Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa dhati kabisa lakini nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii ya Nishati. Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Naogopa kusema hapa mimi binafsi au labda kwa sababu ndugu yetu huyu ni Msukuma tabia ya unyenyekevu hii kwake yaani ni ya ajabu kwangu ana unyenyeku uliopitiliza. Wapo waliosema hapa lakini mimi binafsi nasema tu kwamba katika Mawaziri ambao wanaofanya kazi vizuri, kaka yangu Mheshimiwa Kalemani Mungu akubariki sana, umejitoa na unafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitagusa kidogo kwa habari ya TPDC. Shirika hili la Maendeleo ya Petrolini nchini lilianzishwa mwaka 1969 kwa Amri ya Rais chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma (Public Corporation Act). TANESCO wamefanya kazi vizuri sana na wanaendelea kufanya kazi vizuri lakini TPDC nilikuwa najaribu kufanya hesabu hapa huyu mtu aliyezaliwa mwaka 1969 sasa ana miaka 52. Pamoja na mambo mengine inayofanya TPDC hoja yangu ya msingi mpaka leo tunaendelea kufanya tafiti za mafuta miaka 52.

Mheshimiwa Spika, Adolf Hitler mwaka 1945 wakati anakwenda kupigana Vita ya Pili ya Dunia German-Austria pale Linz aliwaita wahandisi akasimama na kusema; nakwenda kupigana vita jangwani nahitaji kupata mashine inayotumia air cooling system akawapa siku saba. Ilikuwa wachague moja, ama awapige bastola ndani ya siku saba wakishindwa kazi hiyo au wagundue mashine ambayo itatutumia air cooling system. Ndani ya siku saba wahandisi wale wa Ujerumani walikuja na majibu ya air cooling system. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, akili ya mwanadamu ilivyo ukiiacha iwe huru inazubaa. Mwanadamu siku zote anataka kusumbuliwa. Ukimtia upepo kidogo anashtuka ndiyo maana hata wakati ule sisi tunasoma darasa la saba ukipigwa fimbo kesho hiyo table unaishika vizuri sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri moto ule ule aliotumia TANESCO aupeleke TPDC. Waziri aende TPDC akawaeleze…

T A A R I F A

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa.

MHE. CHARLES J.P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe Taarifa Mheshimiwa Chifu Kunambi kwamba kwa vigezo na uzoefu wa kutafuta mafuta TPDC haijawezeshwa na haiko kwenye viwango vya kutafuta. Ndiyo maana jana nikawaambia kwamba Uganda 2002 - 2015 walikuwa wamechimba visima 11 ambayo ni confirmatory test ya kutafuta mafuta ilhali Tanzania TPDC wanatuambia wamechimba visima vitatu pale juu, sio namna hiyo.

SPIKA: Mheshimiwa Kunambi, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, naipokea Taarifa hiyo lakini bado niendelee kusisitiza tu kwamba Mheshimiwa Waziri sisi Wabunge nadhani kila mmoja hana mashaka na wewe na tunakuombea Mungu aendelee kukubariki na Mheshimiwa Rais aendelee kukuona hivyo hivyo na sisi uendelee kutuhudumia kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine namuomba Waziri atusaidie kuhusu gharama za umeme hasa kwa sisi wananchi tunaoishi vijijini. Ni kweli tumekupongeza, unafanya kazi nzuri lakini hii gharama ya Sh.27,000 tafsiri yake kidogo hebu itazame Mheshimiwa Waziri ni pale ambapo kuna nguzo ya umeme na kuleta umeme kwangu au ni pale ambapo unatakiwa kuvuta nguzo nne au sita? Hili kidogo liwekwe sawa.

Mheshimiwa Spika, kwa mwananchi wa kawaida kabisa wa kijijini ukimwambia alipie hizo nguzo sita mpaka kwenye nyumba yake ni vigumu sana. Jana mimi nilipata meseji tatu za wananchi wangu wanaomba niwachangie laki moja moja nao walau wapate umeme. Kama Mbunge sijui utachangia wangapi wananchi zaidi ya 100,000.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie ufafanuzi anapokuja kuhitimisha hotuba yake jioni ya leo atueleze kuhusiana na suala hili. Watanzania hasa wananchi wa Jimbo la Mlimba wangependa kufahamu gharama hii ya Sh.27,000 inazungumzwa vipi? Ni kuvuta umeme kutoka kwenye nguzo au kuongeza nguzo? Mimi nyumba yangu inahitaji nguzo sita, saba au nane bei hiyo inahusika pia? Kama hoja itakuwa tofauti na hiyo Mheshimiwa Waziri mtusaidie namna gani mnakwenda kama Wizara sasa kufikiri na kutafakari juu ya kupunguza gharama hizi ili kumpunguzia mzigo Mtanzania huyu hasa wa kipato cha chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nimemshukuru kwa dhati kabisa na mimi kwangu bahati nzuri tuna mradi ule wa umeme pale Kihansi na tulikuwa tunashuhudia tu umeme unapita unakwenda Dar es Salaam na maeneo mengine leo hii Mheshimiwa Waziri amekwenda kukamilisha pale Mlimba vijiji 11 vilivyobaki, nakushukuru na nakupongeza sana. Hoja inayobaki kwa wananchi wa Jimbo la Mlimba pamoja na kwamba tunakwenda kukamilisha vijiji hivi 11 je, umeme huu utafika kwenye maeneo muhimu kama vile shule, vituo vya afya na zahanati? Haya ni maeneo muhimu sana kwa sababu utaona umeme unapita kwenye njia tu lakini taasisi muhimu kama hizi hazina umeme.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba niunge mkono hoja na Mungu aibariki Wizara hii muhimu. Ahsante sana. (Makofi)