Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Waziri wa Nishati. Kusema kweli na mimi niungane na wenzangu waliotangulia kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo imeendelea kufanyika toka aliposhika Wizara hii. Hii inonesha kabisa kwamba katika kipindi kifupi kwa maana baada ya mwaka mmoja nchi nzima ya Tanzania itakuwa imepata umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nijielekeze tu kwenye Jimbo langu la Musoma. Mheshimiwa Waziri anafahamu, bahati nzuri nilimwalika na alikuja Musoma na tukawasha umeme kwenye Mtaa wa Bukoba. Baada ya kuwa tumewasha umeme Mtaa wa Bukoba pale pale akatoa agizo kwamba kuanzia sasa kwenye maeneo yote ya pembezoni yatapata umeme. Naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri toka alivyotoka, lile eneo la pale Bukoba hawajapata umeme zaidi ya ule aliowasha. Mitaa ya Nyabisale, Songambele, Kwangwa A, Kwangwa B, Mugalanjabo, Zanzibar, Bukanga hivi ninavyozungumza hawajapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Waziri amechukua hatua za kuzungumza na Meneja wa TANESCO na akamuagiza, bahati mbaya tu sasa hivi hayupo Mwenyezi Mungu amrehemu lakini hilo tatizo kwangu ni kubwa. Nadhani mwezi uliopita Naibu Waziri Mheshimiwa Byabato alikuja Musoma aliweza kushuhudia alikaa mpaka na Wenyeviti wa Mitaa wanamweleza hali ya umeme ulivyo wa shida pale Musoma Mjini.
Mheshimiwa Spika, TANESCO tunapowauliza wao wanasema hivi, ni mita 30 toka pale nguzo ilipo kulia na kushoto zaidi ya hapo hawatoi umeme. Kikubwa zaidi TANESCO kila tunapowauliza wanasema hawana bajeti sasa Mheshimiwa Waziri leo ataniambia nini kwa sababu kwenye vitabu hata kwenye ile miradi ya Peri-Urban sisi Musoma hatumo, sasa endapo Musoma hatumo na TANESCO wanasema hawana bajeti yetu tunafanyaje? Waziri ametangaza hapa kwamba hakuna mwananchi kulipia nguzo sijui wale watu wa Musoma watafanyaje. Naomba baada ya Bunge hili tukubaliane kwamba tukishaahirisha twende wote akawaambie kwamba ndugu zangu ile ahadi aliyotoa kwamba watu wa Musoma watapata umeme wa Sh.27,000 haipo badala yake walipie tu zile gharama za kawaida za shilingi laki tatu na kitu tofauti na hapo tutaendelea kuonekana sisi wengine ni waongo.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri labda atoe maelekezo ili fedha ziweze kupatikana kwenye maeneo kama haya ya Peri-Urban kama ambavyo imetokea kwenye mikoa mingine na ameweza kuonesha ili na sisi watu wa Musoma tuweze kupata umeme. Faida za umeme kila mmoja anazifahamu na kwa sababu watu wetu sasa walishajua kwamba umeme wa Sh.27,000 unakuja kila siku inaonekana mimi Mbunge ndiye ninayewakwamisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Waziri aangalie fedha zile zinazokwenda kwenye mfuko wa REA ziweze kwenda kwa Mameneja wa TANESCO wa Mikoa ili zile ahadi ambazo Serikali inazitoa basi iweze kuzitekeleza. Kusema kweli pamoja na kazi kubwa na nzuri ambayo imeendelea kuonekana lakini kwetu sisi wengine hali si shwari kabisa. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba atakapokuwa anajibu basi suala la Musoma asiweze kulisahau.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa sababu ya muda naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)