Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muda ulionipatia ili niweze kuzungumzia changamoto ambazo zinawakumba wananchi wa Nkasi Kaskazini. Kutokana na umuhimu wa Wizara hii nitachangia mambo machache kwa kuwa mengi yamefanyika.

Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kuhusiana na namna ambavyo Waziri pamoja na Naibu wake na Cabinet yote wanavyowajibika kwenye nafasi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mazuri ambayo mnayafanya hasa kupitia miradi ya REA bado kuna changamoto kadhaa. Changamoto ya kwanza, kutokana na ukubwa wa hii miradi ambapo imesambaa maeneo mbalimbali TANESCO wanakabiliwa na changamoto ya usafiri. Kama tunavyoona kuna mambo mazuri mmeyafanya lakini bado kuna changamoto kwenye uzuri wake wa jambo hilo la usafiri. Kwa hiyo, kwa sababu Serikali ina nia njema kuwafikishia wananchi huduma ya umeme, basi tuone namna bora ambayo tunaweza tukaifanya ili hawa TANESCO waweza kuwajibika inapotokea changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la REA, naungana na Wabunge wote ambao tumekwenda kufanya research ya kutosha na Mheshimiwa Waziri anajua tumekwenda Manyara, Singida na maeneo mengine, wakisema wamepeleka umeme kijiji fulani utakuta watu wachache tu ndiyo wamepata lakini lengo la Serikali ilikuwa wananchi wote sio wachache. Kwa maana hiyo turudi kwenye lile lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma hii ya umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini katika tafiti chache ambazo nilizifanya kwenye Kamati yetu ya PAC tulivyozunguka si kwamba wananchi hawataki kupata huduma ya umeme au hawataki umeme majumbani mwao, kuna watu ambao hata hiyo Sh.27,000 ni changamoto. Sasa kama lengo ilikuwa ni hilo na tumeingiza fedha za kutosha ili kupeleka miradi, kwa nini Serikali isibebe jukumu hilo la kuchukua hiyo Sh.27,000 wananchi wakapelekewa huduma na wakaanza kukatwa taratibu taratibu kulingana na huduma ambazo wanazipata? Naamini wananchi wengi watafurahia jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hizo, katika Jimbo langu lenye vijiji 49 vijiji 9 havina huduma ya umeme kabisa. Vijiji hivyo ni Itindi, Sentamapufi, Lyele, Matine, Mienge, Mpenge, Kalila pamoja na Mkombe. Natambua kwamba kuna maeneo ambayo jiografia yake ni ngumu kama Jimbo langu, kuna vijiji ambavyo unavuka ziwa ndio unakwenda pembeni unawakuta wananchi na wale wananchi wanajishughulisha na uvuvi na leo tunasema kwamba waende kwenye viwanda lakini umeme haujafika. Kwa hiyo, bado wanaendelea na uvuvi uleule kama tunavyosoma historia ya Yesu walivyokuwa wanavua ukishapita muda fulani hawajauza samaki wale wanaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe Serikali kwa kuwa lengo ni jema pia tuangalie yale maeneo ambayo yana umuhimu zaidi. Natambua kwamba wote wanafanya kazi na wanahitaji kupewa umeme, kuna wengine wanatumia kwa ajili ya mwanga peke yake lakini tunatazama miradi hii ya REA namna ambavyo itasaidia pato la Taifa kwa wananchi kuweza kuendelea na majukumu yao kupitia suala la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia kukatika kwa umeme na hili ndilo limenifanya nisimame hapa. Wilaya ya Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla umeme unakatika isivyo kawaida. Imefikia mahali kwa sababu watu walisahau vibatari na taa lakini wanaona ni bora walikuwa wakiweka mafuta kwenye taa anajua haya mafuta niliyoweka yatanitosha mpaka kesho nitaweza kununua mafuta mengine lakini leo umeme umekuwa haueleweki yaani unaweza ukakatika zaidi ya mara saba. Mheshimiwa Waziri na sisi watu Nkasi ni Watanzania; kuna wafanyabiashara, kuna wamama kule wameamua kutengeneza juisi na vitu vingine, tungependa kujua tatizo ni nini. Pamoja na kwamba umeme unapokatika wenye wajibu wa kutoa taarifa ni TANESCO kwamba kwa nini umeme umekatika na utarudi baada ya muda gani lakini mambo haya hayafanyiki na ni mazoea tu ambayo yanaendelea. Sasa hawa wananchi kwa sababu hii ni huduma tunahitaji basi kuwajibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye jambo hili naomba pia Kitengo cha Emergency, kama neno lenyewe emergency bado kuna changamoto hakuna emergency tena sasa hivi. Ni vizuri tukaboresha kitengo hicho kiwe emergency kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa navyozungumza Kata za Kalando na Itete toka jana mchana mpaka leo wako gizani. Sisi tupo mpakani mwa Congo na Burundi amani ya nchi yetu inakuwaje kama watu wako gizani? Ni lazima tuwape kipaumbele watu wa mipakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijasimama hapa kuchangia nimeongea na Meneja wa TANESCO anasema ni tatizo la nguzo kuungua toka jana, ni vizuri tukaboresha kitengo hiki. Kama lengo la kupeleka REA ni kuwahudumia wananchi basi tuboreshe na hivyo vitengo maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)