Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na kunipatia fursa hii angalau na mimi niwasemee wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini kuhusiana na suala hili muhimu sana la nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara na hasa Waziri Kalemani kwa usikivu wake mwingi sana tunapokuwa tuna mahitaji kwake, tukiwa na shida mbalimbali kwa kweli, amekuwa msikivu na anatusikia. Namuomba aendelee kuwa mnyenyekevu na asipandishe mabega. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie mambo machache matatu makubwa, umeme wa REA, umeme wa upepo Mkoani Singida na ule umeme mkubwa unaotoka Namanga – Arusha – Singida. Kwa upande wa REA, kata zangu tano hadi sasa hazijaguswa kabisa na umeme hata nyumba moja zinakaa gizani, lakini unakuta kata imezungukwa, wamegusagusa kwenye centres za kata lakini maeneo ya jirani yameachwa.

Mheshimiwa Spika, mathalani Kata ya Ughandi yenye Vijiji vya Senenemfuru, Laghane, Damisinko, haijaguswa hata kidogo. Upande wa huku Msisi angalau wameguswaguswa upande wa Mashariki Ntinko, kuna baadhi ya maeneo yameguswa, lakini kata iko katikati kwa nini hata vijiji vya jirani visipate umeme?

Mheshimiwa Spika, Kata ya Itaja ambayo iko barabara kuu, Arusha Road, vijiji vyake hata kimoja havijapata umeme, lakini kuna vijiji vya jirani ambavyo vina umeme. Kwa nini sasa wasingekuwa wanaunganisha vijiji kulingana na jiografia?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe Vijiji vya Ngimu, Bohama, Mbwighanji, Lamba, Kinyagigi, Makuro, Mkenge, Matumbo, Poku, Ghalunyangu, Mwalala, Migugu, Minyenye, Ikiu, Mwarufyu, Mdhae, Mwasauya, Sefunga, Ndwamoghanga, Unyampanda vipatiwe umeme. Nashukuru kwamba tumepatiwa huyu mkandarasi at least tunapata matumaini na wananchi wetu wanapata moyo, wamefurahi sana; nimewajulisha kwamba, tumepata mkandarasi sasa mtulie umeme unakuja utekelezaji basi uwe ni ule ambao tunautarajia. Naomba hawa wakandarasi wawasikilize viongozi wanapowaelekeza anzieni hapa, wawe wasikivu sio wawe miungu watu, watusikie tunapowaomba at least yale maeneo ya vipaumbele wayafanyie kazi. Naomba haya malalamiko sasa yasirudierudie tena kwa sababu umeme ndio maisha ya Watanzania, umeme ni uchumi. Tunataka twende kwenye uchumi wa viwanda, utawezekanaje bila umeme? Vijana wetu wana shughuli mbalimbali zinazohitaji umeme, kuchomelea, kunyoa, watafanyaje hizi shughuli bila umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikirudi kwenye umeme wa upepo Mkoani Singida, mradi huu una miaka zaidi ya sita hivi sasa na mkandarasi alishaweka kila kitu chake pale field lakini hadi sasa ameshindwa kupewa go ahead ya kuendelea kutekeleza mradi huu na unapita katika vijiji nane vya jimbo langu. Niombe sasa Waziri atakapokuja hapa ku-wind up atupe commitment ya kuanza kwa mradi huu ili angalau wananchi wa vijiji vile nane wapate matumaini ya kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa huu umeme mkubwa unaotoka Namanga – Arusha – Singida, una Kilowatt 2000 ni umeme mkubwa ambao ungeweza kuondoa kabisa tatizo la umeme nchini lakini hadi sasa hatujajua muendelezo wake unakuwaje. Kwa hiyo, niombe pia Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa atupe commitment kuhusu eneo hili ili tupate umeme kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, nimuombe Mheshimiwa Waziri, mimi ninayeongea hapa Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini nakaa gizani umeme hamna nyumbani kwangu, Waziri haoni aibu? Nimeshamueleza mara kadhaa, nimeshamueleza hata DG wa REA, Meneja wa Kanda hata wa mkoa wameshindwa kunisikiliza. Jamani, sasa kama Mbunge hasikilizwi mwananchi wa kijijini kule ataweza kusikilizwa? Naomba kuwasilisha. (Makofi)