidia vijana kubaki vijijini. Serikali itambue uongozi katika ngazi za Wilaya, na Mikoa kushawishi wawekezaji katika maeneo yao kufuatia fursa zilizoko zitenge maeneo kwa wawekezaji kwa kuondoa urasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ile dhana ya kujitegemea ya ki-ujasiriamali nashauri Waziri wa Viwanda, awasiliane na Waziri wa Elimu ili kuingiza somo la ujasiriamali katika mitaala ya shule. Kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari, na katika mafunzo ya ufundi stadi, hii itasaidia kupanua elimu na matayarisho ya kazi ili kuongeza hali ya kupenda kuanzisha na kuendeleza ujasiliamali, ili kuwafanya vijana kubaki vijijini. Vijana wakifundishwa ujasiriamali kuanzia msingi, sekondari na katika mafunzo ya ufundi stadi, watabadili mitazamo yao watapenda kujiajiri tofauti na ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona nijikite hasa katika suala zima la ujasiliamali, huko vijijini ili kupunguza idadi kubwa ya vijana kuja mijini kutafuta kazi (ajira) ambazo nazo hapo naomba tujipange vizuri. EPZ tutazipata katika Wilaya zetu na Mikoa yetu, fursa zipo tukiamua na kila mtu akatekeleza na kutimiza wajibu wake ndani ya muda mfupi tutapata matokeo chanya na tutabadilisha maisha ya vijana na kuinua uchumi wa nchi yetu Tanzania. Naomba niwaombe wataalam wote wa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara yako wafanye kazi kwa kuzingatia weledi wao, tuangalie wapi tulikosea na tuparekebishe na tusonge mbele kwa ari mpya. Ili ile ndoto ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli na Watanzania kwa ujumla, Tanzania iwe nchi ya viwanda ili tuweze kuzalisha kwa matumizi ya ndani na baadaye tusafirishe nje ya nchi ili tupate pesa za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongeza ajira na vijana wetu waweze kubaki katika maeneo yao ya uzalishaji, Mheshimiwa Waziri tulikuwa na viwanda vingi sana kabla ya kubinafsishwa ningependa kujua ni jinsi gani agizo la Mheshimiwa Rais umelitekeleza. Hasa kwa wale waliojitwalia viwanda na kuvitelekeza mbali na kwamba hadi leo hawajalipa pesa zote kufuatia na mkataba wa mauziano (MOU), ni hatua gani umezichukua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha nguo, kiwanda cha zana za kilimo asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima wa pamba, nyuzi, matairi, korosho, kahawa, asali, nyama na kadhalika, ni kichocheo cha upatikanaji wa ajira fedha za kigeni lakini nchi yetu itaitwa nchi ya viwanda. Nchi haiwezi kuitwa nchi ya viwanda wakati viwanda vilivyopo havizalishi katika uwezo wake na havizidi 200-500 tunakuamini Mheshimiwa Waziri, lakini tunakuomba ukaze buti wewe na Wataalam wako, ndiyo mtaifanya nchi hii kuitwa nchi ya viwanda. Ushirikiano na Wizara zingine nchini hii ni kutokana na kutegemeana. Pia chuo chako cha CBE Dar es Salaam nilichosoma mimi kitazamwe upya, elimu inayotolewa pale ni tofauti na zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.